Na Deodatus Balile

Wiki tuliyoimaliza imekuwa na matukio
mengi. Tumesikia kifo cha Mkurugenzi wa
Fedha na Mipango wa Hospitali ya Rufaa
Bugando, Mtawa Susan Bathlomeo. Kifo
hiki kimeacha maswali mengi. Wapo
wanaosema amejirusha, wapo wanaosema
amerushwa kutoka ghorofani. Mpaka sasa
uchunguzi unaendelea na hatujapata jibu
kamili.
Sitanii, mwezi Agosti umekuwa na vifo vingi
kwa kiwango cha kutisha. Wakati
tunaomboleza kifo cha Mtawa Susan,
tukasikia kuwa mwanafunzi wa darasa la
tano katika Shule ya Msingi Kibeta iliyoko
Manispaa ya Bukoba, Sperius Eradius (13),
amekufa baada ya kupokea kipigo kikali
kutoka kwa mwalimu. Mwalimu Respicius

Patrick (50) anashikiliwa na polisi kwa
tuhuma za kumpiga mwanafunzi huyo hadi
kumuua.
Hili jingine ni la asili, kwamba Askofu wa
Jimbo la Bukoba (mstaafu), Nestory
Timanywa, naye amefariki dunia katika
Hospitali ya Rufaa Bugando, Agosti 28,
mwaka huu. Nimelazimika kugusa kifo cha
Askofu Timanywa kwani mchango wake ni
mkubwa katika maisha yangu ya elimu. Ni
kupitia mkono wa Askofu Timanywa nilipata
ufadhili wa Shirika la Kijerumani la Misereor,
lililonilipia gharama za masomo yangu ya
Stashahada ya Juu ya Uandishi wa Habari
pale Nyegezi Social Training Institute
(NSTI).
Katika hili si mimi tu, wapo vijana wengi
kutoka Bukoba na mikoa mbalimbali ya
Tanzania walisaidiwa na Misereor kupata
masomo ya elimu ya juu. Ilifika mahala hata
wafadhili walipopunguza ufadhili kwa
asilimia 40, Baba Askofu Timanywa
aliniandikia barua niliyoitumia kupita katika
taasisi, nyumba na watu binafsi kuomba
kuchangiwa Sh 380,000 zilizokuwa
zinapungua kwenye ada.
Katika darasa letu tulikuwa na Wakenya,
Waethiopia, Waganda na watu kutoka

mataifa mengine huku tukifundishwa na
Wamarekani kwa wastani wa asilimia 70 ya
walimu wetu. Tulikuwa na mapadri na
watawa wengi, ambapo wengine sasa ni
viongozi wa juu huko AMECEA na
mwenzetu mmoja ni askofu. Kama si Askofu
Timanywa, nisingepata fursa ya
kufahamiana na familia hii kubwa ya
Nyegezi ya wakati huo na inawezekana
nisingepata fursa ya kutumikia Watanzania
kwa kiwango cha sasa. Raha ya milele
umpe ee-Bwana, na mwanga wa milele
umwangazie.
Sitanii, kwa kweli nawashukuru wasomaji
wangu maana baada ya makala ya wiki
iliyopita iliyokuwa na kichwa cha habari
kisemacho: ‘Tamu, chungu ya Magufuli’
nimepata mrejesho mkubwa ajabu.
Nimepata mawazo kutoka kambi zote za
kisiasa. Wale wa kutoka chama tawala na
wale wa vyama vya upinzani. Kwa uwiano,
asilimia kubwa waliunga mkono hoja
kwamba Rais John Magufuli anafanya kazi
nzuri katika ujenzi wa miundombinu, ila
wakataka arekebishe kidogo katika eneo la
uhuru wa kutoa mawazo/habari.
Wengi niliozungumza nao wamesema
bayana kuwa Rais Magufuli ataingia katika
historia ya nchi hii kama kiongozi aliyejenga

