Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM,) Mkoa wa Njombe imeonya na kupiga marufuku vijana kuwa chawa kwa lengo la kutafuta uongozi au kipato na kuwataka kutumia njia sahihi za kupambania chama kwa kuwa kina utaratibu mzuri wa kuwapika na kuwapata viongozi sahihi.

Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Samwel Mgaya wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya jumuiya hiyo kuanza kampeni maalum ya kumuunga mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kutokana na mambo yote ya maendeleo yaliyofanywa katika Mkoa wa Njombe.

“Vijana lazima tuonyane, chama chetu kina utaratibu mzuri wa kuoka na kuandaa upatikanaji wa viongozi sio kujipendekeza na kuwa machawa ila vijana wenzangu kazi zetu ndizo zitakazotupambanua na kutuweka mahali panapostahili” amesema Samwel Mgaya Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Njombe

Vilevile jumuiya hiyo imesikitishwa na baadhi ya maeneo ambayo yameonyesha ubadhilifu mkubwa wa fedha kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupitia ripoti iliyokabidhiwa hivi karibuni kwa Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na kuwataka watumishi wa umma kuwa wazalendo katika nafasi wanazopewa ili kuwatumikia watanzania.

“Tunawataka watendaji waendane na kasi ya Mh! Rais,wawe waaminifu kwenye fedha za serikali na wawe wabunifu kuleta miradi yenye tija,pia tunataka kwa dhamani waliyopewa wawe waadilifu na tunaamini ripoti ya CAG ijayo itakuwa haina ubadhilifu kama hii” amesema.

UVCCM Mkoa wa Njombe inatarajia kuanza kampeni hiyo mkoa mzima wa Njombe kwa jina la Nasimama na Mama itakayozinduliwa Mei 2 mwaka huu kwa kuzungumzia miradi mbali mbali inayotekelezwa mkoani Njombe huku pia wakitarajia kufanya mijadala na midahalo ili kuzungumzia shughuli zinazofanywa na serikali.