Na Hassan Aufi, JamhuriMedia

Mtazamo wa wataalamu wa Sosholojia (Sociologist) kuhusu tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani, unaonyesha kuwa hali hii inajitokeza kutokana na kukosekana uimara kwenye mifumo ya kimalezi ya familia zetu na kwa kiasi kikubwa katika mifumo ya malezi ya kijamii.

Haya ni matokeo ya kushindwa kwa taasisi ya familia na taasisi nyengine zinzosaidiana na familia katika kusimamia malezi kama vile dini, tamaduni (mila na desturi), uchumi n.k. Kwa kupitia nadharia ya utendaji wa kimuundo, haya pia ni matokeo ya kushindwa kwa sehemu fulani ya mfumo wa kijamii.

Serikali, Mashirika ya Kiraia (CSO’s), wataalamu wa masuala ya kijamii wanapaswa kueneza ufahamu kuhusu matatizo ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani duniani kote.

Kwa juhudi kubwa za Serikali, mashirika ya haki za binadamu, na watetezi wa haki za watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani, watoto wa mtaani wanaweza kuokolewa kutoka mtaani, kurekebishwa tabia na kuwaweka katika nyumba zenye upendo na familia zenye ulinzi (wazazi/walezi mbadala (yaani watu wakuaminika, ndugu/jamaa n.k.

Sambamba na kuwatafutia nyumba salama, lengo pia ni kuwaelimisha, kuwapa msaada wa matibabu, huduma za kisaikolojia na kijamii (PSS) na kuwafunza ujuzi wa maisha bora (Kurejesha matumaini na kubadilisha maisha yao).

Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani ni watoto kama watoto wengine katika jamii. Ni watoto wetu wanaohitaji kuangaliwa kwa makini na kusaidiwa maana ni kweli mtaani sio salama kwa maisha na maendeleo yao ya baadae.

Mkurugenzi Mtendaji wa Akili Platform Tanzania Roghat F Robert , akigawa mbegu kwa vijana

Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani nchini Tanzania ni watoto wanaohamasika na wanaohamahama kwa sababu mahitaji yao na hali zao hubadilika mara kwa mara kutokana na athari mbalimbali za ndani na nje ya nchi yetu.

Ingawa jitihada kubwa zinafanyika katika kila kona ya nchi yetu ikiwemo serikali, mashirika ya haki za binadamu, asasi za kiraia na wengineo, lakini tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani bado ni kitendawili.

Juhudi kubwa zinafanyika katika kupunguza tatizo hili lakini kwa kiasi kikubwa bado hazijaleta matokeo tarajiwa ya kulimaliza kabisa suala hili, swali la kujiuliza tunapozungumzia changamoto ya ongezeko au uwepo wa watoto wa mitaani, Ni mkakati au mbinu gani za kitaalamu zinazofanyika kupunguza tatizo hili?

Bila shaka kuna hitajio kubwa la kufanyika tafiti nyingi zitakazo akisi ukubwa wa tatizo na njia sahihi ya kulitatua tatizo hili. Hakika ukifuatilia kwa ukaribu zaidi, wadau wengi wanaofanya kazi na watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani wana mbinu zinazofanana katika kutatua changamoto hii ambayo kila uchao bado linaongezeka zaidi kutokana na changamoto na matatizo ya kijamii ambayo kila siku yanakuja na sura mpya tofauti na ile ya mwanzo. Hitajio la kufanyika tafiti za mara kwa mara ili kupata ufumbuzi sahihi wa taizo hili ni muhimu kuliko tunavyofikiria. 

Sababu zilizopelekea watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani kwa miaka ya 1990’s haziwezi kuwa sawa na za nyakati hizi za sasa. Kwa hakika ongezeko la matatizo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yamepelekea kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa sababu mpya za kuongezeka wimbi la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.

Hivyo basi ni jukumu la serikali na wadau wote wanaofanya kazi kwa karibu na watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani kuja na wazo la kufanya tafiti za msingi kwenye eneo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani ili tuweze kupata majibu sahihi na kutafuta njia sahihi ya kuliondoa kabisa tatizo hili.

Uongozi wa Shirika la Akili Platform Tanzania ukisalimiana na mkuu wa chuo kabala ya mafunzo ya ujuzi jengefu kwa wanachuo cha TTC juu ya ujuzi wa kijana.

