DAR ES SALAAM
Na Mwalimu Samson Sombi
Msingi mkubwa wa maendeleo, pamoja na mambo mengine, ni elimu bora inayotolewa kwa wananchi.
Hakuna nchi duniani iliyofanikiwa kupiga hatua kubwa kimaendeleo bila kuweka nguvu katika elimu, hasa elimu ya wote – ya awali.
Elimu ya msingi ni muhimu sana katika kumjengea mwanafunzi msingi imara na kumwandaa kikamilifu kuendelea na masomo katika ngazi za juu.
Elimu hii inapaswa kupewa kipaumbele kikubwa kama msingi wa nyumba ya ghorofa.
Jamii ina mtazamo hasi juu ya umuhimu wa elimu ya msingi nchini. Haitilii maanani elimu hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa, badala yake jamii imeweka matumaini makubwa kwa elimu ya juu.
Watoto wasipojengewa msingi imara wa elimu wakiwa ngazi za awali, itakuwa vigumu na mara nyingine ni gharama kubwa kuwasomesha ngazi za juu za elimu. Hii ni kutokana na misingi mibovu waliyo nayo.
Miaka ya karibuni kumeibuka idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza wasiojua kusoma huku vyuo vikuu wakilalamika kupokea wanafunzi wa mwaka wa kwanza wasiokidhi vigezo vya kujiunga na elimu ya juu.
Mbali na hiyo, kumekuwa na changamoto nyingine ya idadi kubwa ya wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza kutohitimu elimu ya msingi (miaka saba), kutokana na sababu mbalimbali, mojawapo ni utoro.
Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wenye umri wa kuanza shule ya msingi wanakwenda shuleni, jitihada ambazo zimewezesha watoto wengi kuingia darasa la kwanza.
Utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ya mwaka 2014, imepata mwitikio mkubwa kwa watoto wengi kuandikishwa darasa la kwanza na kidato cha kwanza kwa shule za umma.
Waraka Namba 5 wa elimu wa mwaka 2015 unaoruhusu elimu bila malipo, unampa mwanafunzi fursa ya kusoma na kupata elimu bila mzazi au mlezi kulipa ada wala michango ya fedha iliyokuwa ikitozwa awali.
Serikali chini ya Rais Dk. John Magufuli ilianza utekelezaji wa sera hiyo mwaka 2016.
Juni 16, 2020, wakati wa kulivunja Bunge la 11, Dk. Magufuli alieleza mafanikio ya miaka mitano ya uongozi wake ikiwamo kuongezeka kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari, idadi iliyosababisha kuongezeka kwa shule hizo.
Rais Magufuli alisema elimu ni miongoni mwa sekta zilizopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano, mbali na kutoa elimu bure, idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka 2020 na shule za sekondari kutoka 4,708 mwaka 2015 hadi 5,330 mwaka 2020.
Katika hatua nyingine, serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo ndani ya mwaka mmoja.
Machi 1, mwaka huu, Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa, alibainisha idadi ya watoto walioandikishwa shule za awali, msingi na kidato cha kwanza, akisema uandikishaji kwa shule za awali umefikia asilimia 93.5; elimu ya msingi asilimia 101.08 huku elimu ya sekondari ikifikia asilimia 83.5.
Mbali na mafanikio hayo katika uandikishaji, Bashungwa alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejenga shule 15,000, vyumba vya madarasa 18,219 kwa shule za sekondari na za msingi.
Pamoja na ukweli huo, wanafunzi hawa huwa hawafanikiwi kumaliza safari ya elimu katika ngazi husika, utoro ukiwa miongoni mwa sababu.
Idadi ya wanafunzi wasiomaliza shule kutokana na utoro imeongezeka karibu mara tatu kati ya mwaka 2017 na 2020.
Ripoti ya Elimu Msingi (Best 2021) iliyotolewa na TAMISEMI hivi karibuni inaonyesha kuongezeka kwa wanafunzi watoro kutoka 66,142 (ambao hawakumaliza shule mwaka 2017), hadi 198,620 mwaka 2020; hivyo kuchangia asilimia 98.1 ya wanafunzi wasiomaliza shule kwa mwaka 2020 kutoka asilimia 93 mwaka 2017.
