Uvamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 27, umeendelea kushika kasi huku kukiwa hapo na tishio la kuongezeka kwa migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya wahifadhi, wafugaji na wakulima.
Uvamizi huo umechochea kwa kiwango kikubwa uharibifu wa mazingira na hivyo kuongeza athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwamo kupungua kwa maji na kuongezeka kwa mafuriko, ukame na mmomonyoko wa udongo.
Aidha, kupungua kwa malisho ya wanyamapori kumesababisha wanyamapori wengi kuhama katika baadhi ya maeneo ya hifadhi, hatua inayosemwa imeathiri shughuli za utalii.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwapo na tatizo kwa baadhi ya wananchi kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa kisheria kwa ajili ya shughuli za kibinadamu kama vile makazi, kilimo na kulisha mifugo.
Takwimu zinaonesha kuwa tatizo la uvamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa zikiwamo hifadhi za taifa hasa uingizwaji holela wa mifugo, imeongezeka kutoka ng’ombe 23,182 mwaka 2009 hadi wastani wa ng’ombe 75,701 kwa mwaka kwa miaka mitano mfululizo kutoka 2010 hadi mwaka jana.
Hali hiyo si tu inahatarisha ustawi wa kiikolojia wa maeneo yaliyohifadhiwa bali pia inatajwa pia kuchangia kukuza migogoro kati ya mamlaka za hifadhi na wananchi hasa waishio vijijini.
Hatua hiyo imesababisha kuwapo kwa msukumo kutoka kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wa ardhi kutaka kuhaulishwa kwa maeneo ya hifadhi, na hivyo kuyapunguza kwa ajili ya matumizi mengine yasiyo ya kiuhifadhi hususani ufugaji.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanzania inayo mapori 28 ya akiba yakiwa na jumla ya kilomita za mraba 114,783 na misitu ya hifadhi ikiwa 455 yenye jumla ya eneo la kilomita za mraba 142,561.
Kwa upande wa mapori tengefu, Tanzania inayo jumla ya 42 yakiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 58,565 huku hifadhi za Taifa zikiwa 16 zikiwa na jumla ya kilomita za mraba 57,366.
Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro iliyopo mkoani Arusha, ni moja ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 8,292 huku kukiwapo na hifadhi 10 za kihistoria zenye jumla ya kilomita za mraba 710.
Maeneo hayo yaliyohifadhiwa kisheria, yana umhimu mkubwa kiikolojia, kiuchumi na kijamii, kwani huchangia ustawi katika sekta ya kilimo, mifugo, nishati na maji.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, anasema manufaa makubwa ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ni pamoja na upatikanaji wa maji kwa ajlii ya matumizi ya majumbani, kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa umeme.
Anataja manufaa mengine kuwa ni pamoja na upatikanaji wa maji ya kuendeshea viwanda, ustawi wa wanyamapori, samaki na viumbe wa majini pamoja na kulisha maji katika bahari, maziwa makuu na madogo.
“Kwa mfano Mto Pangani hulisha moja kwa moja Ziwa Jipe na Bwawa la Nyumba ya Mungu, ambayo hutumiwa na idadi kubwa ya wananchi waishio vijijini kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji na uvuvi,” anasema Prof. Maghembe.
Kwa mujibu wa Prof. Maghembe, vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria huchangia takribani aslimia 60 ya umeme wote unaozalishwa nchini kwa ajili ya Gridi ya Taifa ambako jumla ya megawati 1,717.33 huzalishwa.
Mfano, kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu hutegemea maji yake kutoka Mto Ruaha unaopokea maji kutoka Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa ambako jumla ya megawati 558.34 huzalishwa.
Bwawa la Mtera hupokea maji yake kutoka Mto Ruaha ambao nao hupokea maji kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na pori tengefu na Usangu ambako jumla ya megawati 166.68 huzalishwa.
Vituo vingine vya kuzalisha umeme ni Hale, ambacho hupokea maji kutoka Mto Pangani ambao unategemea maji kutoka vyanzo vya maji katika hifadhi za Tafa za Kilimanjaro na Arusha, na huzalisha megawati 36.11 za umeme.
Kituo cha New Pangani kinazalisha megawati 137.2 huku Bwawa la Nyumba ya Mungu likizalisha megawati 21.53 na Bwawa la Kihansi likizalisha megawati 795.17 ambalo hupokea maji kutoka Mto Ruaha.
Prof. Maghembe alikuwa akiwasilisha mada juu ya mtazamo wa wizara yake kuhusu kupunguzwa kwa maeneo ya hifadhi nchini kwa ajili ya kupitisha shughuli za kibinadamu hivi karibuni bungeni mjini Dodoma.
Katika taarifa yake, anasema pamoja na faida zinazotokana na upatikanaji wa maji, hifadhi za misitu zinachangia kupunguza athari za hewa ya ukaa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambako inakadiriwa jumla ya tani milioni 17 za hewa ya ukaa zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 62.410,431 zimenyonywa katika misitu iliyopo nchini.
Athari za kupunguza maeneo ya hifadhi kwa ajili ya mifugo
Prof. Maghembe anasema kuwa mchanganuo wa faida za maeneo yaliyohifadhiwa na zile za ufugaji, yanaonesha wazi kuwa hifadhi ya maliasili ni sekta mhimu, pana na mtambuka na kwamba sekta hiyo ndiyo msingi wa kuwapo kwa maendeleo ya sekta nyingine nyingi.
Anataja miongoni mwa sekta hizo kuwa ni pamoja na kilimo, mifugo, uvuvi, umwagiliaji, nishati na viwanda pamoja na ustawi wa binadamu huku akisisitiza kuwa kwa maana nyingine sekta ya maliasili si sekta tegemezi, bali inahitaji kuimarishwa ili kuendelea kuwa mhimili wa kusaidia sekta nyingine.
“Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 32.4 ya eneo la nchi yetu limehifadhiwa, na hifadhi hizi zimetawanyika katika maeneo mbalimbali kwa kuzingatia ukubwa wa nchi yetu, ni mhimu maeneo haya yaendelee kuhifadhiwa kwa ukubwa uliopo ili kutoa huduma za kiikolojia,” anasema Prof. Maghembe.
Waziri Maghembe anaonya kuwa uvamizi huo katika maeneo yaliyohifadhiwa si tu unahatarisha ustawi wa maeneo hayo na kutishia ustawi wa utalii kwa ujumla wake, bali pia unakaribisha jangwa na kutoweka kwa maisha ya viumbehai.
Anasema tatizo linalojitokeza si upungufu wa ardhi kama inavyodhaniwa bali ni kuwapo kwa ufugaji huria usiofuata miongozo ya kitaalamu kwa mujibu wa sera, sheria, taratibu na miongozo ya sekta ya mifugo.
Prof. Maghembe anahitimisha kwa kutoa rai kwamba ipo haja sasa ya kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera na sheria pamoja na miongozo iliyopo kwa manufaa ya sekta za uhifadhi na ufugaji, lengo likiwa ni kuyalinda maeneo yaliyohifadhiwa kisheria zikiwamo hifadhi za Taifa.