George Benerd Shaw alipata kuandika haya: “Maendeleo hayawezekani bila mabadiliko ya fikra na wale ambao hawawezi kubadilika namna wanavyofikiri hawawezi kubadili chochote.” Kila kukicha mwanadamu anakabiliwa na zoezi la kufanya uchaguzi fulani.

Ulimwengu huu hauna nafasi kwa watu wanaopuuzia maarifa ya mhimu. Kila kukicha yeyote anaalikwa kuukaribisha utajiri na kuuaga umaskini au kuuaga utajiri na kuukaribisha umaskini. Methali ya Kichina yasema wazi kwamba: “Dunia ni ya wale ambao wanavuka madaraja mengi katika kufikia kwao kabla ya wengine kuona daraja hata moja.” Mantiki inatunong’oneza ukweli kwamba, fikra zilizotufikisha katika mazingira tuliyomo kwa sasa na hali tuliyonayo leo, fikra hizo kwa uhalisia wake hazitaweza kututoa kwenye matatizo tuliyonayo kwa sasa. Methali ya Kifaransa inatukumbusha kwamba: “ Anayengoja kuvaa viatu vya marehemu anaweza kutembea pekupeku kwa muda mrefu.’’  Kusubiri maendeleo yatokee pasipo kufanya kazi kwa bidii ni kwamba unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu. Kulalamika kwa kila jambo pasipo kubuni mbinu na mikakati ya kukuinua kiroho, kimaadili, kisiasa, kiafya na kiuchumi, ni kwamba unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu. Dhana ya kung’ang’ani imani za uchawi ni kusubiri viatu vya marehemu.

Mwandishi wa Kihispania, Anais Nin, anasema: Hatuoni vitu kama vilivyo, tunaviona kama tulivyo.” Huu ni wakati wa kuviona vitu vilivyo na si wakati wa kujiona tulivyo. Kila mtu sasa na ajihisi kama mvumbuzi, mtafiti na mtatuzi wa matatizo yanayoikabili jamii yetu.

Uhodari wa kuishi si uhodari wa kuishi miaka mingi, la hasha! Ni uhodari wa kuwa msaada katika jamii inayokuzunguka na ulimwengu kwa ujumla wake. Lakini yote katika yote tunahitaji kuandika upya historia mpya ya maisha yetu na taifa letu. Tuyatazame mazingira yetu tunayoishi kwa jicho la ushindi. Tuutazame huu ulimwengu kwa jicho la ushindi. Wahenga walipata kunena: “Penye nia pana njia.”  Hannibal [183-247] mgunduzi wa silaha za kivita anatushauri hivi: “Lazima tuone njia kama haipo tuitengeneze.” Ni wakati sasa wa kuitengeneza njia upya. Kwa sababu huko nyuma tumekuwa tukiishi kama wanyama. Hatuwezi kubadili kilichotokea, kwani ni historia tayari. Na sasa Tufungue macho yetu tuzione fursa zinazotuzunguka.

Tanzania inahitaji kipindi cha ufahamu. Hiki kipindi naweza kukipachikia jina la falsafa ya ufahamu (Philosophy of consciencism). Falsafa ya ufahamu ni falsafa ambayo inatoa mtazamo mzima juu ya ufahamu wa taifa letu lianzie wapi na liwezeje kujiendeleza kiuchumi, kisisa, kijamii na kiutamaduni. Mawazo ya Hegel yanasema: “Haitoshi tu kuufahamu ulimwengu ulivyo, bali ni kubuni mawazo yanayoweza kuuongoza ulimwengu.” Katika historia yote ya kuyatafakari mawazo ya mwanadamu na mifumo ya miundo yake, wanafikra adhimu karibu wote duniani wanakubaliana kuwa tendo la kuelewa hususan kufikiri huwezekana tu katika mfumo wa udhanishaji wa mawazo jumla (universal concepts). Waafrika na walimwengu kwa ujumla wanastaajabu mapinduzi makubwa ya kiuchumi ya taifa la China na wanajenga hoja kwamba tuwaige Wachina, lakini wanashindwa kufahamu kuwa kile tunachokiona kwa Wachina leo hii ni matokeo ya akili na uwezo wao wa kuyafikiri mambo kwa kina na kuyaumba kwa vitendo. Hegel anasema: “Mifumo yote ya kiuchumi na kijamii ni ujielezo wa ulimwengu wa akili wa jamii husika.” Naye Plato anasema: “Kile kionekanacho katika matukio ni kivuli cha ulimwengu wa fikra wa jamii husika.”

Ni hakika kwamba, ulimwengu tulionao uko huru kutokana na mategemeo na matarajio yetu. Hata hivyo ni pale tu ambapo tutautambua huo ulimwengu ndipo tutakapojitambua na sisi wenyewe. Kwa muktadha huo, tutambue tunajua nini, na nini hatujui, tunakosa nini na nini hatukosi, tunataka nini na nini hatutaki, njia ipi inafaa kupita na njia ipi haitufai kupita.

Falsafa inatufundisha kwamba, ukweli halisi hauko katika dunia ya vitu mwonekano. Vitu mwonekano ni vivuli vya vitu halisi na vitu halisi vinaishi katika dunia ya uwazo. Bila elimu bora ni ndoto kwa Watanzania kuishi kwenye dunia ya uwazo.

Kwa muda mrefu Watanzania tumekuwa mateka wa kifikra kwa sababu ya mfumo wetu mbovu wa elimu. Tujitahidi sana kukilea hiki kizazi chetu katika misingi ya kifalsafa ili kisiwe mateka wa fikra. Ninaomba kutamatisha makala yangu kwa kukubaliana na Libba Bray kwamba: “Hatuwezi kurudi nyuma. Tunaweza tu kwenda mbele.” Tanzania bila imani za uchawi inawezekana. Afrika bila dhana ya uchawi inawezekeza. Mungu ibariki Afrika watu wake wafikiri vema.