Rais wa Marekani Donald Trump amesifu hatua yake ya kuziongezea ushuru bidhaa za nchi nyingi duniani zinazoingizwa Marekani akisema ni muhimu kwa maono yake kwa ajili ya Marekani.

Kauli yake inakuja wakati akiiongezea maradufu ushuru China wa hadi asilimia 104.

Rais Trump amekiri kuwa mkakati wake wa nyongeza za ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani kwa kiasi fulani umepitiliza lakini amesisitiza maafisa wake wanafanya mazungumzo na nchi nyingi zinazotaka kufikia makubaliano ya kibiashara.

Wakati huo huo, masoko ya hisa barani Asia yameshuka zaidi baada ya Marekani kutangaza kuzibandika bidhaa za China ushuru wa zaidi ya asilimia mia moja.

Masoko ya hisa ya Tokyo na Australia yamesuasua na sarafu ya Korea Kusini imeporomoka kwa viwango ambavyo havijashuhudiwa katika kipindi cha miongo miwili.

Hata hivyo, Beijing imekataa kutimiza makataa ya Trump ya kuondoa ushuru wake wa kulipiza kisasi kwa Marekani.

Lakini baadhi ya wachambuzi wanasema ushuru huo utaiathiri China pakubwa, na kuilazimu kurekebisha uchumi wake na kutegemea pakubwa matumizi ya ndani.

Kwa kweli, ushuru wowote unaozidi 35% utafuta faida zote ambazo biashara za Wachina hupata wakati wa kuuza bidhaa za nje hasa zinazoingia Marekani au Kusini Mashariki mwa Asia, alisema Dan Wang kutoka kwa ushauri wa Kundi la Eurasia.

“Ushuru wowote ambao ni wa juu ni ishara tu,” alisema, akitoa mfano wa takwimu za sekta ya viwanda.

Masoko ya hisa kote duniani yamepoteza matrilioni ya dola tangu hatua hiyo ya Marekani kuanza kutekelezwa.

Wawekezaji wanazidi kutiwa wasiwasi na kuongezeka kwa ushuru ambao huenda ukautumbukiza uchumi wa dunia katika mgogoro mkubwa.

Baadhi ya Wamarekani waliozungumza na BBC wamekaribisha ushuru, wengine wanaogopa kushuka kwa uchumi.