Mara baada ya Uhuru baadhi ya wageni kwa dharau za makusudi kabisa walijaribu kuchezea uwezo wa Serikali ya Taifa letu huru. Nitoe mifano ya dharau za namna hiyo.
Siku chache baada ya Uhuru mkoani Lindi alitokea mzungu fulani alimvalisha mbwa wake beji ya Taifa kama alama ya kukejeli uhuru wa nchi hii. Serikali ilipopata habari ile kutoka kwa wananchi wazalendo ikamfukuza mzungu yule katika muda wa saa 24 asionekane katika ardhi ya Tanganyika . Na kweli alirejea kwao Ulaya!
Huko Korogwe nako mwaka 1963, nafikiri, mkuu mmoja wa mkoa (Jacob Namfua) alikataliwa huduma za chakula pale Korogwe Travellers Inn- hoteli ya wazungu walima mkonge mkoani Tanga. Serikali iliifunga hoteli ile na mwenye hoteli alifukuzwa nchini katika muda wa saa 24.
Hapa Dar es Salaam katika Hoteli ya Palm Beach , Meneja wa hoteli hiyo aliwanyima huduma wananchi (Waafrika) kwa dharau na kebehi eti walikuwa ‘nyani’ kasoro mikia. Serikali yetu ilipata taarifa ile, ilimfukuza yule meneja kwa muda wa saa 24 aondoke nchini Tanganyika aende kwao Ulaya, na kweli aliondoka.
Matukio hayo matatu ninayoyakumbuka yalileta heshima kubwa kwa wote waliofikiria Uhuru wa Taifa hili ulikuwa wa kuchezewa! Wageni wote wakawa na adabu.
Hapo Mwalimu alikuwa hatanii juu ya kulinda heshima ya Mtanganyika. Mara tu tulipopata Uhuru, basi tukawa RAIA HURU kweli katika nchi yetu.
Lakini siyo kwa wageni tu, hata baadhi ya wananchi walifikiria bado mzungu anatawala na kwamba Mwalimu Nyerere na Serikali yake walikuwa vibaraka tu. Mifano hai ni hii; kule Songea mwaka 1963 Mhindi mmoja wakili wa Lindi, lakini mtoto wa Songea ukoo wa Pardhani – alimdharau Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma hadharani karibu na Bomani. Kamati ya wakuu wa Idara Mkoa, (nami nikiwa Mkuu wa Shule -Headmaster) wa shule ya Sekondari Wavulana Songea) tuliitwa kuelezwa kisa chote na tukaridhika kulikuwa na dharau ya makusudi – uamuzi wa Serikali kwa Mhindi yule ulikuwa kufukuzwa.
Alihamishwa siku ile ile kutoka Songea (kwa ndege ya Serikali) na kupelekwa Sumbawanga – adhabu namna ile iliitwa “RUSTICATION”. Sijui alikaa muda gani huko Sumbawanga, lakini adhabu ile ilipomalizika inasemekana yule Mhindi alikimbilia Canada sijui ya huko.
Aidha, kule Shinyanga, chifu mmoja wa Wasukuma alidharau Serikali, naye alihamishwa kutoka Shinyanga akatupwa Tunduru miaka ile ya 1963 – 1964. Huyo nilizungumza naye mara kwa mara pale Tunduru maana nilimfahamu.
DC wa Tunduru miaka ile alikuwa anaitwa Zuberi Lukoya aliwahi kusema huyu chifu anatambua uwezo wa Serikali ya Nyerere na anaomba sana asamehewe. Ulipomalizika muda wa adhabu yake hiyo ya “Rustication” – hakurudi kwao Shinyanga – alihamia Nairobi , Kenya ; sana sana alitembelea Moshi tu. Lakini alinyooka na kujua utawala upo!
Labda niongeze mfano mwingine. Mzee mmoja, mswalihina kule Lindi alionyesha dharau na uchochezi mwaka 1964. Mswalihina huyu Serikali ilimhamishia Mkomazi mkoani Tanga.
Adhabu yake ilipokwisha hakurudi kwao Kusini, Lindi bali alilowea Dar es Salaam . Watu walijua Serikali ipo, ina uwezo na isichezewe chezewe.
