Namshukuru Mwenyezi Mungu kupata fursa hii kufafanua juu ya uwekezaji kwenye mashamba ya miti.

Kama tunavyofahamu, misitu ni rasilimali muhimu kwa uhai wetu na viumbe wengine. Hata hivyo, wengi wanaiona misitu kama chanzo cha kupata mbao, magogo, nguzo, mkaa na kuni. Isitoshe, wapo wanaonufaika kwa kufanya biashara ya mazao ya misitu kama kuuza asali na nta.

Kwenye mada hii naeleza kwa ufupi faida zinazopatikana kupitia uwekezaji kwa kuanzisha mashamba ya miti mfano, shamba la taifa la Sao Hill lililopo wilayani Mufindi, Iringa.

Serikali katika miaka ya 1970 iliona ni vema kuanzisha kiwanda cha kutengeneza karatasi. Kutokana na azima hiyo, serikali ilikopa dola milioni tano za Marekani ili kupanda miti kwa wingi. Vilevile, matarajio yalikuwa kujenga kiwanda hicho karibu na Bandari ya Dar es Salaam ili kurahisisha uingizaji malighafi (hasa dawa), lakini pia kusafirisha bidhaa zitakazotengenezwa nje ya nchi.

Ilitarajiwa pia kuanzisha shamba la miti eneo la Msitu wa Ruvu Kaskazini (uliohifadhiwa). Hifadhi hiyo ipo takriban kilometa 70 kutoka Bandari ya Dar es Salaam. Kati ya mwaka 1970 na 1974 hekta 2,000 za miti aina ya pine zikawa zimepandwa hapo. Kwa bahati mbaya miti hiyo haikukua vizuri, hivyo kusababisha nia ya kuanzisha kiwanda cha karatasi karibu na Dar es Salaam itoweke. Kwa hali hiyo ikabidi kutafuta eneo jingine na kwa kutumia takwimu za majaribio (research plots) yaliyofanyika eneo la Sao Hill kati ya mwaka 1939 na 1951, ikaonekana miti ya kutengeneza karatasi inaweza kuota vizuri huko. Vilevile kwa kuzingatia kuwa Reli ya TAZARA inapita Mgololo karibu na Sao Hill.

Shamba la Sao Hill ni miongoni mwa mashamba 23 yanayomilikiwa na serikali na kusimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Katika miaka ya 1970, serikali iliona ni vema kupanda miti kwa kiwango kikubwa na hatimaye kuanzisha kiwanda cha kutengeneza karatasi na vifungashio (paper and pulp mill). Upandaji miti Sao Hill uliongezeka kati ya mwaka 1975 na 1990 ikiwa ni matokeo ya mkopo na sasa ni kichocheo kwa uchumi wa taifa na uboreshaji wa maisha kwa Watanzania.

Shamba hili lina hekta 135,903. Kati ya hizo, hekta 86,003 zinafaa kupandwa miti kibiashara na eneo lililobaki (takriban hekta 48,200) ni kwa ajili ya kuhifadhi na kutunza mazingira ikiwamo kulinda vyanzo vya maji na bioanuai.

Jumla ya hekta 40,352.47 zimepandwa miti kuanzia mwaka 2008/2009 hadi 2017/2018 (kipindi cha miaka 10), ikiwemo asilimia 59.5 ambazo ni eneo lililorudishiwa miti baada ya kuvunwa; na asilimia 40.5 ikiwa ni eneo lililopandwa miti kwa mara ya kwanza. Upandaji miti kwa kiwango kikubwa ni matokeo ya uwekezaji uliofanya na serikali kwa nia njema ya kuendeleza uchumi wa taifa letu kupitia sekta ya misitu na nyuki.

Kupitia mazao ya misitu serikali inakusanya mrahaba na tozo mbalimbali, lakini pia manufaa makubwa yanapatikana kwa wananchi hasa wa vijiji vinavyozunguka mashamba ya miti. Mathalani, kwa miaka 10 iliyopita serikali imepata Sh bilioni 319.5 kutoka shamba la Sao Hill na kwa mwaka mmoja tu wa fedha (20017/2018) zilipatikana Sh bilioni 46.1. Hiki ni kiasi kikubwa kutoka shamba moja tu la miti.

