Kampuni yachukua eneo lote, wakosa hata pa kusimika Bendera ya Taifa

Wakabiliwa na madeni, wakosa uwezo kuwafikia wanachama 

Chama cha Maskauti wa Kike Tanzania (TGGA) kimo katika hali mbaya huku kikikabiliwa na madeni makubwa yanayodaiwa kusababishwa na uwekezaji mbovu uliofanywa miaka kadhaa iliyopita. 

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hata eneo lililokuwa likimilikiwa na kutumiwa kama makao makuu ya chama hicho kwa miaka mingi, ama limo hatarini kuchukuliwa na mwekezaji au tayari limekwisha kuchukuliwa kutokana na aina ya mkataba wa ubia huo unaotia shaka. 

Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya TGGA kinasema mdororo huo umetokana na ubia ulioingiwa kati ya uongozi wa zamani na kampuni iliyotajwa kwa jina la Jeferji Developers Limited (JDL) ambayo kwa sasa inatumia rasilimali za chama kwa masilahi yake. 

“Hayo yalifanyika mwaka 2010 kwa lengo la kuendeleza kiwanja Na. 1088 CT 186169/40 yalipo Makao Makuu ya chama Mtaa wa Kibasila, Upanga Mashariki, jijini Dar es Salaam. Moja kati ya vipengele vilivyomo kwenye ubia huo ni mgawanyo wa asilimia 74 kwa 26 kati ya JDL na TGGA,” anasema mtoa taarifa wetu ndani ya TGGA.

Awali, TGGA ilikuwa na uwezo wa kifedha kutokana na rasilimali zake, ikijitegemea na kuwafikia wanachama wote nchini lakini sasa imepoteza mwelekeo huku ikikabiliwa na madeni makubwa na kupungukiwa wanachama.

Lengo la ubia lilikuwa ni kuendeleza eneo hilo kwa kujenga majengo zaidi ya mawili, lakini katika hali ya kushangaza hati halali ya kiwanja ilibadilishwa na kuwa CT Na. 119338 ikimilikiwa na JDL. JAMHURI linazo nyaraka hizo. 

Majengo yaliyoendelezwa katika eneo hilo ni Towers (minara) A, B na C; kwa pamoja yakijulikana kama ‘Girls Guides Tri Towers’ ingawa zipo taarifa za mipango ya kuyabadili jina na kuwa ‘Maria Nyerere Complex’.

“Mgawanyo wa asilimia 74 kwa 26 si sahihi na bado mwekezaji anatunyanyasa hata kwenye hiyo asilimia 26 ya sehemu ya ndani ya ‘Tower C’ aliyotupatia. Yeye amejimilikisha ghorofa ya 13 na sehemu ya ghorofa ya 14 akidai asilimia yetu 26 inaishia ghorofa ya 12 tu,” anasema ofisa huyo. 

Ofisa mwingine anadai JDL walichelewa kukamilisha ujenzi kwa makusudi ukiwa ni mpango wa kupora umiliki wa TGGA wa eneo hilo huku pia wakijenga hata eneo lisilokuwamo kwenye mkataba.

Kitendo hicho, kwa mujibu wa maofisa wa TGGA, kimesababisha chama kukosa hata sehemu ya kupandishia Bendera ya Taifa. 

JAMHURI linafahamu kuwa uendelezaji wa eneo hilo ulioanza Mei 6, 2010, ulitarajiwa kutumia miaka mitatu na kukamilika Mei 5, 2013, badala yake jengo hilo lilikabidhiwa Februari 2018; takriban miaka minane tangu ujenzi ulipoanza.

“Makubaliano ilikuwa pamoja na kuendeleza, libaki eneo la wazi kwa ajili ya kambi za Skauti wa Kike na maegesho ya magari,” anasema ofisa mwandamizi wa TGGA.

Katika makubaliano ya awali, JDL walikubali kuwapa TGGA Sh 20,000,000 kama gharama za kuhama, pamoja na Sh 15,000,000 kila mwezi hadi ujenzi utakapokamilika. 

