Watanzania tuna ugonjwa mmoja mbaya sana. Ugonjwa wa kutokuhoji lolote. Hatuna utamaduni wa kuhoji vitendo na kauli tata za viongozi na watawala wetu. Tumeridhika kuwa liwe liwalo; au yote maisha.
Kutokana na hali hiyo hatuna na hatuoni sababu za kuwawajibisha viongozi waongo, wazushi, matapeli na mafisadi. Matokeo yake viongozi na watawala hawa wamekuwa wakitumia udhaifu wetu wa kutokuhoji kufanya watakavyo.
Tumekubali kuwa watumie ufisadi, uongo na uzushi wao kupata utukufu. Leo hii ukiangalia CV za wabunge na mawaziri wetu kwenye tovuti ya Bunge letu utashangaa. Wengi ni waongo! Utakuta wengine wametaja kupata taaluma zao kwenye vyuo ambavyo havipo, au kuwa na sifa za kitaaluma ambazo hazijawahi kutokea humu duniani! Hawa ndiyo watunga sheria wetu. Hakuna anayehoji. Tuachane na hayo.
Lazaro Nyalandu, James Lembeli na Peter Msigwa wamekabidhiwa dhamana kubwa sana. Iwe dhamana hizo wamekabidhiwa kwa kuzingatia taratibu na misingi inayokubalika, au wamezipata kwa kutumia ujanja ujanja, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba wana dhamana muhimu sana kwetu. Dhamana ya kutunza maliasili kwa faida ya kizazi hiki na kijacho kwa sasa ni yao.
Kwa kuwa dhamana hiyo wanayo, na kwa bahati nzuri wanagharimiwa na walipa kodi wa nchi hii ili kufanya kazi hiyo, ni juu yetu Watanzania kuhoji kama wanatekeleza wajibu wao vilivyo. Na kama hawakidhi matarajio yetu, wanaendelea kufanya nini?
Makala hii inajaribu kuhoji kwa kujielekeza katika kauli walizowahi kuzitoa viongozi hawa katika nyakati tofauti ambako wamewahi kudai ‘laivu’ kuwafahamu majangili. Hata hivyo, walipotakiwa kutaja majina yao hakuna hata mmoja aliyethubutu kufanya hivyo zaidi ya kutoa kauli za ubabaishaji. Inasikitisha kwamba hata kauli hizi zilipotamkwa mbele ya Bunge letu, hakuna mbunge aliyewataka wahusika kuwa wazi na kuwataja majangili hao.
Nianze na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Lembeli. Kwa muda sasa amekuwa kimya kwenye mijadala inayohusu mambo ya wanyamapori. Wapo wanaodai kwamba amelazimika kuwa ‘mpole’ kutokana na kuumbuliwa pale madudu yake yalipowekwa hadharani. Wanasema kuwa matendo yake yamekuwa kinyume kabisa cha mahubiri yake yaliyomfanya aonekane mzalendo, mkweli, mcha Mungu na mwadilifu mbele ya jamii. Wanaeleza kugundua kwamba Lembeli si msafi.
Itakumbukwa kuwa Lembeli amekuwa kama mungu-mtu. Amejijengea mazingira, kama siyo ya kudharauliwa, basi ni ya kuogopwa sana na wanasiasa na watendaji ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Katika juhudi zake za kujipambanua kama mtu anayechukia ufisadi na ujangili, amewahi kusema na kunukuliwa na vyombo vya habari mara kadhaa akidai kuwa vigogo wakubwa wa Serikali wanaongoza kwa kujihusisha na biashara ya pembe za ndovu.
Akaeleza kwamba hali hii imesababisha mpango wa kuwadhibiti majangili kukwama kwa miaka mingi. Aidha, Lembeli amekuwa akilalamika kuwa wabunge wamepiga kelele kwa muda mrefu kuhusu tatizo la ujangili wa kuua ndovu, lakini Serikali imewapuuza kwa kuwa vigogo wake ndiyo wanaohusika.
Lembeli, katika hali ya kuunadi utakatifu na ucha-mungu wake, akadai kuwa anasubiri nguvu za Mwenyezi Mungu kuwaadhibu watendaji wa Serikali wanaoshindwa kudhibiti mauaji ya wanyama hao katika mbuga na mapori ya akiba ingawa wanajulikana. Hapa ninajiuliza, kama anawajua, nini kinamzuia asiwataje?