Watoto wengi huondoka nyumbani kwa sababu ya vifo vya wazazi wao na unyanyasaji dhidi yao ikiwemo kimwili, kingono, kisaikolojia, kiafya na kutelekezwa. Wazazi wanapofariki, baadhi ya watoto hukumbana na chuki na kushindwa kupata usaidizi wa kimsingi na matunzo kutoka kwa jamaa zao, hivyo hukimbilia mitaani. Wengine hukimbia makwao kutokana na umasikini, kwa dhana kwamba watapata fursa za kiuchumi mitaani kwa kuuza mifuko/vifungashio, kuomba omba na kuiba.

Baadhi ya watoto pia wanakataliwa na familia zao, kwa sababu kama vile ulemavu na magonjwa au wanalazimishwa kufanya uhalifu. Wananyonywa na kunyanyaswa ili wapate chakula. Haijalishi wakiwa wapi, watoto wa mitaani mara nyingi wananyimwa elimu, huduma za afya na haki nyingine za msingi za kibinadamu

Kulingana na Shirika la Consortium for Street Children, mtandao wa kimataifa wa mashirika zaidi ya 100 unafafanua kwamba “watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani ni watoto wanaotegemea mtaa kuishi na kufanya kazi na wale ambao wana uzoefu mkubwa kwenye maeneo ya umma kama vile masokoni, stendi za mabasi, maeneo ya kibiashara, maeneo ya kupumzika n.k.

Imegundulika kuwa watoto wanaoishi mtaani ndio waliotengwa zaidi na wanaokosa ulinzi zaidi ulimwenguni, wamewekwa kando, hawapendwi wala kuthaminiwa. Zaidi ya hayo, hali yao inafanywa kuwa ngumu zaidi kutokana na mitazamo duni ya kijamii ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani, kuna ubaguzi na kutokukubalika kwa watoto hawa ambao hufanywa mazingira yasiwe salama kwao. Pia, wananyanyaswa na kutumika kwa shughuli haramu, ambazo ni pamoja na uhalifu, wizi, utumikishwaji wa watoto n.k.

Watoto wa mtaani mara nyingi hulengwa na vikundi vya usalama, hupigwa, kushikiliwa na kufunguliwa mashtaka bila kufuata taratibu.

Serikali, sera zilizopo, taasisi na jamii huwatenga watoto wa mtaani na kuwanyima haki zao za kimsingi za kibinadamu. Maisha ya mtaani huwaweka watoto kwenye hatari nyingi na kuwanyima faraja na usalama wao. Timu ya Wataalamu (Wafanyikazi wa kijamii na wengine) inatakiwa kuhamasisha jamii juu ya hitajio la kukomesha ubaguzi ili kufanya ulimwengu kuwa salama na rafiki kwa kila mtoto anayeishi mtaani.

Watoto kama hao tayari wako katika hatari ambayo inaweza kuwafanya kuwa katika hatari zaidi ya vurugu, matumizi ya madawa ya kulevya na masuala ya afya ya akili. Ili kukabiliana na hali halisi ya maisha ya mtaani kama vile msongo wa mawazo, magonjwa, njaa, unyanyapaa na ubaguzi, baadhi ya watoto huamua kutumia dawa za kulevya (bangi, gundi, heroine, pombe) kama njia ya kuepuka maumivu ya kutafuta njia ya kuwa salama.

Matumizi ya madawa ya kulevya katika umri mdogo, wakati watoto bado wanakua kimwili na kiakili kunaweza kusababisha matatizo ya muda mrefu katika utu uzima wao. Hvyo basi tunapaswa “Kuwaweka Salama Watoto Wanaoishi na Kufanya kazi Mtaani”

Mkurugenzi Mtendaji wa Akili Platform Tanzania Roghat F Robert akifundisha

Wito kwa serikali, Mashirika ya Haki za Binadamu na Asasi za Kiraia (CSO’s) na wadau wengine wa utetezi, haki na ulinzi wa watoto na wanajamii kwa ujumla kuamka na kusimama kidete kutetea haki za watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani ili kuwaweka salama. Yafuatayo yanaweza kutekelezwa:

A: SERIKALI

  1. Serikali iache kutumia nguvu kwenye kuwaondoa watoto wa wanaoishi na kuafanya kazi mtaani na badala yake iwatumie wataalamu wake (Maafisa ustawi wa jamii) kutumia ujuzi wao wa namna bora ya kufanya kazi na kundi la watoto hawa.

