Na Deodatus Balile, JamhuriMedia
Aprili 17 hadi 21, 2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, alifanya ziara rasmi ya kiserikali nchini Uturuki.
Wiki iliyopita niliandika kuhusu ukubwa wa uchumi wa nchi ya Uturuki, mapinduzi makubwa ya kiuchumi aliyoyafanya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, kati ya mwaka 1994 na 2024, ambayo yameifanya nchi hiyo kuwa taifa kubwa duniani.
Katika makala hiyo nilisisitiza fursa zilizopo na uamuzi mkubwa uliofanywa na marais hawa wawili. Uamuzi wa kwanza ni kusaini mkataba wa dola bilioni 6.4, sawa na Sh trilioni 17.3 zitakazotumika kujenga reli ya mwendo kasi (SGR).
Nilieleza kuhusu wingi wa fedha hizi, na nilirejea idadi ya huduma na bidhaa zilizofanywa kwa kutumia Sh trilioni 1.3 za Uviko – 19, hivyo nikasema kishindo cha dola bilioni 6.4 kuingia katika uchumi wa Tanzania kupitia reli ya SGR ni jambo kubwa na lenye manufaa ya kipekee katika uchumi wetu.
Jambo la pili ambalo ni msingi wa makala hii, ni nia ya Serikali ya Uturuki kufanya biashara na Tanzania yenye thamani ya dola bilioni 1 ndani ya mwaka mmoja ujao.
Uturuki wanaonekana kupendezwa na jinsi Rais Samia Suluhu Hassan anavyoendesha siasa na uchumi wa Tanzania, ambapo hata hapa kwetu ukisikiliza watu wengi wanafurahia jinsi Rais Samia anavyoifungua nchi.
Sitanii, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akitunukiwa Udaktari wa Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Ankara, Uturuki, Aprili 18, 2024, Mkuu wa Chuo Kikuu hicho cha nchini Uturuki, Profesa Necdet Unuvar, alisema wamempa shahada hiyo kutambua jitihada zake za kuendeleza Mageuzi ya Kijamii, Kisiasa na Kiuchumi – 4R.
Aligusia jinsi anavyojali elimu kwa Tanzania – hasa kuwarejesha shuleni wasichana waliopata mimba kabla ya kumaliza masomo, diplomasia ya kimataifa, na kubwa zaidi alivyofungua milango na kuanzisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na sekta binafsi.
Sitanii, kwa sisi tuliopo katika sekta binafsi tunakumbuka tulivyokuwa kwenye chetezo katika awamu iliyopita. Kuna rafiki yangu alipata kuniambia hivi: “Tumetoka katika nyakati za hatari, tumeingia katika nyakati za giza… huko tuendako hakuonekani.” Kauli hii kwa mashabiki wa siasa za kibabe hawakupata kuiona kama inazungumza kitu cha msingi, ila uchumi wa nchi yetu tayari uliishagota.
Nakumbuka marehemu Bernard Membe alipata kusema: “Tanzania siyo kisiwa.” Kwamba hatuwezi kutoshirikiana na nchi za wenzetu, kufanya biashara na nchi nyingine na tukajitosheleza katika kila jambo, ni suala lisilowezekana. Kwa kuiua sekta binafsi, idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi ipatayo milioni 24 Tanzania ilikuwa imewekwa rehani. Serikali inaajiri wafanyakazi wapatao 600 tu.
Taarifa rasmi zinaonyesha kuwa jumuiya ya Waturuki wanaoishi Tanzania wanafikia 1,500. Kati yao hawa, baadhi wanafanya biashara, wengine ni watumishi, wakiwamo walimu na wafanyakazi wa sekta ya afya. Hawa wanachukuliwa kuwa kiunganishi msingi kinachowezesha Watanzania kufikia adhima ya marais wetu ya kufanya biashara ya wastani wa dola bilioni 1 (sawa na shilingi trilioni 2.7) ndani ya mwaka mmoja ujao.
