Na Edward Kondela, JamhuriMedia, Rukwa
Serikali imeanza utekelezaji wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Tanganyika baada ya mpango huo kuonesha mafanikio makubwa katika Ziwa Victoria.
Akizungumza Januari 11, 2024 katika Mwalo wa Kasanga uliopo Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti amesema tayari wizara imeanza kutoa elimu kwa wavuvi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika kabla ya kufikisha vizimba hivyo na mbegu bora za samaki.
Mnyeti ameongeza kuwa kwa sasa serikali imetenga Shilingi Bilioni 20 kwa ajili uwekaji vizimba katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa sababu ufugaji wa samaki unakua kwa kasi maeneo mbalimbali duniani kutokana na upungufu wa samaki waliopo kwenye maji ya asili yakiwemo mabonde, maziwa, mito na bahari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya uharibifu wa mazingira, ongezeko la watu na uharibifu wa mazalia ya samaki.
Ameongeza kuwa ili kunusuru upungufu wa samaki katika masoko ya ndani na nje ya nchi serikali imeamua kuanza kusambaza vizimba kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika ambavyo vitatolewa kwa mkopo nafuu usio na riba.
Awali akiwa katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alipokutana na mkuu wa mkoa huo Mhe. Charles Makongoro Nyerere alimueleza azma ya serikali ya kulipumzisha Ziwa Tanganyika katika shughuli zozote za uvuvi kwa kipindi cha miezi mitatu kila mwaka kwa miaka mitatu mfululizo ambapo kwa mwaka huu litafungwa kuanzia tarahe 15 mwezi Mei hadi 15 mwezi Agosti 2024 ili kupisha samaki waweze kuzaliana.
Amesema kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo ni utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Usimamizi wa Uvuvi endelevu katika ziwa hilo na bonde lake ambapo nchi wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika kwa maana ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokeasia ya Kongo, Tanzania na Zambia zilitia saini mkataba huo Tarehe 9 Mwezi Desemba Mwaka 2021 kwenye mkutano wa 9 wa mawaziri wa nchi hizo.
Amebainisha kuwa kupumzishwa kwa ziwa hilo kutatoa fursa kwa wavuvi kujifunza namna bora ya kufuga samaki pamoja na kuwa na njia nyingine za kujipatia kipato zikiwemo za kufuga mifugo na kilimo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Charles Makongoro amesema mpango wa serikali kuhamasisha kufuga samaki kwa njia ya vizimba ni mzuri kwa kuwa wavuvi watapata fursa ya kujifunza namna nyingine ya kuendeleza biashara ya samaki na kwamba mkoa utasimamia utekelezaji huo ili wananchi waendelee kunufaika na mazao ya uvuvi.
Baadhi wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika wakiwa kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti katika Kata ya Kasanga, wamepongeza juhudi za serikali kwa kuwatafutia njia mbadala ya kuendeleza Sekta ya Uvuvi na kuiomba serikali kuzidi kutoa elimu zaidi juu ya ufugaji kwa njia ya vizimba.
Aidha, wamekiri kwamba kwa sasa mazao ya samaki yamepungua kwa kiasi kikubwa katika ziwa hilo na samaki wanaopatikana ni wadogo ambao wanahitaji kubakia ziwani ili kukua.
Naibu Waziri Mnyeti amepata pia fursa ya kushuhudia maendeleo ya ujenzi wa soko la samaki katika Kata ya Kasanga linalogharimu Shilingi Bilioni 1.4 na kuwataka wananchi hao mara soko litakapokamilika ni vyema wakaliendesha wao wenyewe na kulifanya la kisasa zaidi.