Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo amesema kuwa ushiriki wa wanamichezo kutoka TRA katika michezo ya aina mbalimbali katika michezo ya Mei Mosi unalenga kusambaza ujumbe wa ulipaji kodi pamoja na kuhamasisha suala zima la kutoa na kudai risiti za kieletroniki za EFD.
Mkurugenzi Kayombo ameyasema hayo alipotembelea kambi ya wanamichezo wa TRA wanaoshiriki michezo ya Mei Mosi inayoendelea mjini Singida tarehe 29.4.2025.
“Tunaposhiriki michezo hii tunatambua kuwa tuna fursa ya kutoa ujumbe mbalimbali kama vile kutoa risiti, kuwasilisha ritani, kujisajili kuwa Mlipakodi na kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari “ amesema Kayombo.
Aidha, Kayombo ameongeza kuwa ushiriki kwenye michezo hii na uwepo wa wingi wana michezo ambao wanavaa ujumbe mbalimbali umekuwa chachu ya kusambaza ujumbe wa kodi kwa wananchi wa mkoa wa Singida pamoja na wageni wote waliofika mkoani hapa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani hapo tarehe 1 Mei, 2025.
Wanamichezo kutoka TRA wameshiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, pete, kikapu, volleyball na michezo ya jadi ambapo washindi wa michezo hii watatangazwa mbele ya mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



