Ndiyo kusema licha ya fursa kubwa kielimu walizopata watu wa mwambao siku zile kuelimisha watoto wao, jamaa hawa Waswahili hawakuzitumia.

Hapo ndipo zinapoonekana sababu za kuwafanya Waislamu wasitumie kikamilifu fursa zilizotolewa na Serikali kwa elimu ya raia wote wa Tanzania. Waswahilii hawakuamini ile nia nzuri ya Serikali kwa watoto wa mwambao.

 

Aidha, kwa vile shule za Misheni ziliendeshwa na Wazungu na hizo shule za Serikali zilifunguliwa na Wazungu na kufundishwa na Wazungu, basi Waswahili wa mwambao waliogopa zisije zikawaghilibu watoto wao wakaacha utamaduni wa Kiislamu waliouzoea, na wakakumbatia utamaduni mpya wa Kizungu ambao kwa maoni na fikra zao ulikuwa unawaongoa kuwa Wakristu.


Basi, tofauti za kiimani kati ya Ukristu na Uislamu ziliwafanya wazee wetu pale zamani kuwa wazito kupokea elimu kutoka kwa wazungu. Pili, hofu ya kuwa watoto wataongolewa na kuwa Wakristu, iliwazuia Waislamu kupokea mara moja hii elimu ya kawaida kutoka kwa Wazungu. Mimi naita hofu au woga wa namna hii uwe ni wa kweli au wa kufikirika tu (real or imaginary only) kisaikolojia iliwadumaza wengi katika maeno ya mwambao.

 

Maeneo namna hii ni kule Pangani, Bagamoyo, Dar es Salaam, Uzaramoni kote, Undengerekoni kule Rufiji, Umatumbini kule Kilwa, hata kwa Wamaraba wa Mikindani na Lindi – sehemu zile zote Uislamu ulikoshamiri ambako Waarabu walieneza hofu ile ya Ukristo hata maeneo ya Mrima au kama Tabora, Kigoma-Ujiji, Kondoa Irangi hadi Tunduru ambako hali namna hiyo ya kudumaa kielimu inaonekana.

 

Kihistoria basi, tofauti katika elimu kwa watoto wa Tanzania (disparity in education) ilianzishwa na wale wageni waliotuletea elimu hii ya kawaida ya darasani. Tofauti zao za kidini sisi wananchi zimetuathiri kifikra. Lakini sasa tuna miaka 51 ya Uhuru wetu kweli bado tunalishabikia hili tatizo la tofauti za kiimani? (Still entertain such fallacy?)

 

Wizara yote ya Elimu inaendeshwa na vijana wasiojua hata hali hiyo ya tofauti zilizokuwapo enzi zile za ukoloni.


Kinachonishangaza mimi leo hii ni wazo lile la kuwa Mzungu aliyeunda Idara ya Elimu hapa Tanganyika mwaka 1920 alitokea nchi ya Misri kule Cairo, alikokuwa Afisa Mkuu wa Elimu. Misri ni nchi ya Kiislamu. Na imeendelea sana katika elimu.


Akaja Zanzibar mwaka 1907 kuanzisha Idara ya Elimu, kutoka kule ndipo akaja Tanganyika. Huyu anaitwa Bwana Stanley River Smith. Vipi hakuweza kusahihisha hii tofauti (disparity) kati ya watoto Waislamu na Wakristu na kuweka mfumo sawa wa elimu kwa wote?


Pili, enzi zile za utawala wa Mwingereza hitilafu hii ilikuwapo. Kwanini wananchi hawakuipigia kelele hadi wakati tunadai Uhuru ndipo tatizo hili likaanza kuibuliwa kwa kupwelea kugawana madaraka baada ya Uhuru? Napo ndipo pa kujiuliza hasa NANI ALAUMIWE – Serikali ya mkoloni au Serikali yetu wananchi?

 

Tofauti katika elimu zimeibuka kati ya watu wa imani mbalimbali baina ya Wakristu na Waislamu, pia tofauti katika elimu zimeibuka kati ya mikoa katika nchi yetu, tena kati ya makabila mbalimbali kama vile Wamaasai, Wagogo, Wayao, Wandengereko kwa kulinganishwa na makabila kama ya Wachagga, Wanyakyusa na Wahaya.


Hivyo basi, mara tu baada ya nchi yetu kuwa Jamhuri, Desemba 1962 Rais wa Kwanza wa Taifa letu na ambaye ndiye Baba wa Taifa, alitangaza wazi tatizo hili la tofauti ya elimu katika makundi ya wananchi na mikoa ya nchi hii.


Alisema kuwa kuna tofauti katika elimu kati ya Waislamu na Wakristu na kuwa hali namna hii tumeirithi kutoka kwa mkoloni. Basi, akatahadharisha kuwa kuna uwezekano wa kuzuka uadui miongoni mwetu juu ya hilo wakijatokea wakorofi wenye nia ya kutusambaratisha katika uhuru na umoja wetu hapa nchini (Nyerere: Uhuru na Umoja uk. 179).

 

Si hivyo tu, bali hata katika makabila na mikoa yetu zipo tofauti katika elimu. Aliendelea kusema yapo makabila yaliyoendelea kielimu na yapo yaliyodumaa kutokana na mfumo wa elimu enzi za kikoloni tuliorithi wakati wa Uhuru (Nyerere: Uhuru na Umoja uk. 181).

 

Akapendekeza namna ya kusawazisha hali hiyo na akawaomba wananchi wote watambue kwamba; Mosi, hali ya nchi tuliyorithi kutoka kwa wakoloni siyo sawa na hali ya nchi inayotarajiwa kujengwa na sisi wenyewe kwa manufaa ya vizazi vijavyo. Pili, jukumu letu kwa sasa ni kuuelewa upungufu au matatizo tuliyonayo baada ya Uhuru na kuelewa kwamba kwa sasa hakuna njia ya mkato kuyatatua na kuyamaliza kwa mara moja.

Alitoa mfano wa hili tatizo la dosari katika elimu na njia ya kulisawazisha ili kusiwepo na tofauti kielimu kati ya Waislamu na Wakristu au kati ya Wagogo kuwa kama Wachagga au Wamaasai kuwa kama Wahaya kielimu.

 

Tatu, alikumbusha wajibu wa kila mmoja wetu kuepuka kishawishi cha kulaumiana kwa hayo yaliyotokea wakati wa ukoloni, ambako hakuwapo hata mmoja wetu aliyehusika au aliyesababisha hali namna hiyo kutokea.


Hatimaye aliomba sote katika umoja wetu tushikamane tulijenge Taifa hili kwa namna tunavyotaka liwe ili tofauti zetu hizi zisiwepo na sote tuishi kwa usawa na kwa amani.

 

Ndipo akatoa mwito kwa maneno haya, nanukuu, “And to ALL OUR CITIZENS as a whole, I say this, my friends let every one of us put all he has into the work of building a Tanganyika in which there will be no more such distinctions and divisions (Nyerere: Uhuru na Umoja uk. 181).

Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).