Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Geita

“Kila mwanadamu ameumbwa kwa kusudi maalumu la mwenyezi Mungu” msemo huu hutumiwa sana na baadhi ya watu wenye imani tofauti wakimsifu na kumtukuza Muumba wao kwa matendo makuu aliyowatendea katika dunia tuliyomo.

Kuna watu wanafikiri uwepo wao au watu wengine wapo duniani kwa bahati mbaya jambo ambalo siyo kweli,hapa duniani hakuna aliyeumbwa kwa bahati mbaya.

Mchungaji Rick Werren,anasema “Hapo zamani kabla haujawa katika tumbo la mama yako ulikuwa katika mawazo ya Mungu”.

Ifahamike kuwa kila mwanadamu ni bora mbele za Mungu,japo sisi tunabaguana, kuchekana,kunyanyapaana, kutesana na wakati mwingine kujeruhiana na kujiona bora kuliko wengine.

Upo msemo wa mwanafalsafa Confucius, “Kila kitu kina uzuri,lakini siyo kila mtu anauona” msemo huo unadhihirisha kuwa wapo watu hupenda kukashifu wengine kwa mabaya tu pasipo kuona mazuri ya mtu.

Siyo ajabu kusikia mtu akimbeza mwingine kwa mwonekano wake kimaumbile,kihisia,kiakili, kisaikolojia na hata kumnyanyapaa mwenzake.

Mbali na hayo,Makala hii inajikita kuzungumzia changamoto za wanawake wenye tatizo la kutozaa(tasa) na madhira wanayopitia katika jamii.

MAONI YA WANANCHI

Ikumbukwe kuwa Mei 10, 2024 Penina Petro(70) mkazi wa kijiji cha Siwandete,kata ya Kiranyi,Arusha alijitokeza na kuangua kilio mbele ya mkuu wa mkoa wa Arusha,Paul Makonda,akiomba kusaidiwa na serikali kutokana na unyanyapaa anaofanyiwa na ndugu zake kwa sababau ya kutojaliwa kupata mtoto.

Penina, anaeleza kuwa amekuwa akinyanyasika na kwamba maisha yake yapo hatarini kutokana na nyumba anayoishi kuanguka huku ndugu zake wakikataa kuijenga kwa madai kwamba ameshazeheka na hana mtoto wa kulisi mali zake.

Kitendo hicho kimekuwa kikimsononesha na kujutia maisha yake hapa duniani licha ya kwamba hajui kusudi la Mungu kutompatia mtoto.

Veronika Michael,mkazi wa kibaha Pwani,anasema alijaliwa kupata mume miaka saba iliyopita lakini ndoa yake ilivunjika baada ya mumewe(jina tunalihifadhi) kudai kwamba hawezi kuishi na mwanamke asiyezaa.

“Niliishi na mme wangu kwa miaka mitatu pasipo kupata mtoto,nilikunywa dawa za Jadi na takribani mwaka mzima pasipo mafanikio,baadaye nilikwenda hospitali kufanya uchunguzi na kupewa dawa lakini sikufanikiwa kupata mtoto.

Baada ya jitihada hizo zote kufanyika bila mafanikio mume wangu aliniomba tuachane au aoe mwanamke mwingine,kwa kuwa sikupenda kuishi maisha ya uke wenza niliamua kurudi nyumbani kwetu” anasema Veronika.

Monica Masalu, mkazi wa kijiji cha msilale,anadai unyanyapaa kwa wanawake wenye utasa ni mkubwa sana katika jamii na kwamba hakuna jitihada zinazofanyika ili kundi hilo kupata faraja ya nafsi jambo linalowakatisha tamaa ya kuishi.

Nikutokana na maisha aliyopitia kuwa yenye misukosuko mingi tangu nyumbani kwao hadi kwenye jamii ambapo alikuwa akitukanwa na kusetwa kuwa ni tasa ndiyo maana mambo yake hayafanikiwi.