Watu tukawa sasa tumejenga nchi ndiyo maana kukawa na amani na maendeleo ya haraka kati ya mwaka 1962 – 1970. Hapa nimeonesha uwezo wa mhimili wa utawala, kujenga amani, heshima na utulivu kwa Serikali kwa kufuata sheria ili tuishi kwa amani.
Kwa mazingira ya wakati ule ilibidi kuhalalisha uamuzi wa namna hiyo kwa kutunga sheria kuonesha wakubwa kwamba hakuna upuuzi hapa (Nyufa uk. 15 – 17 juu ya rushwa).
Lakini vipi sasa mbona mambo hayaendi tulivyotarajia? Wanasiasa baada ya kuona kila walipovunjiwa heshima wakosaji wamechukuliwa hatua kali kulinda heshima ya utawala wakaingilia kuvuruga uti wa mgongo wa utawala bora. Huu uti wa mgongo tunaita “the rule of law”- utawala wa kisheria. Huo utawala wa kisheria una taratibu na kanuni zake hapa nchini.
Upo MSAAFU WA SHERIA ZA UTAWALA BORA huu tuliuita “GENERAL ORDERS” za Serikali. Msaafu huu umetengeneza kanuni zake za utekelezaji zikiitwa “standing orders” na nyaraka za mara kwa mara zikiitwa “Establishment Circulars”. Kwenye dini tuna vitabu vya imani zetu – Wakristo, Biblia; Waislamu, Qur’an Tukufu.
Humo kumeelezwa yote yale Bwana Mungu wetu anataka sisi viumbe wake tuyatekeleze ili hatimaye tufike kwake mbinguni. Mungu alimpa Nabii Musa kule jangwani katika mlima wa Sinai amri 10 katika mawe mawili.
Jiwe moja lilikuwa na amri tatu zinazomhusu Mungu mwenyewe, jiwe la pili lilikuwa na amri saba zinazohusu uhusiano na binadamu wenzetu. Si mnajua hayo? Rejeeni Biblia kitabu cha Mwanzo sura ya 20 aya 1 – 17.
Katika Qur’an Tukufu ipo mistari au aya zinazoonesha maagizo ya Mungu wetu kwa wanadamu; mathalani ile sura ya 40 (XL uk. 461) inayoitwa Moamin aya Na. 53 ninasema “and certainly we gave Musa the guidance and we made the children of Israel inherit the Book” – yaani hakika tumempa Musa mwongozo na tulifanya wana wa Israeli warithi wa kitabu” kile. Tena katika aya ile ya 62 tunakuta maneno kama hayo “that is Allah, your Lord, the Creator of everything, there is no God but He, “… Huyo ni Mungu, Bwana wako, Muumba wa vitu vyote, hakuna Mungu mwingine ila yeye tu…” Hii ilikuwa kuweka utawala bora duniani ili binadamu tuishi kwa upendo na amani huku tukimcha Muumba wetu aliyetuweka hapa duniani.
Vivyo hivyo, Taifa linakuwa na Serikali inayoweka taratibu kwa raia wake kuishi kwa utulivu na amani. Kuna kitu kinaitwa Civil Service – utawala; ambacho kinatunza na kusimamia taratibu za kuendesha Serikali kila siku. “Civil Service” ndicho chombo kinacholinda na kusimamia General Orders.
Kwa kifupi kabisa kitabu hiki cha General Orders kilitamka hivi, na nukuu “…these General Orders contain the conditions of Service of Civil Servants and other employees of the Government of Tanganyika…” Ndiyo kusema kanuni hizi zinaelekeza masharti ya utumishi kwa wafanyakazi wa Serikali na wa umma katika nchi yetu.
Lakini GOs hizi zinatoa angalizo kwa maneno namna hii, namnukuu tena; “…furthermore, although these orders are intended to provide a fair and equitable answer to all the ordinary problems of Service Administration and Establishment, no regulations, however carefully framed, can hope to cover every eventually and every set of circumstances…”. Hii ilikuwa na maana kuelezea kuwa kanuni hizi hata zingetengenezwaje, haziwezi kukidhi kwa ukamilifu mahitaji yote kwa wote na katika hali zote hapa nchini. Kwa maelezo namna hiyo, basi ni dhahiri kitabu kile cha General Orders kilikuwa MWONGOZO muhimu sana kwa utumishi serikalini kuendesha utawala bora.