Vilevile kupitia mazao ya misitu serikali inaongeza mapato kupitia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inayosimamiwa na TRA; wakati tozo ya CESS inanufaisha mamlaka kwenye Serikali za Mitaa. Kwa kipindi cha mwaka 010/2011 na 2017/2018 makusanyo ya CESS kwa Sao Hill yalifikia Sh bilioni 6.1.

Manufaa vijijini na kwa wadau yamekuwa ya kutia moyo. Shamba limekuwa likisaidia vijiji kujenga miundombinu kwa ajili ya huduma za afya, shule, ofisi za vijiji na masoko. Kati ya mwaka 2010/2011 na 2016/2017 Sh milioni 491 zilitumika kujenga na kuimarisha miundombinu kwenye vijiji 21. Vilevile; madawati 4,112 yamesambazwa mikoani katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Mtwara, Njombe, Rukwa, Singida, Shinyanga na Tanga. Shamba limeajiri watumishi 273 ambao ni asilimia 72.5 ya mahitaji yake. Isitoshe huajiriwa wafanyakazi wa muda takriban 3,000 kila mwaka. Vilevile, vijiji na wadau wengine hunufaika kutokana na vibali vya uvunaji miti na kilimo katika maeneo yaliyovunwa miti.

Shamba linazungukwa na vijiji 60. Katika kipindi cha mwaka 2011/2012 na 2016/2017 vijiji vilipata meta za ujazo 61,600 zenye thamani ya Sh milioni 3.08. Mwaka wa fedha 2013/2014 kata 30 zilinufaika na 12,800m3 zenye thamani ya Sh milioni 640.

Kipindi cha mwaka 2014/2015 vikundi 48 wilayani Mufindi vilinufaika kwa kupata 12,000m3 kwa thamani ya Sh milioni 600. Mwaka wa fedha 2015/2016 taasisi za serikali zilipata 2,800m3 kwa thamani ya Sh milioni 140. Vilevile kwa kipindi hicho vikundi vinne vilinufaika na 800m3 zenye thamani ya Sh milioni 40. Kwa 2016/2017, Mamlaka ya Mji Mdogo Mafinga, na Halmashauri ya Mufindi walinufaika kwa kupata 10,000m3 kwa thamani ya Sh milioni 500. Taasisi za kidini 2016/2017 zilipata 1,200m3 zikiwa na thamani ya Sh milioni 60.

Manufaa mengine yatokanayo na shamba la Sao Hill ni viwanda vikubwa vya misitu kama Mufindi Paper Mill (MPM) na Sao Hill Forest Industries Ltd. Vilevile, vipo viwanda vya kati na vidogo visivyopungua 500. Vyote vinatoa ajira – watumishi wa kudumu na wa muda kwa wakazi wa Mufindi, Mkoa wa Iringa, mikoa mingine na hata kutoka nje ya nchi.

Kusema kweli manufaa ya shamba la miti Sao Hill ni mengi ukilinganisha na niliyoainisha hapa. Nimetumia shamba hili kuonyesha kuwa fedha zilizokopwa miaka ya 1970 zimenufaisha nchi na watu wake, lakini pia kuonyesha kuwa kuwekeza kwenye mashamba ya miti si kupoteza rasilimali fedha na nguvukazi.

Mabilioni ya fedha yanayopatikana kila mwaka ni ishara kuwa thamani ya miti ni kubwa. Nichukue fursa hii kuiomba serikali kuwekeza zaidi kwenye mashamba ya miti.

Mahitaji ya mazao ya misitu ni makubwa kuliko uwezo, hivyo kuna upungufu wa meta za ujazo milioni 19.5. Ili kuondoa upungufu huo, tunatakiwa kupanda hekta takriban 200,000 kwa mwaka. Kiwango hicho kinahitaji fedha nyingi, hivyo kuna haja ya kukopa. Taasisi za serikali kama TFS na za sekta binafsi zikiwezeshwa kupanda miti kwa wingi misitu itachangia kwa kiwango kikubwa kwenye uchumi wa viwanda na kuinua kipato cha wananchi.

Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician Kilahama, ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI). Anapatikana kwa simu: 0756 007 400.