Baada ya kusema ameongea na Feisal Salumu na amemuelewa hivyo atabaki Yanga, hii leo Haji Manara amebandika bandiko la sheria zinazoweza kuibana klabu ambayo itamsajili Fei Toto kutokea Yanga bila kufuata utaratibu.
Nimejiuliza maswali kwamba ikiwa walielewana hiyo habari ya kuishitaki klabu itakayomsajili Fei Toto inatokea wapi? Fei Toto amemgeuka Manara baada ya makubaliano waliyoyafanya kwenye mazungumzo yao?
Kulikuwa kuna uharaka gani kwa Haji Manara kutangaza kuwa Fei Toto amekubali kubaki Yanga kabla ya makubaliano yote na klabu kukamilika? Manara alitaka kuwa the man behind the story ya Fei Toto kurejea Yanga au alitaka ‘kugain credibility’ kwa wanayanga na viongozi wake katika kuweka mambo sawa.
Kuna wakati Haji Manara akiwa Simba aliwahamasisha mashabiki kuweka ‘hashtag’ ya kumuomba Mohamed Hussein kubakia Simba na Kusaini mkataba mpya.
Wanachama waliitikia lakini nilihoji urahisi wa Manara kuhamasisha mashabiki kuandika hashtag kuliko ilivyo rahisi kwake kuwashawishi viongozi wa Simba kumuongezea mkataba Zimbwe Jr katika maslahi anayoyataka. Stori ile ile ya Manara wa Simba imejirudia kwa Manara wa Yanga.
Ikiwa Manara alisaidia Zimbwe Jr kusalia Simba haikuwa wajibu wake kama sehemu ya uongozi? Kwanini alitoka hadharani kuonesha yeye ndiye ametumia bidii za hashtag kumfanya Zimbwe Simba kama alivyorudia tena kuonesha kwamba ushawishi wake ndio utambakiza Fei Toto ndani ya klabu ya Yanga?