Nani wanafadhili mgogoro huu? Nani wananufaika kwa mgogoro huu? Nani anayesema kweli? Haya ni mambo ambayo nitayajadili kwenye mfululizo wa makala haya ambayo naamini yataendelea kutoka kwa wiki kadhaa. Soama sasa.
Loliondo ni makao makuu ya wilaya na kati ya tarafa tatu zinazounda Wilaya ya Ngorongoro, Mkoa wa Arusha, kaskazini mwa Tanzania.
Kihistoria, Loliondo ni jina lililotokana na kuwapo kwa miti mingi aina ya “loliondo” kwa jina la kitaalamu ‘Olea capensis subsp, O.welwitschii’ katika moja ya msitu wa hifadhi wa Serikali, Kusini mwa mji wa Loliondo.
Watanzania wengi wanaijua Loliondo kutokana na migogoro mingi ya ardhi na sifa ya “Babu wa Kikombe”, Mchungaji Ambikile Mwasapila. Wazungu wao wanaijua Loliondo kutokana na utajiri mkubwa wa rasilimali za wanyamapori, bioanuai [biodiversity] na ecosystem yake ya asili hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa watalii, uwindaji na sehemu muhimu ya uwekezaji vitega uchumi vya utalii na upigaji picha.
Wenyeji tunaifahamu Loliondo kama eneo lililo nyuma kimaendeleo, linaloongozwa na asasi za kiraia, lenye siasa za kifalme na ubaguzi uliokithiri wa kikabila.
Tarafa ya Loliondo inakadiriwa kuwa na watu 65,000 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Mgogoro wa sasa ni moja kati ya migogoro mitatu ya ardhi inayotajwa na wananchi wilayani hapa, baada ya mmoja wenye umri mkubwa kuliko yote nchini kusuluhishwa hivi karibuni na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Mwingine ni madai ya wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro kuruhusiwa kulima kilimo cha kujikimu ndani ya Mamlaka ya Ngorogoro [NCAA] pamoja na kuwa moja ya maajabu saba ya Afrika na dunia.
Pengine, mawazo haya hayatapokewa vyema na baadhi ya watu, lakini nia ya makala haya ni kuwaelimisha Watanzania juu ya upotoshwaji wa makusudi unaofanywa na kikundi cha watu wachache wanaonufaika na rasilimali zetu kwa mgongo wa kuwatetea wana-Loliondo, kumbe yanayotetewa ni maslahi ya wawekezaji wa Kizungu.
Abadan, huwezi kwenda Loliondo leo, ukaondoka kesho ukaujua vema ukweli na undani wa mgogoro wa Pori Tengefu Loliondo kwa sababu za mfumo wa maisha ya wananchi kuwa wa kifalme, hivyo kabla mtu, taasisi au chombo chochote hakijajadili mgogoro huu hapana budi kwanza waweke kambi katika vijiji vya Loliondo.
Tuweke kando ukabila, ukanda, siasa, jazba, vitisho, woga, ushabiki na maslahi binafsi au ya kundi fulani na kutanguliza kwanza mbele maslahi mapana ya Taifa ili kujua kilicho nyuma ya biashara ya Loliondo hadi watu kutoana kafara.
Mgogoro huu ulianza mwaka 1993, lakini ni sinema mithili ya volkano hai ambayo kwa miezi ya hivi karibuni imelipuka tena na kushika kasi mithili ya moto wa nyika kwenye vyombo mbalimbali vya habari vya ndani, nje [CNN, BBC, VoA, Al-Jazeera, Reuters] na kwenye mitandao ya kijamii baada ya Serikali kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kutangaza nia ya Serikali ya kumega sehemu ya ardhi yake na kuvimilikisha kisheria vijiji vinavyozunguka eneo la LGCA, kilometa za mraba 2,500 ili wananchi waanzishe Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori, yaani Wildlife Management Area [WMA] na Serikali kuendelea kumiliki kilometa za mraba 1,500 kati ya kilometa za mraba 4,000 za awali katika pori hilo.
Binafsi, sipendi kuwa mtu wa ndimi mbili, lakini baada ya Rais kumteua na kumwapisha Balozi Kagasheki kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, amejitahidi kadri ya uwezo wake kushirikiana na wadau wengine kuisafisha Wizara hii iliyogubikwa na kashfa za kila aina hadi Mkurungenzi wa Idara ya Wanyamapori na mtangulizi wa Waziri Kagasheki, wakaondolewa kwa kashfa ya kusafirisha nje ya nchi shehena kubwa ya wanyamapori hai kinyume cha sheria.
Amesimamia vema sekta na idara zilizo chini ya wizara yake, ameondoa migogoro ya kimaslahi katika Kamati ya Ushauri ya Ugawaji Vitalu vya Uwindaji, amedhibiti rushwa kwenye vitalu vya uwindaji, amejitahidi kudhibiti ujangili kwenye mbuga za wanyamapori, amedhibiti uharibifu wa mazingira, ameongeza na kudhibiti mapato yatokanayo na utalii, ameimarisha mbinu za kutangaza vivutio vyetu hadi kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania, amesuluhisha migogoro mingi kati ya wananchi na Wizara yake sehemu mbalimbali nchini, na sasa ameamua kwa dhati kabisa kumaliza mgogoro wa Loliondo.
