Wimbi la ushirikina limezidi kushika kasi mkoani Mbeya kutokana na kuripotiwa kwa matukio mbalimbali yanayoashiria vitendo hivyo ikiwemo ya uchomaji moto nyumba za watu na wengine kuzikwa wakiwa hai.
Moja ya matukio ya kishirikina yaliyoripotiwa mkoani hapa ni pamoja na familia nne katika Kijiji cha Ihahi, wilayani Mbarali kukosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuteketezwa kwa moto na wananchi wenye hasira wanaozituhumu kufanya mauaji ya kishirikina.
Tukio la kuteketezwa kwa nyumba hizo lilitokea hivi karibuni na kusababisha mali zote zilizokuwa ndani ya nyumba hizo, ikiwemo mifugo kuteketea kwa moto.
Watu waliochomewa nyumba zao walitambulika kwa majina ya Mohamed Mangea na mkewe, Pili Hamisi wanaotuhumiwa kwa ushirikina, Ramadhani Mhongole na wengine waliotambuliwa kwa jina moja moja la Mwampishi na Sekilulumo.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na JAMHURI wamesema wamefikia hatua ya kuteketeza makazi ya watu hao baada ya Serikali wilayani kupuuza madai yao dhidi ya watu hao walipotoa taarifa za mauaji.
Mwenyekiti wa Kijiji, Ramadhan Hassan anasema tuhuma za kuwepo kwa mauaji ya kishirikina yaliyofanywa na watu waliochomewa nyumba zao yamekuwepo kwa muda mrefu sasa, lakini Serikali ngazi ya wilaya haikuzifanyia kazi ipasavyo.
Kwa upande wake, Ramle Ibrahim ambaye ni mtoto wa mmoja wa waathirika wa tukio la kuchomewa nyumba anasema kabla ya kuchoma nyumba ya wazazi wake vijana kadhaa walikwenda nyumbani kwao wakiwa wamebeba mapanga.
Anasema walianza kuwapiga wazazi wake na kuwataka waondoke kijijini hapo. Wakati wa tukio hilo wazazi wake walilazimika kukimbilia kituo cha polisi kunusuru maisha yao.
“Asubuhi kundi la watu ambao wengi wao walikuwa ni vijana walikuja wakiwa na mapanga na wakaanza kuwaamuru wazazi wangu waondoke hapa nyumbani,” anasema Ibrahim.
Anasema katika vurugu hizo mama yake alijeruhiwa ubavuni baada ya kukatwa na panga na mmoja wa vijana hao. Wilayani Mbarali, nako yamejitokeza matukio ya ajabu baada ya wananchi wa Mtaa wa Ilolo, jijini Mbeya kuwakataa na kuwafukuza wanachi wenzao kwa ushirikina.
Wananchi hao walimfukuza mtaani, Zainabu Zuberi wakimtuhumu kuhusika na ushirikina. Siku moja baadaye kijana mwingine alikamatwa akiwa na kiganja cha mkono wa mtu nyumbani kwake.
Polisi wamemkamata Baraka Kibona (30) mwishoni mwa wiki katika eneo la Mndali ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Ilolo akiwa na kiganja cha mkono wa kulia ndani ya nyumba yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakael Masaki amelithibitishia JAMHURI uwapo wa matukio hayo. Anasema kijana huyo alificha kiganja hicho kwenye boksi kwa kukizungushia kamba.
Mtuhumiwa anakiri kumiliki kiungo hicho anachodai alipewa na mganga wake wa kienyeji kukitumia kujikinga na wabaya wa biashara na fedha zake zisichukuliwe kishirikina.
Majirani wameliambia JAMHURI kuwa mtuhumiwa amekuwa akijigamba kuwa atafanya vitu vikubwa ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za kifahari na kununua magari.
Wanasema mtuhumiwa alitumia kiganja hicho kwa ‘chuma ulete’ na siyo kujilinda kama anavyodai. Chumba kilimokuwa kiganja alikipanga na alikuwa hakitumii.
Chumba kilikutwa na unga, maboksi yaliyokuwa na fedha Sh 500 kila moja zilizowekwa juu ya nguo nyeupe zinazodhaniwa kuwa ni sanda.
Wilayani Rungwe mtoto wa miaka 11 mkazi wa Kijiji cha Kandete (jina linahifadhiwa) ametimuliwa katika kijiji hicho baada ya kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kishirikina.
February 5, mwaka huu wananchi walipata taarifa za mtoto huyo kutamba kuwa hakuna mtu yoyote katika kijiji hicho mwenye uwezo wa kushinda nguvu zake za kishirikina.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Issa Mwemsi ameliambia gazeti hili kuwa ofisi yake imeshindwa kuingilia uamuzi huo wa wananchi kutokana na mtoto kukiri kuhusika na ushirikina.
Anasema kijijini hapo kumekuwepo matukio ya kushangaza ambayo yanahusishwa na imani za kishirikina.
Hata hivyo, Mwenyekiti amebainisha kuwa mtoto huyo amekuwa akitaja baadhi ya matukio ambayo ameyafanya kijijini hapo kuwa ni pamoja na kuua mifugo ya wanakijiji. Matukio mengine ni kuwapoteza watu katika mazingira ya kutatanisha, kupandikiza magonjwa ndani ya jamii ambayo yamekuwa yakiwatesa kijijini hapo na mengine.
Mwenyekiti anasema kutokana na hali hiyo ametoa taarifa kwa vyombo husika kulifanyia kazi suala hilo.
Mtoto baada ya kutimuliwa kijiji hapo, haijulikani amepotelea wapi hali iliyozua hofu kwa wanakijiji waliomfukuza kutokana na majigambo yake kwani wakati anakimbia aliwaonya wote waliomfukuza kuwa wangeyeyuka. Amelelewa na bibi yake.
JAMHURI imebaini kuwa ushirikina unachochewa na ugumu wa maisha kwa wananchi kuamini kuwa utawaletea kipato.