“Nikiwa nyumbani nilikuwa natukanwa naambiwa mwanamke gani wewe huna hata mtoto ndiyo maana huolewi, hata baadhi ya wanaume walikuwa wakiniambia ili wanioe lazima kwanza niwazalie mtoto,lakini pia wengine walikuwa wananiambia namhangaikia nani atakaye rithi mali zangu”anasema Monica.

Anasema unyanyapaa huo upo zaidi kwa jinsia ya kike licha ya kwamba hata wanaume wapo wasio na uwezo wa kuzalisha mtoto.

Mama Tamara kutoka Mombasa nchini Kenya anasema ilisalia kidogo sana aweze kuondoka katika ndoa yake baada ya kusimangwa na ndugu wa mume wake baada ya kutopata mtoto muda mrefu.

“Ukweli ni kwamba tamaduni nyingi za kiafrika kwa kiasi fulani zinawakandamiza sana wanawake pale wanapoolewa na kukaa muda mrefu bila kupata mtoto”.

“Ndugu, jamaa na marafiki hasa kutoka upande wa mume huanza maneno ya kejeli,kashfa,zarau na mengine mengi ya kuudhi kwenda kwa mke kisa tu hajajaliwa kupata mtoto jambo ambalo muda mwingi unakuta lipo nje ya uwezo wake”

Anasema kwake jambo hilo lilimtia uchungu sana moyoni mwake, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa na kiu ya kupata mtoto,na kwamba alikuwa akiona wivu kwa wanawake wengine mpaka pale alipofanikiwa naye kuzaa watoto wawili.

Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la “Engender Health” nchini Tanzania,Dkt. Moke Magoma, anasema kuwa changamoto ya suala la utasa na Ugumba linayakabili makundi yote kati ya wanaume na wanawake na kwamba hali hiyo husababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo magonjwa.

Dk. Magoma, ambaye pia ni Bingwa wa Magonjwa ya wanawake anasema kwa jamii ya kiafrika wanawake ndiyo wamekuwa wakinyanyapaliwa zaidi kuliko wanaume kutokana na jamii kubwa kuamini kuwa changamoto hiyo hulikumba kundi hilo kuliko wanaume.

Kwa mujibu wa Dkt. Magoma,Ugumba ni hali ya mtu kushindwa kupata mimba licha ya kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwenza wake, na sababu za kutokea hali hiyo inawekwa kwenye makundi manne muhimu ikiwemo tatizo kuwa upande wa mke,mume, wote pamoja au katika hali isiyoelezeka.

“Maana yake ni kwamba hali ya kutobeba mimba inaweza kusababisbwa na aslimia 30 kutoka kwa mwanamke, aslimia 30 mwanaume, aslimia 30 wote pamoja na aslimia 5 inatokea japo mara chache sana unakuta wote hawana shida yoyote isipokuwa mimba haitungi tu,ndiyo hiyo kitaalamu tunaita hali isiyoelezeka”anasema Dkt. Moke.

Anasema kwa wanawake wengi waliopo kwenye ukanda wa jangwa la Sahara hali ya kutobeba ujauzito hutokana na maambukizo kwenye milija ya uzazi na kwamba baadhi yao hushindwa kujua tatizo hilo mapema na badala yake hufahamu wakati hali imeshakuwa mbaya zaidi.

Kwa upande wa wanaume, hali hiyo hutokana na baadhi yao kushindwa kusimamisha uume kutokana na sababu mbalimbali jambo ambalo huwa vigumu kumwingizia mbegu za kiume mwanamke.

“Zipo sababu mbalimbali zinazoweza kumfanya mwanaume asitungishe mimba ikiwemo magonjwa ya kuambukiza ambayo huathiri mfumo wa uzalishaji wa mbegu kutoka kwenye korodani,kushindwa kusimamisha uume wake,kuwa na mbegu chache sana,kukosa kabisa mbegu au kuwa na mbegu za kiume zenye maumbile ya ajabu”.

