Madaktari Bingwa wa Samia Suluhu Hassan wamefanikiwa kumtoa uvimbe wenye uzito wa gramu 800 kwenye kizazi mgonjwa alioishi nao kwa zaidi ya miaka 10.

Hayo yamebainishwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake na uzazi, Dkt. Emmanuel Imani Ngadaya kutoka Hospitali Rufaa ya Kanda ya kusini aliyeongoza jopo la Madaktari Bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara mara baada ya kukalilika kwa upasuaji huo.

Dkt. Ngadaya ameeleza kuwa wakiwa katika utekelezaji wa kampeni hiyo walipokea mgonjwa aliyekuwa na tatizo la uvimbe kwenye kizazi.

“Jana tulikuwa tukiendelea na shughuli zetu za kutoa huduma za kibingwa na bingwa bobezi tulimpokea mgonjwa mwenye umri wa miaka 49 mwanamke ambaye amekua akiteseka na uvimbe kwenye kizazi kwa muda wa miaka 10 sasa”, amesema Dkt. Ngadaya

“Mara baada ya uchunguzi tukagundua kuwa amekuwa na hali ya uvimbe tumboni uliomsababishia kutofanya shuguli zake za kila siku za kujiingizia kipato” ameeleza.

Ameongeza kuwa kwa kushirikiana na madaktari wa Hospitali ya Mangaka iliyopo Halmashauri ya Nanyumbu ambapo madaktari bingwa wameweka kambi hiyo katika Masasi waligundua kuwa uvimbe wake unahitaji kufanyiwa upasuaji.

Aidha amesema kuwa ule uvimbe uliotolea wanafanya utaratibu wa kuusafirisha kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa vipimo na uchunguzi zaidi.

Akizungumza mara baada ya upasuaji huo mgonjwa ambaye jina lake limehifadhiwa amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujali wananchi wake na kuwasogezea huduma za ubingwa na ubingwa bobezi karibu kwani hakuwa na uwezo wa kusafiri na kulipia gharama za kufanya upasuaji huo.

“Leo najisikia vizuri hata hamu ya kula nimepata awali kabla ya upasuaji nilikuwa hata hamu ya kula sina namshukuru sana mama Samia kwa hii kampeni yake ya huduma za madaktari bingwa bobezi ambayo imesaidia kuondolewa uvimbe ambao umenitesa kwa muda wote huo na kuninyima muda wa kufanya kazi za kuniingizia kipato” ameeleza.   

Please follow and like us:
Pin Share