Hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere aliyoitoa tarehe 2 Novemba, 1978 alipokuwa akitangaza vita vya kupambana na uvamizi wa majeshi ya Idd Amini katika ukumbi wa Diamond Jubilee
Ndugu wananchi,
Nimewaombeni tukusanyike tena hapa niwalezeni jambo ambalo kwa sasa wote mnalijua, lakini nadhani si vibaya nikieleza. Nitajitahi kueleza kwa kifupi. Wakati nilipokuwa katika ziara kule Songea juma la pili la mwezi uliopita, ilitangazwa habari kutoka Uganda kwamba Jeshi la Tanzania limeingia Uganda, kwamba limechukua nafasi hiyo sehemu kubwa ya Uganda, na linaua watu ovyo. Siku hiyo ulipotangazwa uwongo huo nilikuwa nimealikwa kwenye chakula na vijana wetu wa Jeshi la Wananchi pale Songea. Kwa hiyo nikachukua nafasi hiyo kukanusha uongo huo, na kwa kweli kuwalaumu hao waliozua uwongo, na pia kuvishutumu vile vyombo vya habari duniani ambavyo vinapenda sana kutangaza- tangaza uwongo wa Amini. Amin hutamka la uwongo, na hurukia na kutangaza kana kwamba ni kweli. Huo ndio ulikuwa uwongo wake wa kwanza, na kuendelea.
Baadaye akabadili sura ya uwongo huo, akaongeza uwongo wa pili; kwamba Watanzania hao bado wapo Uganda wanapiga watu huko, wanaua watu huko na sasa wanasaidiwa na wanajeshi wa kutoka Cuba. Huo nao ulikuwa ni uongo, tuliendelea kuukanusha na kupuuza. Kwa kweli tulikanusha na kuupuza uwongo mzima.
Lakini Alhamisi iliyopita , saa za asubuhi, ndege za kivita zikaja. Vijana wetu wakazitupia risasi zikarudi. Vijana wetu wakazitupia risasi tena zikakimbia, lakini moja ikaangushwa. Ijumaa zikaja ndege za kivita katika eneo la Kyaka. Zikatupa mabomu. Vijana wetu akazitupia risasi, mbili zikaangushwa.
Wakati huo huo bahati mbaya ndege zetu nyingine nazo zilikuwa zinatoka hapa zinakwenda Mwanza. Kwa bahati mbaya katika hali ya giza, zikakosea katika kutua kwenye kiwanja cha Mwanza. Zikataka kujaribu tena. Lakini ndege zinakwenda kasi sana, na ili ziweze kugeuka Musoma. Na katika maeneo yale tangu Idd Amini alipoanza kutangaza uwongo, ingawa tulikuwa tunapuuza ule uwongo, lakini hatuwezi kupuuza yote: kwa hiyo vijana wetu walikuwa wameshaambiwa ndege za vita zikionekana zipigwe. Kama zile za Bukoba zilivyopigwa, na za Kyaka zilivyopigwa, hizi nazo, kwa bahati mbaya, zilipofika Musoma wakadhani ni adui. Zikapigwa. Tukapoteza ndege tatu. Lakini katika mambo ya vita ajali zinatokea. Vijana hao walikwisha ambiwa zikionekana ndege wapige. Wangeziacha anajuaje pengine ni za adui. Kwa hiyo ikatokea bahati mbaya hiyo.
Matukio hayo hatukuyatangaza. Hata kule kupiga ndege za Amin hatukutangaza. Hatukutangaza kwa sababu hatukutaka jambo lenyewe kulipa uzito mno. Tulisema akiendelea- endelea kuleta hizi ndege zake tutaendelea kuziaangusha. Yeye ataendelea kuongopa, lakini hizi ndege tutaziangusha kila zinavyokuja. Uwezo wa kuangusha upo na mwenyewe alijua kwamba uwezo upo na ni vizuri akujua yeye.
Tulikuwa tunaepuka kulipa uzito mno jambo hili kwa sababu mwanzo wake ni uwongo kabisa kwa kuzua. Kwa hiyo uwongo wake ukaendelea na tukazidi kuukana, na haya matukio ambayo yalikuwa ni kweli nasema hatukuyatangaza kwa sababu hiyo niliyoisema.