Kushirikiana na wadau, mashirika na taasisi zinazofanya kazi na watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani kama vile SOS Children Village, Amani center for street children, Railway Children Africa, Baba Watoto na mengineyo katika kutatua changamoto zinazowakumba watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

  • Kuziimarisha nguvu za kiuchumi familia masikini na fukara kupitia mfuko wa TASAF ili kuweza kufanya shughuli na biashara ndogo ndogo ambazo zitaweza kuwaingizia kipato na kuweza kujikimu vizuri ili kupunguza wimbi la watoto wa mtaani ambao wapo mtaani kwa sababu ya umasikini.
  • Kuwatumia viongozi wa dini na wakitamaduni katika kutoa elimu ya kimalezi na kimaadili zenye lengo la kuwambusha wajibu wao katika uangalizi wa kimalezi kwa watoto wao.
  • Kuimarishwa kwa sheria na sera za ulinzi katika kuwalinda watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.Kama ilivyo Kwenye Muongozo ya Watoto Wengine Ambapo serikali imeanzisha baraza la Watoto Ili Kuwa Kama Chombo Cha Watoto kutolea Maoni Yao, pia Serikali Ione Haja ya kuanzisha jukwaa la Watoto (Street Connected Children Platform) Kuanzia ngazi ya Mtaa Hadi Taifa Ili Kuwa Chombo Chao Rasmi Cha Maoni. Kutumia Maoni ya Watoto na Mapendekezo Yao (Child Centered Approach) Huenda kukaleta manufaa ya kulipunguza Kwa Kasi tatizo Hili Kama Si kulimaliza kabisa.
  • Kufanya tafiti mara kwa mara katika kuakisi tatizo hili ili kuja na majibu sahihi ya matumizi ya mbinu ya kulitatua tatizo hili.

B: FAMILIA

  1. Kutengeneza misingi mizuri ya kimalezi kwa watoto wao ili kupunguza idadi ya watoto wanaoenda kuishi mtaani kwa sababu ya misingi mibovu ya kimalezi kutoka katika familia zao.
  2. Kuimarisha misingi mizuri ya upendo kwa wanafamilia/wanajamii katika kuishi na watoto walioachwa na ndugu zao baada ya kufariki au kupata maradhi ya kudumu juu ya kuwapa huduma stahiki.
  3. Familia zinapaswa kuwa sehemu salama kwa watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili.
  4. Kurejeshwa Kwa Mfumo wa kale wa Malezi Ambapo Mtoto anakuwa ni WA Jamii na anarekebishwa na Jamii Kwa kadiri inavyofaa. Mbinu Hii ilitumika kuimarisha Tabia na misingi Bora ya Malezi na makuzi ya Watoto na Kuwa na Kizazi Bora Kwenye Jamii.
  5. Familia zinapaswa kujiimarisha kiuchumi kwa kujiunga na vikundi vya kuweka na kukopa (VICOBA), kujiunga na mfuko wa serikali wa kusaidia kaya masikini TASAF, kujiunga kwenye vikundi vinavyonufaika na mikopo kutoka katika halmashauri ili kuweza kujinasua na janga la umasikini na ufukara uliopitiliza ili kuweza kumudu katika utoaji wa mahitaji ya msingi kwa watoto wao.

C: WADAU WA MAENDELO/MASHIRIKA YASIYO YAKISERIKALI

  1. Kushirikiana na serikali kuangalia namna bora ya kufanya kazi na watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.
  2. Kuanzisha miradi inayolenga katika kufanya kazi na watoto wanaoishi mitaani ili kuweza kuwasaidia wao na familia zao kiuchumi na kijamii ili kupunguza wimbi la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.
  3. Kutumia wataalamu wao katika kufanya kazi na watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani pamoja na familia zao ili kuweza kutoa elimu ya kitaalamu yenye malengo ya kupunguza wimbi la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani
  4. Kuzijengea uwezo na kuziimarisha familia kiuchumi ili ziweze kujikimu na kuwapatia watoto wao mahitaji ya msingi
  5. Kushirikiana na serikali katika kufanya tafiti zinazo akisi tatizo hili ili kuja na mbinu na afya sahihi ya kulitatua tatizo hili.

N.B: Tuungane pamoja katika kuhakikisha kwamba watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani wanalindwa, wanakuwa salama na kupewa haki zao za msingi kama watoto wengine. Tufahamu kuwa watoto wote ni sawa hivyo basi tutambue ya kwamba “Mtaa hauzai mtoto Tuwajibike

Hassan Aufi

Afisa Ustawi Jamii.

0764002024