Serikali ya Tanganyika ilichukua msimamo wa kuwa kusaidia ASP baada ya mwaka 1960 na kabla ya mwaka 1964 kwenye uchaguzi Zanzibar.

Tanganyika ilitaka kutoa msaada wa hali na mali kwa ASP ili ishinde uchaguzi wa mwaka 1961 na wa mwaka 1963. Miongoni mwa masharti ya misaada hiyo tangu mwaka 1962 ilikuwa ni Zanzibar kujiunga na Shirikisho la Afrika Mashariki pindi wataposhinda. Mwalimu Nyerere na Rashid Kawawa waliwaambia viongozi wa Zanzibar kwenye maongezi tofauti kwamba watawasaidia, lakini kwa maelewano kwamba watakubali kujiunga kwenye Shirikisho la Afrika Mashiriki.

Miongoni mwa misaada ambayo Tanganyika ilipatia ASP ulikuwa ni kuwapa nafasi watangaze kwenye redio ya Tanganyika Broadcast Corporation (TBC). Serikali ya kikoloni ya Zanzibar ililalamika sana kuhusu hili, lakini Tanganyika ikaendelea. Serikali Tanganyika iliendelea kuruhusu matangazo yaliyosaidia ASP.

Kulikuwa na mvutano kati ya ZPFL na ASP mnamo Januari, 1963. Adam Mwakanjuki alienda Dar es Salaam akatangaza TBC kwamba hakukuwa na mvutano kati ya ZPFL na ASP. Hata hivyo, Abbas Sykes alienda Zanzibar mwishoni wa mwezi huo kuwaambia viongozi wa ZPFL kuacha kushambulia viongozi wa ASP au hawatapata tena msaada kutoka TANU na hawatakubalikwa kuingia Tanganyika tena.

Sykes alikuwa Regional Commissioner na mmoja wa viongozi wa TANU; Mwalimu Nyerere alimtuma Sykes Zanzibar mnamo Januari 27 kwenda kupatanisha ASP na ZPFL. Sykes alihudhuria mkutano wa Central Committee (Kamati Kuu) wa ASP ambao walikuwapo Ahmed Diria Hassan na Hassan Nassor Moyo.

Sykes aliwaeleza kwamba ametumwa na Mwalimu Nyerere kuhakikisha hakuna ugomvi kati ya ASP na ZPFL. Baadhi ya viongozi wa Zanzibar walianza kuzungumzia mapinduzi kama hakutakuwa na uchaguzi Julai 1963. Ahmed Diria Hassan alisema kwamba “Master Plan for National Revolution” itachukuliwa hatua kama uchaguzi wa mwaka 1963 hautakuwapo.

Viongozi tofauti wa ASP walizuru Tanganyika Februari, 1963 na kukutana na viongozi wa TANU. Inasemekana TANU ilikuwa inatoa msaada wa pesa. Viongozi wa ASP pia walipata msaada kutoka PAFMECSA (jina lilibadilishwa kutoka PAFMECA mwaka 1962 ili kujumuisha nchi za Kusini mwa Afrika).

Miongoni mwa masharti ya msaada huo ilikuwa kwa Zanzibar kujiunga kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki pale ASP wataposhinda uchaguzi. Abeid Amani Karume alienda Tanganyika Machi 1963 akapewa Sh 10,500 kutoka kwa Katibu Mkuu wa PAFMECSA, Peter Koinange. Katika mkutano wa ASP Machi 10, 1963 Karume alisema Shirikisho la Afrika Mashariki litaundwa baada ya ASP kushinda. Karume alitaarifu Kamati ya Utendaji ya ASP Machi 19 kwamba PAFMECSA imetoa jumla ya Sh 30,500.

