Kutekwa na kupatikana kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji (Mo) kutaleta athari kubwa katika mienendo ya maisha ya watu maarufu. Hatuwezi kubashiri iwapo zitakuwa athari nzuri au mbaya.

Kwanza, na ambalo litajitokeza mara moja ni kupanda kwa maombi ya umiliki wa silaha. Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari juma lililopita, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro alipendekeza wale wenye uwezo kuomba vibali vya kumiliki silaha kwa madhumuni ya kuimarisha usalama wao.

 

Siyo wote wenye uwezo wa fedha za kumiliki silaha. Kwa wenye uwezo itakuwa ni hatua inayothibitisha hofu juu ya usalama wao. Watu ambao awali walichanganyika na Watanzania wenzao bila woga sasa watajenga kuta – kiuasilia na kitamathali – kulinda usalama wao.

Mtu mwoga anayemiliki silaha ni hatari kuliko mmiliki wa aina hiyo ambaye hana woga. Tuombe tu kuwa hatutasikia matukio ya mmiliki wa silaha kumpiga risasi mtu aliyemdhania, kwa makosa, kuwa na nia ya kumdhuru.

 

Imekuwa kawaida sasa yanapotokea matukio ya kutekwa kwa watu kuhusishwa na sababu za kisiasa. Hatufahamu sababu ya kutekwa kwa Mo ingawa lina dalili la wahusika kudai malipo ili kumuachilia.

Hata hivyo, zipo sababu nyingi ambazo siyo zote zinaweza kufahamika kwa urahisi. Hatupendi tabia mbovu, lakini tukiri kuwa hata mwanaume mzinzi, ambaye haoni tatizo la kufaidika na mahari ya mtu mwingine, naye anaweza kutekwa na kudhuriwa na watu waliotumwa na mwenye mali yake.

Wasio na uwezo wa kununua silaha au kuajiri walinzi watalazimika kuchukua tahadhari za kiusalama ambazo hazihitaji kutumia pesa. Zipo nyingi, lakini zipo baadhi ambazo ni rahisi kufuata.

Washauri wa usalama wanasema unapotembea tahadhari mojawapo nzuri ya usalama kuhakikisha huna mtu usiyemfahamu anakufuata nyuma ni kugeuka na kurudi ulikotoka. Mtu yeyote anayekufuata bila uzoefu atababaika unapogeuka ghafla. Lakini faida nyingine ya kufanya hivyo ni kuwa akiendelea kukufuata utaweza kuchukua hatua za tahadhari.

Tahadhari za kiusalama zinahitaji kuweka umakini wa hali ya juu wa mazingira uliyomo na kuweka kumbukumbu ya kinachojitokeza. Kujirudia rudia kwa mtu au kitu ni dalili kuwa mambo si shwari. Unapomuona mtu au watu wale wale mara mbili au tatu kila baada ya muda ni ishara unafuatiliwa.

 

Kuna jamaa yangu mfanyabiashara alichukua pesa nyingi kwenye benki moja ya Mwanza akiwa safarini kwenda Dubai na aliweza kubaini kuna mtu ambaye anamfuata kwa kukumbuka kuwa alimuona mtu huyo benki, akamuona tena mara kadhaa akiwa njiani akielekea Nairobi na akachukua tahadhari kulinda usalama wake.

Ni nadra mtu kutekwa kwenye eneo la watu wengi, kama kwenye mechi ya Yanga na Simba. Watekaji huvizia kwenye maeneo ya watu wachache, kama ilivyotokea kwa Mo, au wanapokuwa na mlengwa tu. Kuwa miongoni mwa wengi ni tahadhari nzuri. Kuhakikisha kuwa hauko peke yako wakati wote pia kunaongeza usalama.

 

Tunafahamu si mabilionea pekee wanaotekwa. Kuna tabia siku hizi ya watu kuanika maisha yao ya kifahari kwenye mitandao ya kijamii. Leo yuko ndani ya ndege anaenda Ulaya, kesho kapiga picha mbele ya gari lake la kifahari, na siku nyingine atatoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kupitia Facebook kujaaliwa kununua nyumba yenye thamani ya mabilioni ingawa thamani yake halisi si hiyo. Ni tabia inayorahisisha kazi ya mhalifu. Wahalifu wanatumia mitandao ya kijamii kufuatilia maisha na mienendo ya wanaowalenga.

Kutotabirika ni kinga nyingine muhimu. Wahalifu wa aina hii huchunguza tabia ya mlengwa: anaenda wapi, na anafanya nini mara kwa mara. Wataalamu wa usalama wanashauri kutotumia njia ile ile wakati wote kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Ipo sababu ya kiusalama kwa misafara rasmi ya viongozi kuendeshwa kwa mwendo kasi. Kwa mwendo wa kawaida ni rahisi zaidi kwa mhalifu kusimamisha gari na kumteka au kumdhuru mhusika. Lakini kupendekeza mwendo kasi kama njia mojawapo ya kujiongezea usalama ni kukaribisha vurugu.

 

Hata hivyo, wapo watu wengi ambao watakuwa tayari kulipa faini ya mwendo kasi ilimradi walinde usalama wao. Kama nilivyobainisha awali, mtu mwoga aliyeshika silaha ni mtu hatari. Lakini woga, kama wa kutoroka wahalifu kwa kuendesha kwa mwendo kasi, unaweza kuwa na manufaa kama utatumika ipasavyo.

Mtu mwoga ni mtu makini, na anaweza kutumia umakini ule kuchunguza na kuepuka mazingira hatarishi na kuchagua yale salama. Mtu anayejiamini sana anaweza kujiingiza kwenye hatari kwa kuamini kuwa anaweza kumudu kila kitisho mbele yake.

Lakini tunafahamu kuwa tahadhari zote hizi hazizuii, bali zinapunguza tu uwezekano wa matukio ya utekaji. Na pia tufahamu kuwa kuna aina ya watekaji ambao hawana ustaarabu wa aina yoyote na wanaweza kukuteka mchana kweupe na bila kujali kuonekana kwao.

Kama kuna jambo moja la uhakika la kuibuka kwenye tukio la kutekwa na kuachiliwa kwa Mo ni kujengeka na kuimarika kwa utengano kati ya raia na watu mashuhuri kama Mo na viongozi mbalimbali ambao majukumu yao yanawalazimu kuwa karibu na watu.

Pengine uzinzi nao utapunguka kidogo. Au kuongezeka?