Dhana kwamba wanasiasa wanapaswa kuwa watu maskini huenda imepitwa na wakati. Rais wa Marekani, Barack Obama yeye na familia yake wanamiliki utajiri wa dola 19,225,070 sawa na Sh 31,529,114,800.

Obama kama Obama, utajiri wake ni dola 12.2 sawa na Sh bilioni 20, ikiwa utapiga hesabu za kubadilisha fedha kwa viwango vya dola moja sawa na Sh 1640 za sasa.

 

Rais huyu wa 44 wa Marekani ambaye alikuwa Seneta wa Jimbo la Illinois, ukwasi wake unatokana na mshahara na mauzo ya vitabu anavyoandika.

 

Kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani, alitumikia vipindi vitatu kama Seneta wa Jimbo la Illinois, lakini sasa ameweka historia ya kuwa Mmarekani mwenye asili ya Afrika kuwa Rais wa taifa hilo lenye uchumi mkubwa kuliko taifa lolote duniani.

 

Vitabu viwili; The Audacity of Hope and Dreams of my Father, ndivyo vimempatia ukwasi mkubwa Rais Obama. Kitabu cha “Dreams from My Father: A Story of Race and Inheritance” alikiandika mwaka 1995.

 

Hadi mwaka 2005 pato la Obama liliongezeka kutoka wastani wa dola 200,000 (Sh milioni 328) na kufikia dola milioni 1.7 (Sh bilioni 2.8).

 

Mwaka 2006 alitangaza kuwa amepata 916,000 (Sh bilioni 1.5). Kitabu cha “Audacity of Hope” alichokiandika mwaka 2006, kilipata mauzo ya kutisha na kuongeza utajiri wake hadi kufikia dola 4.2 (Sh bilioni 6.9).

 

Vitabu hivi vinampatia wastani wa dola 3.75 kwa kitabu chenye jalada gumu na kiasi cha dola 1.12 kwa kitabu chenye jalada la karatasi.

 

Historia ya mapato ya familia ya Obama na jinsi pato lao lilivyokua ni kama ifuatavyo kwa kuandika mwaka na kiasi cha fedha walizokuwa wanamiliki kama familia:-

 

Mwaka 2000 dola 240,000 (Sh milioni 393.6), Mwaka 2001 dola 272,759 (Sh milioni 447.3), Mwaka 2002 dola 259,394 (Sh milioni 425.4), Mwaka 2003 dola 238,327 (Sh milioni 390.8), Mwaka 2004 dola 207,647 (Sh milioni 340.5) na Mwaka 2005 dola 1,655,106 (Sh bilioni 2.7).

 

Mwaka 2006 dola 983,826 (Sh bilioni 1.6), Mwaka  2007 dola  4,139,965 (Sh bilioni 6.8), Mwaka 2008 dola 2,656,902 (Sh bilioni 4.4), Mwaka 2009 dola 5,505,409 (Sh bilioni 9.0), Mwaka 2010 dola 1,728,096 (Sh bilioni 2.8), Mwaka 2011 dola789,674 (Sh bilioni 1.3) na Mwaka 2012 dola 662,076 (Sh bilioni 1.1). Jumla Kuu ya fedha hizo zote ni dola 19,225,070 (Sh bilioni 31.5).

 

Ukiacha mauzo ya vitabu, Rais Obama anapta mshahara wa dola 400,000 kwa mwaka sawa na Sh milioni 656. Pia anarusiwa kama Rais wa Marekani kutumia fungu la dola 150,000 sawa na Sh milioni 246 kwa matumizi binafsi.

 

Rais huyu wa Marekani pia ametengewa fungu la wastani wa dola 100,000 sawa na Sh milioni 164, ambazo anaweza kuzitumia bila kutakiwa kulipa kodi. Kwa maana kwamba hahitaji kuzitolea maelezo popote kwenye vitabu vya serikali kuwa amezitumiaje.

 

Si hayo tu, Rais Obama ametengewa dola 20,000 sawa na Sh milioni 32.8 kwa mwaka kwa ajili ya matumizi ya ukarimu pale anapotembelewa na wageni.

 

Utajiri wake unaongezeka mwaka hadi mwaka, na inakisiwa kuwa utajiri ulioorodheshwa ni chini ya utajiri halisi wa Obama hasa baada ya kuwa amepata zawadi ya Nobel iliyompatia mabilioni ya fedha alizoamua kugawa sehemu ya pato hilo kwa watu maskini.