Mtu aliye chini ya umri wa miaka 18 ni mtoto. Kisheria si kosa kumwajiri mtoto. Nataka tuelewane vizuri katika hili. Tunatakiwa kuifahamu sheria.

Wengi wanadhani ni kosa kumwajiri mtoto. Wanaposikia kampeni za ajira kwa watoto wanadhani ni kosa na haramu kabisa  kumwajiri mtoto.

Ndiyo maana nikasema inabidi tuelewane na tuijue sheria ili siku nyingine tunaposikia kampeni hizi tujue zinamaanisha nini.

1. Je, ni kosa kumwajiri mtoto?

Kifungu cha 77(1) cha Sheria Namba 21, Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 kinasema mtoto ana haki ya kufanya kazi. Kifungu kidogo cha (2) kimetafsiri neno kazi kumaanisha ajira. Kwa hiyo haraka tunaona kuwa mtoto anayo haki ya kuajiriwa. Ndicho tunachosema kuwa si kosa kumwajiri mtoto.

2.  Mambo ya kuzingatia unapomwajiri mtoto

Kwa kuwa ajira kwa mtoto imeruhusiwa, basi sheria imeweka mipaka au mambo ya kuzingatia unapoamua kumwajiri mtoto. Sehemu ya VII vifungu vya 78-85 vya sheria ya mtoto vimeeleza kuwa kazi yoyote/ajira anayopewa mtoto isiwe  hatarishi, ya unyayasaji, unyonyaji, ubaguzi au yenye kumsababishia mtoto madhara yoyote ya kimwili au kiakili.   Kazi au ajira itahesabika kuwa hatarishi, ya unyanyasaji, unyonyaji, ubaguzi au yenye kumsababishia mtoto madhara ya kimwili au kiakili ikiwa: –

Itamzuia mtoto kwenda shule. Kwa namna yoyote ajira ikimzuia, ikikiuka au kuingilia haki ya elimu kwa mtoto, ajira  hiyo inakuwa haramu na kosa kwa mwajiri.

( ii ) Ikiwa ajira hiyo ina madhara yoyote kwa afya ya mtoto, basi inakuwa haramu na isiyo ruhusiwa kwa mtoto.

( iii ) Ikiwa ajira/kazi hiyo anaifanya zaidi ya saa sita, inakuwa kosa. Kama mtoto ataajiriwa hapaswi kufanya kazi zaidi ya saa sita. Zikizidi mwajiri ameingia katika makosa.

( iv ) Ikiwa mtoto aliyeajiriwa yuko chini ya umri wa miaka 14 linakuwa kosa. Kisheria mtu anahesabika ni mtoto pale anapokuwa chini ya umri wa miaka 18.  Kwa suala la ajira, mtoto anayeruhusiwa kuajiriwa ambaye tunamwongelea katika makala hii yote, ni yule wa miaka 17, 16, 15, na 14 basi. Miaka 13, 12, na kushuka hairuhusiwi katu kumuajiri. Inaposemwa haki ya ajira kwa mtoto inazungumziwa miaka 17, 16, 15 na 14 tu.

(v) Ikiwa mtoto anafanya kazi mpaka saa mbili za usiku, litakuwa ni kosa. Muda wa mwisho wa sheria ni saa 1:59 jioni. Kuanzia saa mbili kamili usiku hadi saa 12 kamili asubuhi humo kote katikati mtoto haruhusiwi kufanya kazi.

(vi)Ikiwa halipwi ujira/mshahara unaolingana na kazi anayofanya ni kosa. Ujira/mshahara unaweza kuwa mkubwa kuliko kazi anayoifanya, au ukalingana na kazi anayoifanya, lakini usiwe mdogo kuliko kazi anayoifanya.

(vii ) Ikiwa anafanya kazi/ajira  ambayo kwa muonekano au mazingira yake  kuna viashira vya ngono. Hilo nalo litakuwa ni kosa kubwa.

(viii) Pia ikiwa ni kazi za baharini, ziwani, mitoni, kazi za migodini, viwandani, kumbi za starehe na baa, kadhalika zile za kubeba vitu vizito zimekatazwa kwa watoto. Isipokuwa kama mtoto anakwenda huko kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo au sababu za kimasomo.

Kwa ujumla  haya juu katika I –VIII yakitokea ndiyo yataitwa ajira hatarishi, za unyanyasaji na unyonyaji kwa mtoto.

3. Kwa nini imeruhusiwa mtoto kuajiriwa?

Ni kwa sababu tunahitaji kukuza vipaji na vipawa vya watoto. Duniani kote wanaofanya maajabu huanza wakiwa watoto na baadaye wakiwa watoto hivyo hivyo huchukuliwa na kampuni kubwa kukuza na kuendeleza vipawa vyao.

Iko hivyo kwenye michezo, kwenye  teknolojia na tasnia nyingine pia, kama hawa wangeachwa kwa kubanwa na sheria hadi wafikishe miaka 18 hakuna shaka mbeleni ingetengenezwa jamii butu na dhaifu mno.

Mtaona hata zile timu zetu za chini ya miaka 18 nk, zote hizo ni ajira kwa watoto.