Sasa Jumatatu ndipo akavamia nchi yetu. Akaagiza majeshi yake kwa nguvu kubwa yakachukua sehemu kubwa, yakaingia ndani mpaka Kyaka. Hili tulilitangaza, kwa sababu ilikuwa ni jambo la kweli. Yeye, kama kawaida yake, akakana, akasema haikutokea hivyo. Akaenda kusema tu kwamba Watanzania wao ndio wako Uganda wamechukua sehemu za Uganda. Amin akakana, akasema haikutokea hivyo. Akaendelea kusema tu kwamba Watanzania wao ndio wako Uganda wameachuka sehemu ya Uganda. Amini akakana ukweli huo, lakini sisi tukawaeleza Mabalozi walioko Dar es Salaam kwamba huyu mtu amevamia nchi yetu. Sasa jana ametangaza mwenyewe: kwamba ni kweli majeshi yake yamevamia nchi yetu, na kwamba amechukua sehemu hiyo ya Tanzania iliyo kaskazini mwa Mto Kagera, na kwamba tangu sasa eti sehemu hiyo ni ya Uganda na itataliwa kijeshi kama Uganda na inavyotawaliwa. Ndivyo alivyotangaza mwenyewe. Sisi ametusaidia katika kutangaza jambo hilo kusudi sasa ubishi uishe, tusiwe tena na tatizo la kuwaambia watu wenye akili duniani ni nini kimetokea. Sasa hiyo ndiyo hali, tufanye nini?
Tunayo kazi moja tu, Watanzania sasa. Ni kumpiga. Uwezo wakumpiga tunao. Sababu ya kumpiga tunayo. Na nia ya kupiga tunayo. Tunataka dunia ituelewe hivyo kwamba hatuna kazi nyingine, na tunawaomba marafiki zetu wanaotuambia maneno ya suluhu waache maeneo hayo.
Kuchukua nchi ya watu wengine makusudi siyo kwamba majeshi yamekosea njia, na kusema sasa sehemu hiyo mmeichukua ni kutangaza vita na nchi ile nyingine. Lakini siyo sisi tuliofanya hivyo. Amefanya hivyo mwenda wazimu. Amefanya hivyo katika jambo ambalo amewahi kulitangazia zamani. Aliwahi kusema zamani kidogo kwamba mpaka wa haki wa Uganda na Tanzania ni Mto Kagera na siku moja ataichukua. Ametimiza dhamira hiyo. Sasa rafiki zetu kama ni marafiki wa kweli, watataka tumwondoe mtu huyu. Hawawezi kutuomba suluhu, au kutuomba jambo la jabu kabisa la kurudisha majeshi yetu nyuma. Niyarudish e wapi? Kwa hiyo ninasema tunayo kazi moja.
Ssis hatukupenda kufanya hivi; hatukupenda kupigana vita. Maadui wetu ni mabeberu, kwa sasa hivi wako Kusini. Serikali za Afrika hata tunapokuwa hatupendi vitendo vya viongozi wao, hatuwezi kuwahesabu kama ni adui wetu. Na kama Amin angekuwa anasema kwamba Tanzania ni adui sisi tungeendelea kumpuuza kama ni maneno tu. Lakini kafanya hasa kitendo cha uadui. Amekuja mwenyewe, ameingia Tanzania mwenyewe. Mtu huyu ni mshenzi, ameua watu wengi sana. Kwa hiyo nasema tunayo kazi moja. Tutampiga.
Vijana wetu wako mpakani sasa hivi, wako kule; mapambano yanaendelea. Sasa haya si mapambano ya T.P.D.F ; ni yetu wote. Kwa hiyo ninchowaombeni wananchi wote kwanza ni hiyo kazi iliyo mbele yetu. Pili, tuwasaidie vijana wetu, kila mtu kwa mahali alipo. Na kila mapambano yatakavyoendelea, tutaelezea nini cha kuifanya, na nani afanye nini. Tutawaeleza wakati wote wakati tunamwondoa huyu nyoka katika nyumba yetu.
Tunawaomba mtulie. Katika mambo haya ya vita, na hasa kama watu mlikuwa na mazoea ya amani , manaweza kubabaika sana. Masibabaike; tulieni. Fanyeni kazi kama kawaida. Eleweni vitendo tutavyovifanya; na mataviona vitendo tutakavyovifanya; na mpaka hapo kazi itakapokuwa imekwisha. Lakini mjue vitendo hivyo kazi yake ni hiyo moja; kumpiga mshezi huyu aliyekuja katika nchi yetu.