Mkazi yeyote wa Loliondo anajua vema kuwa eneo la Pori Tengefu Loliondo linamilikiwa kihalali na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mujibu wa Tangazo la Serikali namba 269 la mwaka 1974 kwa nia ya uhifadhi wa wanyamapori na si vijiji kama inavyopotoshwa. Sasa vijiji vilivyoanzishwa miaka ya 1990 ni wapi na wapi na Tangazo la mwaka 1974?
Kauli ya Serikali
Kabla ya Balozi Kagasheki kutangaza nia ya Serikali ya kupitia upya eneo hilo, alifika Loliondo zaidi ya mara nne kwa vipindi tofauti kwa nia ya kushughulikia mgogoro alioukuta ukifukuta na kutoa moshi kwenye Wizara yake kwa kuwashirikisha kwenye mazungumzo waheshimiwa madiwani, wanasiasa, Serikali ya wilaya, watendaji wa Serikali, viongozi wa dini, mila [malegwanan] baada ya mapendekezo ya utafiti kadhaa uliofanywa na wataalamu kushauri kwamba kuna haja ya wananchi kunufaishwa na rasilimali zao kiuchumi.
Yaliyojiri kwenye majadiliano hayo ni lugha za dharau, ujeuri, kiburi, hasira na mara nyingine kususia vikao kutoka kwa walea migogoro, badala ya majadiliano kama ilivyokuwa azma ya Serikali.
Binafsi nampongeza Balozi Kagasheki kwa kuthubutu kumaliza mgogoro huu badala ya kumlaumu na kumpinga, kwani anayoyafanya ni kwa faida yetu sote na wote wanaompinga hawana nia ya dhati ya kumaliza mgogoro huu kwani ukiisha watakosa dili.
Waungwana wanasema kama hujafanya utafiti huna haja ya kuzungumza. Baada ya Serikali kuchunguza, kupokea, kuchambua na kuweka mkakati wa kutekeleza mapendekezo ya utafiti uliofanywa na watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania [TAWIRI], tume kadhaa zilizoundwa hasa Kamati Ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira mwaka 2009 iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Job Ndugai, Tume ya Waziri Mkuu ya mwaka 2010 iliyoshirikisha wizara 10 kwa mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo kati ya Orttelo Business Limited (OBC), NGOs, kampuni za uwindaji za Kizungu na wananchi.
Moja ya mapendekezo yake ni kupunguza ukubwa wa eneo la Pori Tengefu na kuvimilikisha vijiji vya Tarafa ya Loliondo vya Soitsambu, Ololosokwan, Arash, Loosoito, Olpilal na Orerian Magaiduru; bila kuathiri vyanzo vya maji, mazalia ya wanyamapori na mapito yao [ushoroba]. Hiyo ililenga kuhakikisha wanaendelea na mzunguko wao wa asili katika sehemu za Hifadhi ya Taifa Serengeti [SENAPA], Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro [Ngorongoro Conservation Area Authority -NCAA], Maasai-Mara na sehemu nyingine.
Baada ya kufuata hatua zote za kisheria kwa nia ya kutatua mgogoro huo na ili wananchi tuishi kwa amani na kufurahia matunda ya uwekezaji, Waziri wa Maliasili na Utalii kwa mamlaka aliyopewa na Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, aliamua kufanyia maboresho Pori Tengefu Loliondo kwa lengo la kuleta manufaa kwa hifadhi zenyewe, wananchi na Taifa kwa ujumla.
Hivyo Machi 21, 2013 alitangaza kwenye vyombo vya habari azma ya Serikali ya kupunguza eneo la Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,000 na kuvimilikisha vijiji kilometa za mraba 2,500; na Serikali kuendelea kumiliki kilometa za mraba 1,500 zilizosalia.
Waziri alisema kwa miaka ya karibuni idadi ya watu imeongezeka na mahitaji ya ardhi nayo yameongezeka kwa kasi, hivyo Serikali imeona umuhimu wa kutekeleza jukumu lake la msingi kwa kutoa ardhi hiyo kwa wananchi na ili kulinda ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti, Pori Tengefu la Loliondo na Mamlaka ya Ngorongoro, Serikali itaendelea kumiliki kilometa za mraba 1,500 na kuisimamia kwa mujibu wa sheria za usimamizi wa wanyamapori na kuendelea kuwa na hadhi kama ya awali ya Pori Tengefu kwa ajili ya kulinda mazalia ya wanyama, mapito ya wanyamapori na vyanzo vya maji katika mto Pololeti, chemchem za Ololosokwan [sero], Olasae na nyingine kwa ajili ya ustawi wa hifadhi, manufaa ya wananchi, utafiti wa kisayansi, mafunzo na kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Ardhi itakayobaki itasimamiwa na vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya Mwaka 1999, tena vijiji vitawezeshwa na Serikali kuanzisha WMA katika ardhi waliyopewa ili kujiongezea kipato na kupunguza umaskini, Serikali itapeleka huduma muhimu za jamii na mifugo kama shule, zahanati, majosho, malambo na minada ili wananchi wafuge kisasa zaidi badala ya kuchunga na mengine mengi.
Hakika hizi ni habari njema, hivyo wanaosema Serikali imechukua ardhi ya vijiji si za kweli, bali Serikali ndiyo imetoa ardhi kwa vijiji nilivyovitaja hapo juu. Ukweli huu wananchi tunaujua, madiwani wetu wanaujua, NGOs zinaujua, lakini kwa sababu ya maslahi binafsi baadhi ya madiwani wetu wameamua kutumiwa kusema uongo ili kutimiza malengo yao ya kisiasa na kiuchumi.
Itaendelea