Kwa sasa takwimu za biashara kati ya Uturuki na Tanzania zinaonyesha ukuaji wa kuridhisha. Hata hivyo, urali wa biashara kati ya Uturuki na Tanzania bado umelalia upande mmoja. Tanzania inauza kidogo ikilinganishwa na kinachouzwa na Uturuki nchini Tanzania. Wakala wa Uratibu na Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uturuki (TIKA) uko tayari kuwapa fursa Watanzania kushirikiana na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali.
TIKA inafanya kazi katika nchi 170 duniani na kwa Tanzania ilianzishwa mwaka 2009. Tayari Tanzania na Uturuki zina jumla ya miradi 106 inayogusa maeneo mbalimbali, mkubwa ukiwa ni mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) yenye urefu wa kilomita 1,596 kutoka Dar es Salaam hadi Isaka, Shinyanga unaojengwa na Kampuni ya Yapi Merkezi. Kampuni nyingine kubwa ya Uturuki iliyopo Tanzania inaitwa Orkun Group.
Uturuki imeanzisha ndege ya moja kwa moja kuja Tanzania kupitia Shirika lake la Turkish Airline, ambalo kwa wiki linafanya safari 18 za ndege kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Kilimanjaro. Safari hizi za ndege zimekuwa zenye manufaa makubwa mno. Takwimu zinaonyesha biashara kati ya Uturuki na Tanzania imekua zaidi baada ya usafiri huu kuanzishwa.
Kwa wakaazi wa Zanzibar na Dar es Salaam, wanafahamu kuwa Waturuki wapo kwenye biashara za hoteli (restaurants), ujenzi, utengenezaji wa mabomba ya plastiki na upigaji rangi wa kiwango chenye ubora wa hali ya juu. Pia kuna matrekta, vifaa vya umeme, magari, nguo na vitu vingine vingi vyenye ubora wa hali ya juu vinavyouzwa nchini Tanzania kutoka Uturuki.
Sitanii, nchi yetu inanunua mitambo, vyuma, nondo, mbolea, samani za ndani, chumvi, aluminium, shaba na bidhaa nyingine kutoka Uturuki, ambazo zinauzwa katika maduka yetu. Kwa sasa Tanzania inauza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 15.99 sawa na Sh bilioni 41.3, huku Uturuki ikiuza Tanzania bidhaa zenye thamani ya dola milioni 252.2 sawa na Sh bilioni 624.8.
Taarifa rasmi zinaonyesha kuwa Uturuki wako vizuri sana kwenye teknolojia ya viwanda vya nguo. Kwa sasa wanahitaji pamba nyingi kuliko maelezo. Kwa fursa zilizotangazwa, Tanzania inaweza kuuza bidhaa nyingi moja kwa moja bila vikwazo, ila hatujafikia hata asilimia 40 ya mahitaji. Fursa hizi ni dhahabu, ufuta, pamba, chai, kokoa, mchele, maharage ya soya na mahindi.
Kampuni za Uturuki ziko tayari kuingia ubia na Tanzania zizalishie hapa hapa kwetu bidhaa zenye ubora unaokubalika katika soko la kimataifa.
Wanasema wapo tayari kutoa ujuzi wa kuandaa vifungashio, kuendesha mitambo na kufanya uwekezaji utakaoiwezesha Tanzania kutumia pamba yake kuzalisha nyuzi badala ya kuuza marobota.
Uturuki ina uchumi mchanganyiko, ambao sekta binfsi inapewa kipaumble na serikali inaanda sheria, sera na miongozo, huku ikibaki na jukumu la msingi la kukusanya kodi na kujenga miundombinu ya msingi kama barabara, reli, viwanja vya ndege, mabomba ya mafuta na mengine ambayo yana ukubwa wa kitaifa.