Desemba 20, mwaka jana, wakati anawasilisha taarifa ya Operesheni Tokomeza bungeni, Lembeli alidai kuwa na majina na ushahidi wa wabunge na vigogo wanaojihusisha na biashara ya pembe za ndovu. Alipoulizwa na waandishi wa habari sababu za kutokuweka majina ya wabunge hao katika taarifa hiyo, alisema: “Hiyo haikuwa kazi yetu. Sisi tulikuwa na wajibu wa kueleza yaliyotokana na Operesheni Tokomeza tu, lakini hayo mengine yapo kwenye viambatanisho.”
Majibu haya ya Lembeli yanatia kichefuchefu. Haiyumkiniki kwamba hili la kuwataja wabunge na vigogo majangili lisiwe kazi yao, lakini lile la kutetea waporaji wa kitalu cha Makao WMA kule Meatu liwe moja ya kazi zao! Hili la pili lina uhusiano gani na Operesheni Tokomeza? Je, nani alimtuma kufanya kazi hii? Huu kama siyo unafiki uliochagizwa na ufisadi, ni nini?
Je, kwa kudai kuwa majina yako kwenye viambatisho ndani ya Ofisi ya Bunge anatupa ujumbe gani kuhusu Bunge letu? Kwamba ni kichaka cha kuficha majangili? Kama ni msafi, mbona hajatangaza kujiuzulu kuonesha kuchukizwa na upogo huu wa Bunge? Vyovyote itakavyokuwa, ni dhahiri kwamba kwa kauli za Lembeli, anawajua majangili wa ndovu nchini. Tunataka awataje. Narudia awataje au akiri kuwa alikuwa mwongo, mzushi na alitumia hiyo kama gea ya kujijengea umaarufu. Kwa maana hiyo, ajiuzulu nyadhifa zake kwa kuwa viatu vya uongozi wa umma vinampwaya.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu, alikanusha vikali tuhuma kuwa viongozi wa Serikali na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanajihusisha na ujangili. Kukanusha huku kulitokana na makala iliyoandikwa na Martin Fletcher wa gazeti la the Daily Mail on Sunday la Uingereza (Februari 8, 2014).
Kutokana na kukanusha huko kwa Nyalandu, Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Msigwa, aliibuka akiitaka Serikali kutoa majibu sahihi kuhusu kilichoandikwa na gazeti la the Daily Mail akidai kuwa maelezo yaliyotolewa na Nyalandu yalijaa siasa, uzushi na uongo. Akasema ukweli lazima uwekwe wazi kwa sababu wanaohusika na biashara hiyo ni baadhi ya watendaji wa Serikali, wafanyabiashara na vigogo wa vikosi vya ulinzi na usalama nchini.
Hata pale Nyalandu, katika hali ya kushangaza, alipoamua kumwalika nchini mtuhumiwa wake Fletcher kwa gharama kubwa za Serikali, Msigwa alirudia tena kuituhumu Serikali ya CCM akidai kuwapo “mtandao wa mauaji ya ndovu unaohusisha Ikulu, wanasiasa, polisi, maofisa wanyamapori na wanajeshi.” Kwa kauli za Msigwa, hakuna chembe ya shaka kwamba naye anawajua majangili! Tunaomba aweke wazi majina na ushahidi ili umma tujue. Vinginevyo naye atangaze kuwa ni mwongo na kwamba anajitafutia umaarufu tu au amewekwa mfukoni na Nyalandu na majangili.
Katika hali ya kushangaza Februari 27, mwaka huu, Nyalandu akarudia kauli aliyoitoa akiwa Uingereza, pale alipodai mbele ya vyombo vya habari nchini kwamba Serikali ina zaidi ya majina 320 ya majangili; na kwamba wangeyaweka hadharani wakati wowote. Aliyasema haya punde tu baada ya kurejea kutoka London kwenye mkutano wa ‘kutafuta msaada’ wa kupambana na majangili. Utajiuliza, kama majangili wanafahamika, London alifuata nini? Waje watusaidie kuwakamata wahalifu tunaowajua tayari? Ni kweli kwamba vyombo vyetu vya dola vimeshindwa?
Nyalandu, katika hali iliyofanya baadhi ya watu kuhoji endapo kuna Lazaro Nyalandu wawili Maliasili, alijikana mbele ya waandishi wa habari Julai 10, mwaka huu. Hii ilikuwa mara tu baada ya kumalizika kwa mkutano wa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, na Waziri wa Afrika wa Uingereza, Mark Simmonds.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Uingereza, namna ya kuzuia uwindaji haramu pamoja na Waziri Simmonds kupata mwanga halisi juu ya hali ya usalama na amani kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na zile za Maziwa Makuu.