Wavulana wa darasa la nne, ripoti hiyo inaonyesha ndio wanaongoza kwa kuacha shule ikilinganishwa na wasichana. Mwaka 2020 asilimia 58.2 ya walioacha shule walikuwa wavulana, huku asilimia 41.8 wakiwa wasichana.
Kati ya wanafunzi wote ambao hawakumaliza shule mwaka 2020, wa darasa la nne walikuwa 62,767, idadi hiyo ilihusisha wavulana 15 zaidi ya wasichana kwa kila wanafunzi 100 wa darasa la nne.
Mbali na utoro, zipo sababu nyingine zilizoainishwa ndani ya ripoti hiyo.
Miongoni mwa sababu hizo ni makundi rika, kukosa mahitaji muhimu, shughuli za uchungaji mifugo, talaka na kutengana kwa wazazi.
Sababu nyingine ni kazi za nyumbani, viwandani, migodini, mashambani, uvuvi, magonjwa, kuozeshwa na mazingira magumu. Pia kuna kujihusisha na biashara ndogondogo na kutunza wazazi na ndugu wengine.
Kukosekana kwa chakula cha mchana shuleni huwafanya wanafunzi wengi kutohudhuria masomo na hata baadhi ya wanaohudhuria kutoroka vipindi kwa sababu ya njaa.
Shule nyingi za msingi wanafunzi huenda asubuhi na kurudi nyumbani mchana kupata chakula; kisha hurudi kuendelea na masomo.
Zipo shule ambazo wanafunzi husoma kwa zamu; yaani kundi la asubuhi hadi saa sita mchana na kundi jingine huanza vipindi mchana hadi jioni.
Unakuta wapo wanafunzi wanakosa chakula shuleni na nyumbani pia, hali inayosababisha utoro. Badala ya kuhudhuria masomo, huamua kutafuta namna nyingine ya kujitafutia chakula.
Kukosekana kwa masomo ya michezo, muziki na stadi za kazi katika baadhi za shule huwakosesha hamu wanafunzi wanaokwenda shuleni kwa sababu ya mambo au masomo hayo kuliko kusoma masomo ya kawaida pekee darasani.
Mwalimu Damian Dismas wa Shule ya Msingi Kiheba, Manispaa ya Ujiji – Kigoma, anasema sababu za baadhi ya wanafunzi kuacha shule ni pamoja na wazazi kukosa uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto na wengine huwapeleka watoto shuleni kwa kuogopa serikali.
“Mimi ninafundisha darasa la kwanza. Mwaka huu niliandikisha wanafunzi 177, lakini hadi mwezi huu kulikuwa na wanafunzi 19 ambao hawakuripoti.
“Baada ya kuwasiliana na wazazi wao, ni watatu tu kati ya hao ndio wameanza kuja shuleni,” anasema Mwalimu Dismas.
Kuhusu mazingira na malezi ya wazazi, anasema mazingira na kipato duni huwafanya watoto kujiingiza katika shughuli za kutafuta kipato kama kufanya kibarua mashambani na biashara ndogondogo.
“Wapo wazazi wanaowashawishi watoto kuacha shule wakafanye shughuli za uzalishaji kama kilimo na biashara. Hii ni kutokana na umaskini,” anasema Mwalimu Dismas.
Mwalimu Dismas anashauri viongozi wa juu serikalini kushirikiana na wenzao wa serikali za mitaa kuwabaini wazazi wanaowazuia watoto kwenda shuleni, wachukuliwe hatua na kufikishwa mahakamani.
Waraka wa Elimu Namba (2016) unaeleza kuwa moja ya majukumu ya kamati za shule ni kuhakikisha chakula cha mchana kinapatikana shuleni.
Maana yake kamati, wazazi na wadau wengine wa elimu wanawajibika kuaandaa utaratibu wa utoaji chakula kwa wanafunzi shuleni.
Chakula cha kutosha chenye virutubisho ni muhimu katika kuimarisha afya ya akili kwa mtoto.
Vijijini shule zinapaswa kuzalisha chakula na mboga. Wanafunzi wafundishwe Elimu ya Kujitegemea (EK), itawasaidia kujenga uwezo wa kuzalisha wakiwa shuleni kuliko kufanya biashara na shughuli hatarishi mitaani.
Ni vema pia kwa serikali kuandaa mazingira rafiki kwa wanafunzi kupenda kujifunza shuleni na kutenga bajeti ya chakula kwa wanafunzi.
0755 985 966