Hata hivyo, fedha kwa ajili ya kuhama hazijawahi kutolewa, badala yake yamekuwapo madeni ya ajabu ajabu yanayojumuishwa kwenye fedha zilizokuwa zikitolewa kwa TGGA kila mwezi kwa miaka minane ya ujenzi huo.

Na sasa nyaraka za JDL zinaonyesha kuwa anakidai chama Sh 731,000,000 alizotumia kununua samani za ofisi ya TGGA na Sh 65,000,000 alizotoa kwa wadhamini Februari 2018 alipoikabidhi bodi majengo hayo. 

“Ununuzi wa samani hizo si halali, kwani haukufuata utaratibu wa kisheria. Ametuwekea masharti kwamba hatupaswi kudai chochote hadi atakapomaliza madeni yake yote aliyoyathaminisha hadi kufikia Sh bilioni 1.7, akisema hiyo itamchukua miaka 10 hivi. 

“Tathmini iliyofanywa na wataalamu wetu imebaini kuwa samani alizotununulia hazilingani na fedha anazodai,” zinadai taarifa kutoka ndani ya TGGA.

Mwaka 2018, uongozi wa TGGA uliitisha Mkutano Mkuu ulioamua kuvunja Bodi ya Wadhamini iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti Anna Abdallah, uamuzi uliolenga kuokoa ‘mali za mtoto wa kike’ wa Tanzania. 

Kabla ya kuvunjwa kwa bodi hiyo, tayari mwenyekiti na makamu wake walikuwa wamekwisha kujiuzulu kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa mkataba wa uwekezaji wa JDL ulioingiwa kabla wao hawajashika nafasi hizo. 

Bodi mpya iliapishwa Oktoba 12, 2018 na kupitia mikataba ya tangu mwaka 2010 na kubaini uvunjaji wa katiba ya chama na ukiukwaji wa taratibu za kiutendaji ndani ya taasisi hiyo. 

Bodi ilibaini pia kwamba JDL imeipa mamlaka kampuni iitwayo Mohamed Builders Limited ya kupangisha na kuendesha jengo la TGGA kinyume cha mkataba. 

Jitihada za bodi kuokoa mali za TGGA ziligonga ukuta, hivyo uongozi ukaamua kupeleka kilio chao kwa mlezi wa chama, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, aliyeshauri Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali itumike kujiridhisha namna kila mmoja anavyonufaika na uwekezaji huo kwa mujibu wa makubaliano. 

Mwanasheria wa JDL, Nixon, ameliambia JAMHURI kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kwani limo mikononi mwa CAG.

“Mambo yetu yalipelekwa kwa CAG, hata jana (mapema mwezi huu) walinipigia simu nikiwa Dodoma wakitaka kukagua nyaraka. Sasa CAG bado hajalitolea uamuzi, mimi ninaweza kuzungumza nini hapo?” anasema Nixon akisisitiza kuipa nafasi Ofisi ya CAG kutoa uamuzi stahiki. 

Kamishna wa TGGA Manispaa ya Kinondoni, Cecilia Shao, anasema mgogoro huo uliwahi kufikishwa kwa Mama Salma Kikwete (mke wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete) alipokuwa mlezi wao mwaka 2014, akawahoji waliouza eneo hilo wakabaki kimya. 

“Alikasirika sana. Akasema anajitoa. Hataki kushirikiana na waovu. Tulimsihi asijitoe, akakubali kuendelea kuwa mlezi na kuwaambia viongozi waliohusika kuhujumu chama kuwa ‘chozi la mtoto wa kike wa Tanzania litawalilia hadi tone la mwisho’,” anasema Cecilia aliyekulia na kulelewa ndani ya TGGA maisha yake yote hadi sasa ni mtu mzima.

Anaushutumu uongozi wa zamani kwa kukihujumu chama kwa kumuuzia JDL theluthi mbili ya mali za TGGA. 

Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TGGA kabla ya kujiuzulu mwaka 2018, Grace Makenya, anakiri kufahamu mengi kuhusu uwekezaji huo. 

“Chama kinapitia wakati mgumu. Kwa sasa siwezi kusema lolote bila ruhusa ya chama. Nikipewa ruhusa nitakueleza kila kitu,” anasema Grace.