Zipo fursa nyingi za elimu kwa Watanzania. Ipo taasisi inaitwa Elimu Maarifa Foundation Schools, ina shule Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar. Ipo taasisi inayoshughulikia elimu kwa Watanzania wanaotaka kwenda kusoma Uturuki inaitwa Rehema Foundation and Olgun Schools (NGOs).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, January Makamba, anasema Tanzania inaendelea kupita katika njia sahihi ya kukuza uchumi na maendeleo ya jamii kupitia nyanja za huduma, utalii, viwanda, elimu, sayansi na teknolojia, maeneo ambayo Uturuki iko tayari kushirikiana na Tanzania kuyaendeleza.
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Balozi Idd Seif Bakari, anasema uhusiano wa Tanzania na Uturuki ulianza kukua zaidi mwaka 2010, Rais Jakaya Kikwete alipoitembelea Uturuki katika ziara rasmi ya kiserikali, ambayo ilifuatiwa na ziara ya Rais Erdogan nchini Tanzania, Januari 23, 2017 alipokutana na Rais (hayati) John Pombe Magufuli.
Anaamini ziara ya Rais Samia ya Aprili, mwaka huu, imesaidia kukuza zaidi uhusiano kati ya Uturuki na Tanzania kupitia biashara, maendeleo ya uchumi, hali itakayozaa maisha bora kwa Watanzania. Hakika ukiangalia mapokezi yalivyokuwa na jinsi Uturuki ilivyojiandaa kushirikiana na Tanzania, kinachotakiwa sasa ni kuongeza uchangamfu kwa upande wetu.
Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dk. Mehmet Gulluoglu, amesema Uturuki inathamini uhusiano unaoendelea kukua kati yake na Tanzania, hasa ukuaji wa biashara unaoongezeka siku hadi siku. Anaamini ziara ya Rais Samia Uturuki imezidi kufungua milango na kwamba nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania kwa maendeleo endelevu.
Mazingira ya Uturuki yanafanana na ya Tanzania. Wakati inapakana na bahari, hata Tanzania inapakana na bahari. Hadi sasa nchi hiyo inahifadhi wakimbizi milioni 3.2 kutoka Syria, ambao hadi mwaka 2011 ilikuwa imetumia dola bilioni 40, zaidi ya Sh trilioni 100 kuwahudumia. Tanzania nayo kwa muda mrefu imekuwa na wakimbizi kutoka Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Sitanii, mpendwa msomaji leo utaona mtiririko wa makala hii uko tofauti kidogo na uandishi wa safu hii ya Sitanii, kwani umefanya marejeo kwa njia ya kihabari yanayogusa viongozi mbalimbali. Nikushirikishe tu uzito wa Uturuki ili msomaji ujue kuwa si taifa jepesi. Kati ya nchi 32 za Jumuiya ya Kujihami ya nchi za Magharibi (NATO), Uturuki ni moja ya nchi nane bora katika uchangiaji wa bajeti.
Katika Umoja wa Mataifa, Uturuki inayoamini kuwa dunia haipaswi kuongozwa na nchi tano pekee, kwenye nyanja ya diplomasia ina ofisi za Ubalozi katika nchi na maeneo maalumu 261. Hii inaifanya nchi hii kuwa na Ubalozi na Ubalozi Mdogo katika karibu kila nchi ya dunia hii. Inaamini katika ukuaji wa pamoja kiuchumi, kwa maana ya uchumi jumuishi duniani. Uturuki ni nchi ya 19 kwa uchumi mkubwa duniani na ya 5 barani Ulaya.
Sitanii, nilichoandika katika makala hizi mbili ni sawa na tone la maji katika bahari. Milango iliyofunguliwa na Rais Samia kupitia ziara hii nchini Uturuki, tunapaswa kuichukua kwa mikono miwili. Naamini nchi zote zilizofuta umaskini katika nchi zao zilipata mtu wa kuzishika mkono. Soko kubwa la bidhaa za Uturuki liko Urusi, China na Ujerumani. Sisi ni nani basi tusifanye biashara na Uturuki nasi tukaingia kwa kishindo katika masoko hayo? Watanzania tuishike nafasi hii isituponyoke. Mungu ibariki Tanzania.