Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma (TAMISEMI), imetangaza kuzuia safari za watumishi wa umma katika ofisi za mikoa, wilaya na mamlaka za Serikali za Mitaa kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi.
Sababu kuu iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu wa TAMISEMI ni kuwa watumishi hao wamekuwa wakitumia muda mrefu kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi hivyo kukwamisha shughuli za maendeleo.
Tunatambua umuhimu kwa watumishi wa umma kuwa katika vituo vyao vya kazi, lakini hatuamini kama kweli kusafiri mara kwa mara kwa watumishi hao kunatosha kuwa na marufuku kama hii iliyotolewa na TAMISEMI.
Pia tunatambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano za kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaratibiwa na ikibidi yapungue. Hakuna ubishi kuwa kwa miaka mingi safari za aina hii zimekuwa kichaka ambamo ndani yake fedha za umma zimetafunwa.
Pamoja na nia njema ya serikali, bado tunaamini kuwa si busara kuzuia safari za watumishi wa umma. Tusifike hatua ya kuufanya utumishi wa umma kama sehemu ya kuwabana mno watumishi kiasi cha kuwafanya wajione walikosea kuomba au kukubali kufanya kazi serikalini.
Kama alivyosema Katibu Mkuu wa TAMISEMI, sababu kuu ya kuchukuliwa kwa uamuzi huo ni tabia ya watumishi wengi kusafiri na kuacha vituo vyao vya kazi. Kwa serikali inayoendesha mambo kimfumo, hii si sababu ya msingi ya kusababisha kuchukuliwa uamuzi kama ulivyotangazwa.
Hii si sababu, kwa kuwa hatujaelezwa ni kwa namna gani wakuu wa vitengo wamekuwa wakitoa vibali vya kusafiri. Je, ni kwa hiari, kwa shinikizo, kwa utaratibu uliopo kwa mujibu wa kanuni za utumishi, au ni kwa kila anayetaka kusafiri, anasafiri!
Pili, kama kuna taratibu za kiutumishi za kusafiri, hao wanaotoa vibali kiasi cha kuacha ofisi zikiwa tupu wanafanya hivyo kwa kulenga kupata nini? Kuwafurahisha watumishi wa umma? Kuikomoa serikali ili ionekane inafeli?
Je, TAMISEMI imeshindwa vipi kuwawajibisha hao wanaotoa ruhusa bila utaratibu? Kama wapo wanaosafiri kibabe, hatua gani zimechukuliwa kuwaadhibu? Kwa ufupi ni kuwa maswali ni mengi.
Kusafiri nje ya kituo cha kazi ni zaidi ya kupata posho. Mtumishi anayesafiri pamoja na kupata posho, hutumia fursa hiyo ‘kusafisha macho’ na hata kutuliza akili. Safari ni tiba ya mwili na akili.
Tunatoa mwito kwa serikali kutotumia udhaifu wake wa kushindwa kuratibu safari za watumishi, hivyo kuamua kuwaadhibu hata wasiostahili. Utumishi wa umma ni utumishi, hivyo usigeuzwe kuwa sehemu ya manung’uniko kwa watumishi. Kama wapo wa kuwawajibisha, wawe hao wanaotoa ruhusa za kusafiri bila kufuata miongozo ya utumishi.