Watumiaji wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza watakiri kuwa uwanja huo ni kiungo muhimu sana kwa shughuli za kibiashara, kijamii na hata kisiasa.

Ni kiungo muhimu sana kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na mataifa yote ya Maziwa Makuu. Kama tungekuwa makini, Mwanza ndiyo ingestahili, pasi na shaka yoyote, kuwa “hub” ya Afrika Mashariki na Kati.

 

Pamoja na kusuasua kwetu katika kuifanya Mwanza kuwa “hub”, yenyewe imejihalalisha kuwa na sifa hiyo. Bahati mbaya ni kwamba viongozi wetu, ama kwa kutojua au kwa uzembe, wameuacha Uwanja wa Ndege wa Mwanza uwe kama kituo cha daladala! Nimewaona wageni wengi wakishangazwa na hali ya uwanja huo.


Mara kadhaa tumesikia mipango kabambe ya kuufanya uwanja huo uwe wa kisasa. Upanuzi au uboreshaji uwanja huo umebaki porojo. Hakuna dalili za wazi zinazoonesha kama kweli tumedhamiria kuufanya uwanja huo kuwa uwanja wa kimataifa – wenye hadhi inayolingana na umuhimu wa Mkoa wa Mwanza kama “hub” ya Afrika Mashariki na Kati.


Kila uchao kunajengwa vibanda mithili ya vile vya kina mama ntilie mitaani. Kama Jumatatu ulikuta kunajengwa kibanda upande huu, Jumatano utakuta kunajengwa kibanda upande ule! Kumekuwapo ujenzi wa vibanda visivyokuwa na hadhi wala mvuto unaoendana na umuhimu wa uwanja huu.

 

Kwa haraka haraka unaweza kuamini kuwa kinachofanywa na waliopewa mamlaka ya kuuendeleza uwanja huo, ni mbinu tu ya kufuja fedha. Kibaya zaidi, uwanja huu unatia aibu mno sehemu ya kupokea mizigo. Hakuna mashine wala utaratibu mzuri wa kupokea mizigo.


Kilichofanywa na “wahandisi” wetu ni kutoboa mashimo makubwa ukutani ambayo yanatumika kupenyezea mizigo ya wasafiri. Hakuna utaratibu kwa abiria kupanga mstari kupokea mizigo yao, badala yake mwenye nguvu ndiye anayeanza kuchukua mzigo unaomhusu. Kwa mgeni ambaye ni mara yake ya kwanza kufika Mwanza, kitendo cha kupokea mzigo kwa staili hiyo kitakuwa kimempa taswira na kiwango halisi cha kufikiri cha Watanzania. Uwanja mkubwa, ulio ‘bize’ kiasi hicho hauwezi kuwa na sehemu ya kipuuzi ya kupokea mizigo ya aina hiyo.


Kinachouma zaidi ni pale unapobaini kuwa Mkoa wa Mwanza ni wa pili nyuma ya Dar es Salaam, kwa kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa (GDP). Unachangia Sh trilioni 3 kwa mwaka. Dar es Salaam inaongoza kwa kuchangia Sh trilioni 5.4.

 

Nje ya uwanja, kuna vibanda vingi vya kipuuzi vilivyojengwa kwa mfumo wa uyoga. Hivi ni vile vinavyotumiwa kuuza vocha za simu, vyakula na huduma nyingine ndogo ndogo.

 

Nini kifanyike? Kasi ya maendeleo kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati ni kubwa mno. Nchi zinazotuzunguka zinasaka maendeleo kwa udi na uvumba kwa kasi ambayo si rahisi kuielezea. Tukishindwa kwenda na kasi hiyo, ni wazi kwamba tutaachwa nyuma.


Tusipoifanya Mwanza kuwa “hub” ya ukanda huu, fursa hiyo itachukuliwa na wenzetu hata kama kijiografia hawana sifa hiyo.


Uwanja wa Ndege wa Mwanza tunapaswa kuuboresha ili uwe na hadhi ya kupokea ndege na wageni wa aina mbalimbali. Uwe uwanja ambao “mwekezaji” akifika, atatuweka kwenye kundi la watu makini, badala ya sasa ambako kwa kuuona uwanja tu, atajua hawa ni watu wa kuhongwa na kuruhusu chochote wanachotaka.

 

Rais Jakaya Kikwete alipozuia ujenzi wa stendi ya muda mkoani Dar es Salaam, alifanya jambo la maana. Aliagiza litafutwe eneo, ijengwe stendi yenye hadhi na ambayo itakuwa imekamilisha jambo hilo.


Ujenzi wa vibanda katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza ni dalili ya uchovu wa fikra, na hauashirii kama kweli tumejiandaa kwenda na kasi ya wenzetu katika suala zima la maendeleo.


Kuendelea kung’ang’ana na vibanda kama vya waganga wa kienyeji, ilhali wenzetu wanajenga majengo ya kudumu na yenye hadhi, ni kujidhalilisha. Ukitazama miundombinu iliyojengwa na Mzee Mwai Kibaki kwa miaka yake mitano ya mwisho, halafu ukatazama Uwanja wa Ndege wa Mwanza, unashawishika kuamini kuwa sisi ni mahodari wa porojo tu.

 

Kwa jinsi tunavyopenda kuunda tume, si ajabu tukasikia inaundwa tume kupata sababu za uwanja huu kuwa duni kiasi hiki!