Msaada kwa vyama vya wafanyakazi uliongezeka mwanzoni mwa mwaka 1963. Hassan Nassor Moyo alimshukuru Mwalimu Nyerere mnamo Machi 1963 kwa simu ya maandishi (telegramu) kwa kumwachia Victor Mkello na wenzake. Mkello, Alfred Tandau na Mohammed Amiri walienda Zanzibar katikati ya Aprili, 1963. Walienda kusaidia vyama vya wafanyakazi wa Zanzibar na kuangalia jinsi ya kutoa misaada mingine.

Viongozi wa Zanzibar walishauriana na wa Bara jinsi wanavyoweza kupata kura zaidi. Katika mkutano wa ASP uliofanyika katika nyumba ya Saleh Saadalla Akida mwishoni wa Aprili 1963, Thabit Kombo alizungumzia tatizo la kura za Wahindi. Kombo alisema kwenye mkutano huo kwamba aliwasiliana na Mwalimu Nyerere kuhusu hilo tatizo.  Kombo aliomuomba atume waziri wake mwenye asili ya Kihindi Zanzibar ili ajaribu kuwashawishi Wahindi wapigie kura ASP.

Uchaguzi wa Julai 1963 ulikuwa wa mwisho. ASP walishinda viti 13, ZNP ilishinda viti 12 na viti 6 vilivyobaki vilienda kwa ZPPP. Chama kitachounda serikali kilikuwa ni kile kilichoweza kujiunga na ZPPP. Jitihada zote za ASP kupata washindi wa ZPPP wajiunge na ASP zilishindikana. ASP walishindwa kuunda serikali kwa sababu walipata viti vichache baada ya ZNP na ZPPP kujiunga. Ikumbukwe ASP walipata kura nyingi zaidi za wapiga kura wote. ASP walipata kura 87,085; ZNP 47,950, na ZPPP 25,609; ZNP/ZPPP ilipata kura 73,559.

Wengi wa Bara na Zanzibar waliona ugawaji wa viti haukuwa wa haki. Hili lilichangia kukubalika kwa wazo la kuchukua serikali kwa nguvu.

Kwa upande wa ZNP, Abdulrahman Babu tayari alikuwa ana matatizo na chama chake mwanzoni mwa mwaka 1963. Babu alijiuzulu uanachama wa ZNP Juni 16. Babu alipanda ndege na familia yake baada ya hapo akaenda Dar es Salaam. Juni 18, Babu alitangaza kuanzishwa kwa chama kipya UMMA akiwa jijini Dar es Salaam. Alitangaza viongozi wa chama hicho kipya wakiwamo Abdulrazak Musa Simai na Salim Ahmed Salim El Riyami.

Ingekuwa vigumu kwa Babu kutangaza chama kipya Dar es Salaam bila kupata idhini ya TANU. Babu aliondoka Dar es Salaam akaenda Nairobi, Kenya ambako alifanya mazungumzo na Oginga Odinga.

Uhusiano wa chama cha wafanyakazi cha Tanganyika na Pemba Federation of Labor uliendelea Juni 1963. TFL na PFL kilitoa tamko la pamoja lililochapishwa na gazeti la Tanganyika Standard mnamo Juni 13; tamko hilo lilisema kwamba vyama hivyo vya wafanyakazi vinataka kuona ushirikisho wa Afrika Mashiriki. Vyama hivyo viliandika kwamba vinataka kujenga “Socialist East African States based on principles of Pan-Africanism and Democratic Socialism.”

Matokeo ya uchaguzi wa Julai 1963 uliweka ASP kwenye hali ngumu. Mkutano ulifanyika Ngambo kati ya Karume, Babu, Othman Shariff na Ali Sultan Issa baada ya uchaguzi kutangazwa. Miongoni mwa maazimio ya mkutano huo ni kuwashawishi viongozi wa ZPPP kuunda serikali ya umoja. Aboud Jumbe, Saleh Saadalla Akida na Hasnu Makame walienda Pemba Julai 15 kujaribu kuzungumza na Mohamed Shamte.

