Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Misungwi
Takriban mwezi mmoja tangu kutangazwa kufutwa kwa timu ya soka ya Gwambina ya Misungwi mkoani Mwanza kwa madai ya mmiliki wake kukerwa na mwenendo wa maofisa wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), undani wa tukio hilo umeanza kuibuka.
Gwambina FC ilikuwa ikidaiwa kumilikiwa na Mbunge wa Misungwi, Alexander Mnyeti, baada ya kuinunua timu ya JKT Oljoro ya Arusha na kuipandisha hadi Ligi Kuu Tanzania Bara.
Januari mwaka huu, Mnyeti alikaririwa na chombo kimoja cha habari akiwatuhumu maofisa wa TFF kumwomba rushwa ili ‘timu yake’ iutumie Uwanja wa Gwambina.
Tuhuma za Mnyeti kwa TFF zilizua malumbano ya muda huku Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo, akimtaka kuwataja maofisa hao ili kulisafisha shirikisho, kitu ambacho hakijatangazwa kuwa kimefanyika hadi leo.
Gwambina FC iliibuka ghafla miaka michache iliyopita na kuwa moja ya klabu chache za soka nchini zinazomiliki uwanja wa mazoezi na mechi za ndani, lakini ikadorora ghafla, ikashuka daraja na baadaye kufutwa kwa kauli ya Mnyeti na kuwaruhusu wachezaji wake kwenda wanakotaka.
JAMHURI limetembelea uwanja huo mapema mwezi huu na kuzungumza na wananchi kadhaa wa Misungwi, wengi wakihofia kutaja majina yao.
“Hii timu imekufa kutokana na ubishi wa mheshimiwa (Mnyeti) alitakiwa aiache kwa wananchi. Mkoa wa Mwanza hauna timu Ligi Kuu, angeweza kuitoa hata mkoani,” anasema kijana mmoja dereva wa bodaboda katika mazungumzo yaliyofanyika Hoteli ya All Seasons, Misungwi.
Anasema wakati timu ikiwa Ligi Kuu vijana walijipatia kipato kwa kuwasafirisha mashabiki wa soka waliofika Misungwi kutazama mechi, hasa zile kubwa.
Kauli yake inapingwa na mzee mmoja hotelini hapo, akisema sababu ya kudorora kwa timu ni Mnyeti kunyang’anywa usimamizi wake.
“Hakuwa mmiliki. Alikuwa akisimamia tu. Sasa mwaka 2021 mmiliki mwenyewe (anamtaja jina) akapata habari kuwa Mnyeti anataka kubadili hatimiliki ya ardhi ulipojengwa Uwanja wa Gwambina.
“Hilo halikukubalika. Kwa hiyo akamzuia kuisimamia klabu hiyo pamoja na Shule ya Sekondari Elpas iliyopo karibu na Uwanja wa Gwambina. Pia ipo baa iliyokuwa ikipiga muziki mkubwa sana inaitwa ‘Gwambina Park’ nayo amenyang’anywa.
“Ndiyo maana kwa sasa ni shule tu ndiyo inaendelea kutoa huduma kama kawaida ikisimamiwa na (anamtaja anayeisimamia) lakini uwanja na Gwambina Park vimefungwa,” anasema mzee huyo akisisitiza kuwa tangu alipojaribu kubadili hatimiliki ya eneo hilo, uhusiano na mmiliki halali wa eneo umedora kama si kufa kabisa.
JAMHURI limefika katika maeneo hayo na kushuhudia kudorora kwa huduma za Gwambina Motel, hoteli iliyopo katika Uwanja wa Gwambina.
Anasema kauli kwamba amekerwa kwa kuombwa rushwa na maofisa wa TFF, hata kama ni ya kweli, lakini si sababu ya kufa au kudorora kwa Gwambina na vitega uchumi vingine.
Watu wa karibu na mmiliki halisi wa mali hizo wamelithibitishia JAMHURI kuhusu kudorora kwa uhusiano wa Mnyeti na mmiliki, lakini hawakuwa wakifahamu nini kichosababisha.
Kuhusu umiliki wa klabu, Ofisa wa TFF, Ndimbo, ameliambia JAMHURI kuwa katika usajili si lazima klabu au timu imtaje mmiliki wake.
“Wao wanatuleta katiba yao. Wanasema huyu ni mwenyekiti na huyu ni katibu. Kwamba wanachama watakuwa na sifa hizi na hizi. Kwa hiyo mmiliki anaweza asitajwe moja kwa moja,” anasema Ndimbo.
Alipotafutwa kuzungumzia utata huo na tuhuma za yeye kudaiwa kutaka kubadii hatimiliki ya eneo uliopo Uwanja wa Gwambina, Mnyeti aling’aka na kusema:
“Nyie ni JAMHURI? Mimi siwezi kuzungumza na wahuni. Endeleeni kutumika na mpumbavu mwenzenu (anataja jina la mtu). Msiyaulizie mambo yangu wala ya Gwambina.”
Mapema mwezi huu, Mnyeti na wenzake wawili walifikishwa mbele ya Mahakama Kuu Kanda ya Babati kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Inadaiwa mahakamani hapo kuwa Mnyeti alitumia nafasi yake kumdhalilisha mfanyabiashara, Dk. Hamis Kibola na kumnyima haki za kibinadamu.
Mnyeti sasa anaiomba mahakama iiunganishe serikali katika mashitaka hayo, kwa kuwa wakati akifanya hayo yeye alikuwa mkuu wa mkoa.