Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Rufiji
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, amesisitiza umuhimu wa kuitunza na kuenzi amani, utulivu na upendo miongoni mwa Watanzania kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizindua bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Ikwiriri, Jimbo la Rufiji, Mkoani Pwani, lililogharimu kiasi cha Shilingi milioni 185.4, alitoa rai kwa wanafunzi waliofikisha miaka 18 na kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, pamoja na vijana, kuhakikisha wanatunza amani katika maeneo yao.

Vilevile, Ussi aliwataka Watanzania na wale wa Zanzibar waliojiandikisha kuhifadhi shahada zao za kupiga kura, ili ifikapo uchaguzi, kila mmoja aweze kutimiza haki yake ya msingi ya kupiga kura na kumchagua kiongozi atakayewafaa.
Kwa mujibu wa Ussi, Mwenge wa Uhuru ni tunu ya Taifa inayolenga kukagua thamani na maendeleo ya miradi inayotekelezwa.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuenzi, kutunza na kuheshimu Mbio za Mwenge wa Uhuru, kama ilivyokuwa falsafa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na waasisi wa Taifa letu.”
Aliwataka Watanzania ,kuendelea kuwa wazalendo kwa kuuenzi Mwenge wa Uhuru kwa maslahi ya vizazi vijavyo.

“Dkt. Samia Suluhu Hassan ameona kuwa ipo haja kwa wasaidizi wake kuendelea kufuata na kusimamia majukumu anayowapatia, na leo hii tumeona usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi huu wa bweni, Mimi pamoja na wenzangu watano tumeridhishwa na utekelezaji wa mradi huu,”
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohammed Mchengerwa, alieleza wizara hiyo itahakikisha ushiriki wa kila mmoja katika mbio za Mwenge, kila pale utakapotembelea sehemu mbalimbali za nchi, kwa kuwa zinahusisha maendeleo.
Alifafanua kuwa ,mwaka 2024, Rufiji ilikuwa Halmashauri ya Wilaya, lakini kutokana na hatua kubwa iliyopigwa kimaendeleo na kiuchumi katika sekta zote, na upandishwaji hadhi vijiji kuwa miji, Rufiji sasa sio Halmashauri ya Wilaya tena, ni Halmashauri ya Mji.

Mchengerwa alieleza, furaha yake kwa kasi kubwa ya maendeleo na utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kimkakati ambayo haijawahi kutokea tangu Rufiji ianzishwe.
“Matarajio yetu na ndoto yetu kwa sasa ni kumuomba Mheshimiwa Rais siku za usoni aweze kuridhia Rufiji kuwa Mkoa, kwani jiografia ya mkoa wa Pwani haipo rafiki, kwa sababu inabidi kupita Dar es Salaam au Morogoro ili kufika Kibaha,” alieleza Mchengerwa.
Mapema Aprili 5, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba, alipokea Mwenge wa Uhuru ukitokea Mkuranga, ambapo ukiwa Rufiji ulipitia miradi sita yenye thamani ya sh. Bilioni 1.614, ambayo imewekwa mawe ya msingi, kukaguliwa na kuzinduliwa.

Miradi hiyo ni pamoja na kuzindua bweni la wasichana Shule ya Sekondari Ikwiriri, litakalotatua changamoto ya upungufu wa mabweni; kukagua kikundi cha vijana cha ufyatuaji matofali; kuweka jiwe la msingi katika mradi wa barabara ya Mahakama; mradi wa maji Nyandakatundu; uhifadhi wa mazingira Shule ya Sekondari Bibi Titi Mohammed; na kukagua ukarabati wa miundombinu ya Hospitali ya Wilaya Rufiji (Utete).

