Badala ya kuendesha shule za kulea watoto kinyemela huko mitaani, makala hii itakueleza namna ambavyo unaweza kusajili, hivyo ukaendesha shughuli hii kihalali.
Ifahamike kuwa ni kosa la jinai kuendesha kituo au shule ya kulea watoto bila usajili. Kanuni ya 4(1) ya Kanuni za Vituo vya Kulea Watoto Wadogo Mchana na Watoto Wachanga za Mwaka 2012, zinasema kuwa mtu hataendesha kituo cha kulea watoto wadogo isipokuwa kama anamiliki cheti halali cha usajili.
Kwahiyo epuka kuingia katika kosa hili kwa kusajili kituo chako, makala itakuwa ikitafsiri Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, pamoja na Kanuni za Vituo vya Kulea Watoto Wadogo Mchana na Watoto Wachanga za Mwaka 2012.
Sifa zinazohitajika kabla ya kuomba usajili
1. Eneo ambapo kituo kitajengwa litatakiwa kukaguliwa na ofisa afya wa eneo husika na kutoa ripoti ya kuridhisha kuwa panafaa kwa ajili ya kulelea watoto. Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 4(3).
2. Kama eneo/jengo ambapo utaendeshea kituo ni la kupanga, basi hakikisha una mkataba wa pango ambao hauko chini ya miaka mitatu. Kanuni ya 4(4).
3. Utatakiwa kuthibitisha uwezo wa kifedha kuwa unaweza kuendesha kituo.
4. Hakikisha eneo lina vifaa vya kutosha kwa ajili ya michezo ya watoto. Hii ni kutoka Kifungu cha 47(1)( c ).
5. Muombaji/waombaji wawe na akili timamu.
6. Uthibitisho kuwa baada ya kupewa cheti cha kuendesha kituo hautatoa, kuuza, kukodisha kituo au cheti chako kwa mtu mwingine yeyote.
Baada ya hayo sasa waweza kuomba usajili kwa utaratibu huu
1. Jaza fomu ya maombi iitwayo D.C.C No. 1 kwa mujibu wa kanuni za Vituo vya Kulea Watoto Wadogo Mchana na Watoto Wachanga za Mwaka 2012.
Fomu hii unaweza kuikopi au kuipakua kutoka kwenye hizi kanuni au ukaenda kuiomba ustawi wa jamii. Ukishaipata utaijaza kama inavyojielekeza.
2. Baada ya kujaza hiyo fomu ya maombi, sasa utaiwasilisha kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii kwa mujibu wa Kifungu cha 47(1) cha Sheria ya Mtoto.
3. Baada ya kupokea maombi yako kamishna ataweka utaratibu wa kukagua eneo husika.
4. Baada ya kuridhika na ukaguzi, basi kamishna atatoa cheti cha usajili kwa mujibu wa Kifungu cha 147(6) cha Sheria ya Mtoto.
Namna hiyo utakuwa umesajili kituo.