Nyalandu, alijikoroga wakati akijibu swali la mmoja wa waandishi aliyetaka kujua ni ushirikiano gani anautaka katika kukabiliana na ujangili, ilhali Serikali imeshindwa kuweka hadharani majina ya majangili 40 ambao Rais Jakaya Kikwete alisema wanawafahamu na kinara wao yuko jijini Arusha, pamoja na ile orodha yake ya 320 aliyosema angeitaja wakati wowote na kwamba angeiweka kwenye mbao za matangazo?
Majibu ya Nyalandu yakawa eti Serikali haiwatambui watu hao kwa majina, bali kwa matendo yao na kwamba, utambuzi huo ulitokana na kikosi kazi kilichoundwa kutoka vyombo vyote vya ulinzi na kutoa taarifa yao. Haya ndiyo majibu ya Waziri mwenye dhamana!
Swali linalokuja hapa ni je, Nyalandu anajua kweli anachokisema? Aliposema atatangaza na kuweka hadharani alikusudia kuweka ubaoni vitendo na siyo watu? Kwani nani hajui kuwa vitendo vya ujangili vipo? Lakini je, ni kweli vitendo hivyo vinaweza kuorodheshwa vikafikia 320? Pengine, swali hili si zuri sana, lakini nashindwa kuliepuka — huu kama si uhuni ni nini?
Naamini kwa dhati kuwa Nyalandu anawajua majangili, na kwamba ana wajibu wa kuwataja na kuwachukulia hatua kama kweli ni msafi. Vinginevyo lazima kuna kitu. Hasa tukirejea tuhuma ambazo zimekuwa zikiandikwa magazetini dhidi yake kwamba naye ni mmoja wa majangili papa; kwamba siku alipoteuliwa kuwa waziri majangili papa wa Arusha walifanya sherehe; kwamba kitendo cha kuwavua madaraka waliokuwa wakurugenzi (Alexander Songorwa na Jafari Kadegesho) na kuwateua watu waliokuwa wanatajwa kama manabii wa ujangili, kilikuwa na nia ya kuimarisha safu yake ya ujangili.
Aidha, Nyalandu atajitetea vipi dhana iliyozuka kwamba kitendo chake cha kugomea mabadiliko yaliyofanywa na Ikulu kwenye Idara ya Wanyamapori majuzi tu, ni moja ya mbinu za kuhakikisha kuwa watu hawa wanamsaidia kufanikisha shughuli za ujangili?
Ni vema Nyalandu akajua kuwa wimbo wake anaoimba kila siku akiwa Serena Hotel wa “Tutawasaka, tutawakamata popote walipo” umechuja mno. Nashauri atafute mwingine. Tumechoshwa na mikutano na Wazungu inayofanyika kwa gharama kubwa kila siku Serena Hotel na Marekani huku wanyama wakiwa wanaisha maporini.
Tumechoka kusikia hadithi za misaada ya ndege na helikopta (zinasemekana kuwa ni vyuma chakavu!) wakati wahalifu wanafahamika. Je, tunahitaji helikopta kuwasaka majangili ambao Lembeli na Msigwa wametuambia kuwa ni wabunge na vigogo wa Serikali ambao Nyalandu ana orodha yake ya majina 320 tayari? Tunahitaji mikutano mikubwa na Wazungu wakati Waziri, Lembeli na Msigwa wanawajua majangili?
Ninachoweza kusema bila woga, ni kwamba hakuna dhamira ya dhati ya kupambana na ujangili nchini. Ndiyo maana unakuta hawa tuliowapa dhamana kupitia serikalini, bungeni na kwenye vyama vyao wameamua kukaa na kuunda UTATU wa kifisadi au kama walivyowahi kuandika wengine, Mtandao wa Shibe.
Si Lembeli wala Msigwa atakayethubutu kumhoji Nyalandu juu ya ile orodha ya majangili 320. Wala Nyalandu hawezi kumdadisi Lembeli wala Msigwa juu ya majina ya vigogo wanaowafahamu kuhusika na ujangili. Wanajua kuwa wanachohitaji ni shibe. Kama tembo watakwisha mwaka kesho si kazi yao! Wamepiga kelele wameshapata mradi wao, sasa wametulia.
Ni jukumu la watu wenye mapenzi mema na nchi yetu, rasilimali zetu na vizazi vyetu vitakavyokuja, kupaza sauti na kuhoji sababu ya mabwana hawa kutumia pesa zetu kama mtaji kujitafutia utajiri na utukufu wakati rasilimali zetu zinateketea.
Niwakumbushe Lembeli na Msigwa kwamba ni vigumu mbwa kubweka kwenye maboma mawili kwa wakati mmoja. Hawawezi kutudanganya kwamba wanasimamia rasilimali zetu huku wakishiriki katika michezo michafu inayoteketeza rasilimali hizo.