miundombinu na msingi wa uchumi imara
katika kipindi chake cha miaka 10. Kutoka
sehemu mbalimbali za nchi wengi
wamenihakikishia kuwa Rais Magufuli
anajenga miundombinu, na ni vema
nimnukuu mmoja kutoka Arusha, neno kwa
neno aliyenigusa: “Balile nimesoma makala
yako nimefurahi. Umeandika makala hii kwa
utulivu mkubwa. Umemtendea haki kweli
Mhe. Rais. Umeanza kwa kutambua
maeneo anayofanya vizuri na ukahitimisha
na maeneo anayostahili kufanya
marekebisho.
“Makala yako inalenga kujenga. Shida
ninayopata na makala nyingi za baadhi ya
waandishi na hata watu wanaochangia
kwenye magazeti mbalimbali, sioni
wakitambua kazi alizozifanya rais na
kumwambia aongeze au kupunguza nini. Hii
tabia waliyonayo baadhi ya watu ya
kumshambulia mwanzo – mwisho bila
kutambua juhudi anazofanya, inaweza
kumkatisha tamaa.
“Kwa kweli Balile kwa jinsi ulivyoandika hii
makala, hata yeye ataona una nia njema ya
kumwonyesha kuwa kumbe kama
asingeminya uhuru wa watu kutoa mawazo,
watu wa kawaida na waandishi
wangemwonyesha wezi wengi wako wapi,

wangetoa mawazo miradi ipi ipewe
kipaumbele au katika sera hii ya viwanda
nini kiongezwe kwenda kasi zaidi.
Nakupongeza sana na naomba uendelee
hivyo.”
Msomaji mwingine kutoka Mtwara,
akaniambia kitu nilichoambiwa na mtu
aliyeko Arusha na mwingine aliyeko
Karagwe. Akasema: “Kwa kweli kwa lugha
laini kama hii, inayofikisha ujumbe bila
kukera naomba umwambie Mhe. Rais
Magufuli kuwa sisi Watanzania sote
tunapenda maendeleo. Tunampenda
kiongozi anayeishi maisha yetu.
“Nakumbuka mke wake aliugua akalazwa
Muhimbili. Sikuwahi kusikia kwa marais
waliotangulia hili likitokea isipokuwa
Mwalimu Nyerere. Angalia dada yake
amefia Bugando. Wengine tungekuwa
tunasubiri maiti kutoka India kwa sasa. Mimi
nadhani Mhe. Rais Magufuli anastahili
pongezi, ila hili lisituzuie kumsahihisha
maana bila kufanya hivyo anaweza kujikuta
anapotea njia.
“Sasa mimi nina ombi moja. Naomba kupitia
Gazeti la JAMHURI umwambie Rais
Magufuli aanzishe sera kama ya wakoloni.
Hili halitamgharimu hata senti tano. Aweke

sera kuwa kila atakayejenga nyumba ya
kuishi lazima awe na tenki la maji
lisilopungua lita 5,000. Watu wavune maji
ya mvua. Hapa Mtwara au sehemu zenye
milima kama Karagwe, Kagera njia rahisi ya
kumaliza tatizo la maji ni kuvuna maji ya
mvua. Hili mkoloni alilifanya, naamini
Serikali yetu ya taifa huru haliishindi.”
Naamini ujumbe wako nimeufikisha
mpendwa msomaji.
Sitanii, wapo walioniambia dhana ya rais
kusaidia kisera katika uwekezaji wa
viwanda vya kuongeza thamani mazao ya
kilimo. Hawa wengi wamenieleza kuwa
matunda na vyakula tunavyovizalisha sasa
kama mazao ya chakula yana nafasi ya
kuzalishwa kibiashara na kuleta faida
kubwa katika familia nyingi. Wengi
wanaunga mkono wazo la viwanda.
“Zamani kule Moshi na Bukoba, kila familia
ilikuwa na kiwanda kidogo cha kukoboa
kahawa, ile mashine ya mkono ya
kuzungusha. Tulipaswa kuanzia pale na
kusonga mbele…” mwingine ameniambia.
Kwa kweli, wakati Watanzania wakisifia
hatua hizi, hawakusita kusema Rais
Magufuli anawadekeza wakuu wa mikoa
wanne, akiwamo Paul Makonda. Hawa
watatu nitawataja wakati ukifika, ila wawili

wapo Kaskazini na mmoja Kusini. Hoja zao
zilikuwa ni sakata la makontena ya
Makonda na jeuri au kiburi
anachokionyesha dhidi ya Waziri wa Fedha,
akisema angemweleza rais.
Sitanii, inawezekana Rais Magufuli hupati
muda wa kupita vijiweni, lakini huko ‘saiti’
Makonda alifikia hatua ya kuitwa ‘Naibu
Rais’. Wakati ule umempatia ulinzi mzito,
akipita barabara zinafungwa, wapo
waliowaza kuwa labda Makonda unamjali
kuliko hata watoto wako wa kuzaa! Wengi
wakahoji ukimya wako juu ya sakata hili.
Tena alipojitokeza Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk. Philip Mpango, kupingana na
Makonda, wakasema si muda mrefu
yatamkuta yaliyompata Nape Nnauye.
Wamekumbusha mengi likiwamo la
Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe, kwamba
huenda kama si Makonda ‘kumchongea’
kwako ukakubali kumtumbua hadharani,
angekuwa hai hadi leo.
Wamenipigia baadhi ya wauza magari Dar
wakadai Makonda alitaka magari yote
yauziwe Kigamboni kwenye viwanja
vivyomilikiwa na marafiki zake kama njia ya
kuwatengenezea pato. Sasa wanasema
amegombana nao hao ‘marafiki zake’ na