“Bahati mbaya kwa mila zetu za kiafrika ikitokea hali hiyo anayetupiwa lawama huwa ni mwanamke pasipo kijiridhisha kuwa tatizo lipo upande upi,lakini inapotokea wote wakawa hawana tatizo lolote na mimba hazitungi hao huwa tunawashauri waendelee na maisha yao muda ukiwadia wanaweza kuona ujauzito unatokea” anasema Dkt. Moke.

Akielezea kuhusu Utasa,anasema sababu hazitofautiani sana kwa madai iwapo mwanamke akipata magonjwa kama ya Tetekuanga kingali akiwa mdogo chini ya miaka 18 inaweza kumsababishia utasa.

Kadhalika inapotokea mirija imeziba au kukosa uhimilivu kusafirisha yai la uzazi mwanamke hawezi kubeba ujauzito.

“Utasa pia unaweza kusababishwa na makovu katika mirija ya uzazi,makovu hayo yanauweka kuzuia yai la mwanamke kupita kwenye mirija au mbegu ya kiume kufikia yai”.

Mbali na hilo anasema ipo hali ya kimaumbile ambayo mwanamke anaweza kuzaliwa akiwa na mfuko ndogo au kutokuwa kabisa na mfuko wa uzazi jambo linalomfanya kutopata kabisa ujauzito.

Vile vile wanaume nao wanaweza kukumbwa na hali ya Utasa kutokana na sababu za kimaumbile ikiwemo kuzaliwa na uwezo mdogo wa kuzalisha mbegu,kutokuwa na mbegu kabisa,au kutokuwa na uwezo wa uume kusimama.

“Wanaume pia hukumbwa na tatizo la Utasa,kutokana na suala zima la uumbwaji,magonjwa kuambukiza kama zinaa na madawa ya kulevya hasa kwa waliokubuhu kwa uvutaji bangi japo siyo wote” anasema Dkt. Moke.

Hata hivyo anatoa faraja kwa wenye changamoto hiyo kuwa bado wanaweza kutibika ama kupata watoto iwapo watahitaji kuonana na madaktari Bingwa na masuala ya uzazi.

“Zipo njia mbalimbali za kutibu matatizo hayo ikiwa ni pamoja na kutoa dawa za kusaidia usafirishaji mzuri wa yai la mwanamke, kutibu magonjwa ya kuambukiza yanayosababisha kutoshika ujauzito pamoja na elimu sahihi za kulinda afya ya uzazi”

“Pia kuna njia ya kupandikiza mimba kwa njia ya ya kibaolojia ambapo mwanamke anaweza kupata ujauzito na kujifungua kwa njia za salama kabisa” anasema Dkt.Moke.

WAZIRI WA AFYA AELEZA MKAKATI WA SERIKALI

Akizungumza kwenye warsha ya uzinduzi wa utafiti wa haki ya afya ya uzazi kwa wanawake wa mijini na vijijini kupitia vyombo vya habari, julai 22,2023 Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu, anasema Tanzania imeridhia na kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo ina lengo la kuboresha afya ya uzazi,mama na mtoto.

Lengo namba 3 la Maendeleo endelevu ya milenia(SDG 3) Kipengele cha 7 linazungumzia upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi kwa wote.

Aidha kifungu namba 14(g) cha itifaki ya Maputo( Maputo Protocol) kinazungumzia haki za afya ya uzazi kwa wasichana na wanawake.

“Nchi yetu inatekeleza mikataba hiyo ya kimataifa kwa kuingiza masuala ya afya ya uzazi wa mama na mtoto katika mipango yake yote kuanzia mpango wa Maendeleo wa tatu wa miaka mitano(2021/22 – 2024/25) Mpango mkakati wa tano wa sekta ya afya(2021/22-2024/25) ambapo mipango hoi yote inatekeleza na wizara kupitia Mpango mmoja wa Taifa wa Afya ya uzazi,mama,mtoto na lishe” anasema Ummy.

“Mbali na mpango huo kuna Mpango maalumu wa uwekezaji katika afya ya uzazi Kwa vijana na kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto(National Accelerated Action and Investment Agenda for Adolescent Health and Wellbeing (NAIA-AHW) 2021/22-2024/25”.

