Kifo cha Ofisa wa Idara ya Uhamiaji, Mkoa wa Rukwa, Chris Kanyama kimeibua utata na uhasama ndani ya idara hiyo nyeti nchini.

Vyanzo vya habari kutoka idara hiyo vinasema kwamba Kanyama kabla ya kifo chake kulikuwa na mlolongo wa matukio yanayozua maswali kwa ofisa huyo.

Akielezea hatua moja baada ya nyingine, mmoja wa maofisa anayefanya kazi katika idara hiyo ambaye walikuwa kitengo kimoja na Kanyama, anasema kwamba ofisa mwezake alikabidhiwa pikipiki na ofisi ili iweze kumsaidia  katika majukumu yake ya kazi.

Hata hivyo, pikipiki hiyo iliibwa nyumbani kwake hivyo aliogopa kutoa taarifa ofisini kwake na kuamua kuanza kufanya upelelezi binafsi ili aipate na kuirejesha ofisini, lakini kabla hajafanikiwa kuipata viongozi wake walipata taarifa hizo na kumkamata kisha kumfungulia kesi ya wizi wa kifaa cha ofisi.

Inaelezwa kuwa baada ya kufunguliwa mashtaka, aliomba ofisi hiyo impatie nafasi ya kuilipa kuliko kumshtaki kwa kosa ambalo binafsi hakuhusika nalo, lakini viongozi wake hao walimgomea.

Tukio hilo aliliripoti kwa ndugu zake ili wamsaidie kulipa deni hilo, kwa mujibu wa mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Adam Kanyama.

Adam aliyezungumza na gazeti hili anasema kuwa Julai, mwaka huu, kaka yake akiwa nyumbani kwake na mkewe, aliamka asubuhi akajiandaa ili aweze kwenda kazini, lakini pikipiki haikuwako ndani ya nyumba.

Alipomuuliza mkewe naye alisema hajaikuta ndani jambo ambalo lilisababisha mtafaruku na mkewe kuondoka nyumbani.

Aliamua kuitafuta pikipiki hiyo, na kuanzia wakati huo ofisi yake ilizuia malipo yake yote ikiwa ni pamoja na mishahara yake ya mwezi.

“Hivi tunavyoongea tangu mwezi wa saba mpaka sasa hakuwahi kulipwa mshahara wake wala malipo yake mengine, sababu ni upotevu wa pikipiki,” anadai Adamu Kanyama.

Anaendelea kusema kuwa alizungumza na kaka yake Chris Desemba 17, 2015  wakati akitoka mahakamani na kumweleza mwenendo wa kesi yake dhidi ya mwajiri wake (uhamiaji).

“Kaka aliniambia kuwa kesi yake ilisomwa, lakini upande wa mlalamikaji ulisema kuwa ushahidi haujakamilika jambo lililomfanya hakimu kufoka na kugomba kwa kusema kuwa hii kesi ni ya majungu hivyo tarehe 29 Desemba 29, 2015 atatoa hukumu,” anasema Adam.

Adam anasema kwamba Chris alipata kumuomba bosi wake kukutana naye ofisini kwake siku hiyo baada ya kutoka mahakamani na alimtaka amwandalie ripoti ya mwenendo wa kesi yake na kisha aipeleke ofisini jioni hiyo.

“Niliwasiliana naye saa kumi na moja jioni wakati amemaliza kuandaa ripoti hiyo, na kunieleza anakwenda ofisini kuonana na bosi wake, lakini jambo la kushangaza kesho yake Desemba 18, 2015 juzi majira ya saa nne asubuhi nilipokea simu kutoka kwa dada yetu Thabita kuniambia kaka alitekwa Desemba 17, na ameokotwa na polisi wa doria akiwa amepigwa, amekatwakatwa na mapanga na kuchomwa visu hali yake ni mbaya, lakini jioni alifariki,” anasema.

Kwa upande wake, Thabita anasema kuwa kifo cha kaka yake ni cha utata kutokana na jinsi alivyopotea katika mazingira ya kutatanisha pindi alipoaga kuwa anakwenda kukutana na bosi wake aliyemtaka kufanya hivyo.

Thabita anasema kuwa ofisi yake ndiyo chanzo cha kifo chake maana tangu kupotea kwa pikipiki hiyo kumekuwa na sintofahamu.

Aidha, baadhi ya wanafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam wanaeleza kuwa wameshangazwa na kifo cha mwenzao ambaye pamoja na kuwa na kesi hiyo, na kuomba kulipa pikipiki hiyo ofisi ilishindwa kumuelewa na kufanya kama ambavyo imekuwa ikifanya wa baadhi ya wafanyakazi ambao wamekuwa wakikumbwa na mikasa ya aina hiyo.

“Hivi tunavyoongea kuna mmoja wa viongozi wetu hapa makao makuu alipata hasara ya fedha za vibali dola za kimarekani 9,000. Lakini hakupewa adhabu yoyote zaidi ya kuambiwa azilipe na amepandishwa cheo ni Mkuu wa Idara wa Mkoa huko Kaskazini, huku ni kuoneana kwa watendaji walio chini wakati huko juu wanalindana,” anasema.

Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Rukwa (RIO), Seleman Kameya akizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki iliyopita, anasema kuwa akiwa safarini kuelekea Jijini Dar es Salaam alipata taarifa kuwa Chris ameokotwa akiwa amekatwa panga kwenye ulevi.

“Nikiwa Mbeya kuelekea Dar es Salaam nimeambiwa kuwa ameokotwa akiwa kwenye ulevi amepigwa panga nikawaambia wampeleke hospitali, lakini nikapigiwa saa mbili usiku kuwa amefariki,” anasema Kameya.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusiana na kesi ya pikipiki alikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai ya kuwa yuko nje ya ofisi.