Umoja wa Watuma Salamu Tanzania (UWASATA) unahitaji nguvu ya wahisani uweze kuongeza misaada kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi nchini.
Mwenyekiti wa umoja huo, Iddi Maziku, amesema mahitaji ya watoto ni makubwa na yanahitaji nguvu ya pamoja kuyakabili ipasavyo.
“Pamoja na kuhamasisha masuala ya uhusiano na ujasiriamali miongoni mwa jamii, tunatekeleza mpango wa kusaidia watoto yatima katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kwa mfano, hadi sasa tumefanikiwa kuwasaidia watoto yatima katika mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam, Manyara, Arusha, Singida na Tanga.
“Jukumu kama hili la kusaidia watoto yatima linahitaji uwezo wa kifedha kulifanikisha. Tunaamini kuwa serikali na wahisani mbalimbali wapo na wana uwezo wa kutuunga mkono katika hili,” amesema Mziku katika mahojiano na JAMHURI Dar es Salaam, wiki iliyopita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Nidhamu wa UWASATA, Abisalimu Msuya, umoja huo unaendelea na jitihada za kuanzisha na kuendeleza miradi mingi ya uzalishaji mali katika sekta za kilimo, ufugaji na ushonaji kuwakwamua wanachama wake kiuchumi.
“Hatuwezi kusema tumepiga hatua kubwa sana ya maendeleo lakini sisi kama UWASATA pamoja na miradi mingine, tumefanikiwa kuanzisha SACCOS (Chama cha Kuweka na Kukopa Fedha) katika Kanda ya Ziwa,” amesema Msuya.
Kwa mujibu wa Msuya, hadi sasa umaja huo una wanachama zaidi ya 250 hapa nchini.
Katika hatua nyingine, Msuya amesema uchaguzi mkuu wa viongozi wa ngazi mbalimbali wa umoja huo umepangwa kufanyika Oktoba 26, mwaka huu mkoani Tanga.
Ametoa wito kwa wanachama wenye sifa za kugombea uongozi katika umoja huo kuhakikisha wanatumia vizuri nafasi hiyo utakapofika muda mwafaka.