Na Mwandishi Maalum
Timu ya Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Quinnipiac chini Marekani wakiambata na Maprofesa wao, wamewasili nchini kupata uzoefu na elimu juu ya uhifadhi na namna tafiti zinavyosaidia uhifadhi wa Maliasili. Ziara yao itaambatana na kutembelea hifadhi za Taifa Tarangire na Serengeti pamoja na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
Kabla ya kutembelea hifadhi hizo Wanafunzi hao watatembelea Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kujifunza jitihada za Serikali katika kuhifadhi Maliasili ya Wanyamapori kwa kutumia taarifa za kisayansi na mchango wa taarifa hizo katika uhifadhi na utalii.
Aidha, ujio huu wa wanafunzi kutoka Marekani ni muendelezo wa ushirikiano kati ya TAWIRI na Kampuni ya The Singing Grass ambayo inaratibu safari ya mafunzo hayo.