Na Bashir Yakub

Tunazo aina kuu mbili za ardhi. Ardhi iliyosajiliwa na ambayo haikusajiliwa. Yote maana yake ni viwanja, nyumba na au mashamba.

Ardhi iliyosajiliwa ni ile iliyopimwa au maarufu kama ardhi yenye hatimiliki, wakati ambayo haikusajiliwa ni kinyume cha hiyo.

Marejeo yetu ni Sheria ya Ardhi, Sura ya 113 na Kanuni zake za Mwaka 2001, Sheria ya Mikataba Sura ya 345 na Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sura ya 334.

Utaratibu wa kununua ardhi iliyosajiliwa


1. Mjue anayekuuzia. Na si lazima kumjua sana. Kumjua tu kuwa ni fulani kunatosha, au kama unaweza kwenda mbali zaidi katika kumjua si vibaya.

  1. 2. Ukishamjua muulize kuhusu umiliki wake, alipataje eneo hilo (kwa kununua, urithi, zawadi), muulize ikiwa kuna mgogoro wowote, kama ameweka rehani popote, ana mke/mume, mara ya mwisho kulipia kodi ikiwezekana akuonyeshe risiti. Muulize kuhusu historia ya jiografia ya eneo hilo (mafuriko, vimbunga), na kingine chochote unachohisi ni muhimu kukijua.

Hapa wengi hawasemi ukweli, na kimsingi hatutegemei ukweli ila ukweli tunautegemea hapa chini.

  1. 3. Baada ya majadiliano sasa ni wakati wa kumuomba akupe kivuli (kopi) cha hati uipeleke Ardhi kujiridhisha na hayo uliyomuuliza hapo juu.

Huko Ardhi utajiridhisha kusu uhalisia wa jina la mmiliki, utajua kama ardhi imewekwa rehani ya mkopo, ikiwa ina zuio la mahakama, zuio la mtu mwingine mwenye masilahi kama mke/mume, ikiwa maeneo hayo watu watalipwa au walishalipwa fidia kupisha mradi fulani, ikiwa kuna mgogoro au jambo jingine lolote lisilo sawa.

  1. 4. Baada ya mambo kuwa sawa, sasa ni wakati wa kujiridhisha juu ya uhalisia wa hatimiliki. Wakati mwingine taarifa zilizo kwenye hati zaweza kuwa sahihi, ila hati yenyewe ikawa si halisi. Hivyo kuna ulazima wa kujua uhalisi wa hati.

Kwakuwa si rahisi muuzaji kukupatia hati yake halisi uende nayo kujiridhisha, basi muombe muambatane hadi Ardhi akiwa nayo, ambako mtaionyesha kwa msajili wa hati atakayesema kama ni halisi au hapana.

  1. 5. Baada ya kuridhika na uhalisi wa hati, sasa mnaweza kuanza kujadili masharti ya mauziano. Bei mnatakiwa muwe mmeijadili kabla, kwa sababu si vema kufanya yote haya wakati hamjafikia muafaka wa bei. Hapa mtajadiliana masharti mengine.
  2. 6. Baada ya kuafikiana kwenye masharti ya mauziano, sasa ni wakati wa kuandika mikataba kwa mujibu wa kifungu cha 64(1) Sheria ya Ardhi, kusainishana na wakili kugonga mihuri.

Hapa hakikisha nyote – muuzaji na mnunuzi mnasaini mkataba wa mauziano. Hakikisha muuzaji anasaini fomu namba 29 na 30, na hakikisha nyote tena mnasaini fomu namba 35, Kanuni za Ardhi za Mwaka 2001.

Aidha, ikiwa muuzaji ni mwanandoa, hakikisha mwanandoa mwingine ambaye hajasaini kama muuzaji anaandaliwa na kusaini nyaraka ziitwazo ‘ridhaa ya mwanandoa’.

Na kama muuzaji ni msimamizi wa mirathi, hakikisha warithi wote wanasaini ‘ridhaa ya warithi’.

  1. 7. Baada ya kusaini mikataba, sasa ni wakati wa kulipana ambapo inashauriwa fedha zilipwe benki ili karatasi za muamala ziwe ushahidi wa kulipa, kifungu cha 10 Sheria ya Mikataba.

Mnaweza kuanza kusaini mikataba halafu mkaenda benki kuhamisha fedha huku mikataba ikiwa mikononi mwa wakili, au fedha ikaingizwa kwenye akaunti ya muuzaji halafu hapohapo benki bila kutoka nje mkasaini nyaraka za mauziano.

  1. 8. Baada ya hayo yote ununuzi halali, salama, na wa kisheria utakuwa umefanyika. Aidha, unashauriwa kumtumia wakili katika hatua zote hizi.