mpango wa magari kuhamishiwa Kigamboni
umekufa. Tena wapo walioniambia kuwa
hivyo viti na masofa kwenye makontena
havikosi mkono wa marafiki zake hao,
ambao kwa sasa hawapikiki chungu kimoja!
Sitanii, kadiri siku zilivyopita nilianza
kuuamini ‘unyunyu’ huu wa mtaani.
Mengine wanayosema yanaogopesha
kuyasanua hapa, maana yanaweza kuhitaji
uthibitisho. Mimi ninachojua Rais
Magufuli SI MPIGA DILI na wala hawezi
kuwa na wakala wa ‘kumchukulia mzigo.’
Kwa kweli tumesikia mengi na mioyo ikawa
inauma.
Hata hivyo, kidogo kidogo tukaanza kuona
tofauti. Nikasikia umemwondolea ulinzi wa
kikosi maalumu Makonda. Barabarani
nikageuka siku moja nikaona tuko naye
kwenye foleni moja karibu na Salenda
Bridge. Baadaye, siku unawaapisha kina
Ally Hapi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
ukashusha nyundo ya kwanza kwa Mkoa
wa Dar es Salaam jinsi ulivyoshindwa
kukusanya kodi. Hili lilinishtua kidogo.
Nikajisemea moyoni kuwa au Mhe. Rais
hakumaanisha hili?
Sasa mzee ukiwa Chato ndiyo umeua
bendi. ‘Unyunyu’ tuliokuwa tunaupata chini

kwa chini kuwa sasa hivi wewe na Makonda
haziivi kutokana na matendo yake
yasiyokuridhisha, ukaukoleza. Wapo
waliodhani ungefanya mbinu akapata fedha
halafu akaonekana amelipa hiyo kodi Sh
bilioni 1.2, lakini kwa kumtaja wazi Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam ukamtaka alipe
kodi na kumweleza mipaka ya mamlaka
yake kuwa kimo chake hakimvuki Waziri wa
Fedha, umetenda vema.
Sitanii, kauli yako hii imefifisha tabia
aliyoianzisha Makonda ikapokewa na
wakuu wa mikoa wengine watatu
wanaowadharau mawaziri wako na kusema
hadharani kuwa mawaziri wako chini ya
mkuu wa mkoa kimamlaka. Cyprian Musiba
huwa ananikera baadhi ya nyakati, lakini
nilipoona kwenye ‘clip’ yake akimwambia
Makonda kuwa yuko chini ya Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, nikakumbuka maneno ya
Wakurya wanaosema: “Amang’ana
gasarikire (mambo yameharibika).”
Nihitimishe makala hii kwa kusema jambo
moja la msingi. Kwamba dunia iliwahi
kujaribu mfumo wa kila mtu katika nchi au
himaya fulani kuwa na mamlaka kama
kambale, ambapo mdogo ana sharubu na
mkubwa ana sharubu. Walipata tabu sana.

Ni katika hatua hii nchi zilichagua mfumo wa
utawala wa sheria. Kwamba kila kiongozi
ajue mipaka ya madaraka yake na atende
kwa mujibu wa sheria. Tukilishika hili, wala
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola,
hatakuwa na kazi ya kuwataka polisi
wakatae amri za kusweka ndani kila
anayetofautiana na mkuu wa wilaya au
mkuu wa mkoa kwa saa 48.
Mwisho kabisa, Mhe. Rais nasema kutoka
kwenye sakafu ya moyo wangu kuwa
kishindo unachokiona cha jamii, vyombo
vya habari vya ndani na vya kimataifa
vikikushangilia kwa uamuzi wako wa
kumtaka Makonda alipe kodi na ukirejea
vifungu vya sheria umejijengea heshima
kama rais asiye na upendeleo wala uonevu
kwa yeyote. Umeithibitishia dunia katika hili,
kwamba kila mtu anapaswa kutii sheria.
Hongera Rais Magufuli kwa kuipa nafasi
sheria hata kwa wanaodhaniwa ni marafiki
zako wa hali ya juu kama Makonda.
Tukutane wiki ijayo.

Mwisho