Kadhalika akiwa katika uzinduzi wa kituo cha upandikizaji mimba cha Hospitali binafsi ya Kairuki(Green IVF) kilichopo Bunju jijini Dar es salaam,Waziri Ummy akasema tatizo la ugumba na utasa ni kubwa na upande wa serikali hakuna kituo hata kimoja kinachotoa huduma ya upandikizaji mimba ispokuwa vya watu binafsi.

“Uhitaji wa huduma ya upandikizaji mimba ni mkubwa nchini,Mhimbili ipo kwenye mpango wa kuanzisha lakini bado,vile vile serikali tunajenga hospitali ya mama na mtoto huko Dodoma na huduma hiyo itakuwepo,ila kwa sasa vipo vituo binafsi vitano tu hapa nchini”.

Anasema serikali bado haina takwimu sahihi za masula ya ugumba na utasa licha ya tatizo hilo kuongezeka siku hadi siku na kwamba ripoti ya afya ya miaka mitano ijayo takwimu hizo zitakuwa zimekusanywa.

SERA YA AFYA

Afya maana yake ni hali ya ukamilifu kimwili,kiakili,kijamii na kutokuwepo kwa maradhi, afya bora ni nguzo na raslimali muhimu katika kuchangia maendeleo ya mtu binafsi,familia na nchi hususani katika kuleta maisha bora na kupunguza umaskini.

Kwa mantiki hiyo afya inalenga kuwa na ustawi endelevu kwa jamii,kwa kuzingatia mchango wa mtu binafsi kulingana na nafasi,uwezo na fursa zilizopo katika kuleta maisha bora.

Upatikanaji wa afya bora unahitaji uwezeshaji wa jamii iwe na uwezo wa kushiriki,kuamua,kupanga na kutekeleza mikakati yao ya kuwaletea maendeleo katika ngazi mbalimbali.

Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali kuimalisha afya ya uzazi kwa wanawake,wanaume,watu wenye ulemavu,vijana na wazee.

Serikali itaandaa miongozo,mikakati,na kuratibu shughuli zinazolenga afya ya uzazi ya makundi mbalimbali pamoja na kuhakikisha huduma za uzazi wa mpango unatekelezwa.

Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha utoaji wa huduma bora za uzazi katika vituo vya kutolea huduma za afya zinazowavutia wanawake,wanaume na vijana.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Afya Ulimwengu (WHO), inaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya sita anakabiliwa na tatizo la Utasa.

Aidha ripoti hiyo imetoa wito kwa nchi kukusanya takwimu halisi kuhusu tatizo la utasa ili kuongeza mkakati wa kushughulikia suala hilo muhimu.

NINI KIFANYIKE ?

Baadhi ya wadau wa afya wametoa maoni mbalimbali huku Dkt. Moke Magoma, akipendekeza serikali kuifanyia maboresho sera ya afya ili kuwaruhusu madaktari Bingwa na bobevu kutoa huduma za afya kwa wanawake kuanzia vituo vya afya,wilaya,rufaa na Kanda.

Serikali iajili wataalamu wa saikolojia na madaktari wa afya ya akili na kuhakikisha wanasambazwa kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za kanda.

Serikali ihakikishe inakusanya takwimu halisi za wanawake wenye Utasa na ugumba hatua itakayoweza kuongeza jitihada za kulihudumia kundi hilo kuliko ilivyo sasa.

Serikali na wadau wengine wa afya wasaidie kutoa elimu kwa jamii ili kuondoa unyanyapaa kwa watu wenye ugumba na utasa.

Wanawake wenye changamoto ya kutobeba ujauzito washauriwe kwenda hospitali ili kufanya uchunguzi na matibabu ya ugumba na utasa badala ya kuamini kuwa wamelogwa.

Viongozi wa dini wasaidie kutoa mafundisho mema kwa waumini wao ili kuondoa Imani potofu kwa jamii kuhusiana na Ugumba na utasa.

                                         

Please follow and like us:
Pin Share