Baadhi ya ripoti zinadai kwamba Shamte alihongwa Sh 60,000 ili ajiunge ZNP; madai hayo hayajathibitishwa. Lakini ni wazi kwamba Shamte alikubali kujiunga na ZNP na moja ya matakwa yake yalikuwa apewe Uwaziri Mkuu.

Tanganyika waliendelea kushawishi viongozi wa Zanzibar wajiunge kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki mwishoni mwa Julai 1963. Walifanya hivyo pamoja na kwamba ZNP/ZPPP walikuwa tayari wameshauunda serikali.

A.N. Swai na Tom Mboya walienda Zanzibar Julai 23, 1963 kuzungumza na viongozi wa Zanzibar kuhusu ushirikiano wa Afrika Mashariki. Swai alizungumza na Othmani Shariff, Hasnu Makame na Jaha Ubwa Jaha huko Migombani. Mwezi Agosti, Hanga na Aboud Jumbe walisema wazi kwenye mikutano kwamba watatumia nguvu kuchukua serikali. Jumbe alisema kwenye mkutano wa ASP Mwembeshauri Agosti 20 lazima serikali ipinduliwe kwa “economic blockade” kutoka Bara au kwa nguvu.

Mkutano uliofanyika Kikwajuni, Septemba 26; Adam Mwakanjuki alisema kwamba waziri lazima atoke ASP ama sivyo watachukua serikali kwa nguvu.

Chama cha UMMA kiliendelea kujijenga na kuimarisha uhusiano wao na serikali ya Tanganyika. Babu na Ali Sultani walisafiri kati ya Zanzibar na Dar es Salaam bila kutumia paspoti zao Agosti na Septemba 1963.

Babu aliondoka Dar es Salaam Septemba kwenda Uingereza kwa kutumia paspoti ya Tanganyika. Kitendo cha serikali ya Tanganyika kumpa Babu paspoti kinaonesha dhahiri kwamba walikuwa wanamsaidia kwenye mipango yake. Babu alijaribu kuhudhuria London Conference, lakini akazuiwa kuingia. 

Ni wazi kwamba wakati mazungumzo yanaendelea Uingereza kuhusu hatma ya Zanzibar, viongozi wa ASP na UMMA walikuwa wanafanya mipango ya siri na viongozi wa Bara. Mazungumzo hayo yalikuwa ni pamoja na wachukue hatua gani kwenda mbele baada ya uchaguzi wa Julai 1963. Tangu mwaka 1962, Kambona na viongozi wengine wa TANU walifanya maandalizi pale ambako ASP watashindwa kuchukua serikali.

Mazungumzo hayo na ushirikiano wa karibu viliongozeka mwaka 1963. Kwa upande wa Tanganyika, viongozi wake walisema wako tayari kuisaidia ASP kwa namna yoyote kwa maelewano kwamba watashiriki kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki. Uamuzi wa serikali ya Uingereza kuipa dola ZNP/ZPPP Desemba 1963 kuliamsha mpango wa kuipindua serikali hiyo. Viongozi wa Bara walikuwa tayari kutoa msaada huo.

Kwenye miaka ya 1950 TANU ilijitahidi kusaidia harakati za uhuru wa Zanzibar. Walijitahidi kuunganisha vyama vya kisiasa mwishoni wa miaka hiyo; lakini kazi hiyo halikufanikiwa. Kuanzia mwanzoni wa miaka ya 1960 viongozi wa Bara waliamua kutoa msaada wao wote wa hali na mali kwa ASP. Hivyo basi, Mapinduzi ya Januari na Muungano wa Aprili, 1964 havikutokea ghafla tu. Mapinduzi na Muungano vilikuwa matokeo ya miaka mingi ya uhusiano wa karibu kati ya viongozi wa Zanzibar na Tanganyika.

 

>>TAMATI>>

 

Mwandishi wa makala hii, Azaria Mbughuni, ni Assistant Professor wa Historia katika Chuo Kikuu cha Lane, Tennessee, Marekani.