Na Lawrence Kilimwiko, DAR ES SALAAM
“Sisi tunaoishi vijijini huku, haki zetu zote zina bei. Yaani hata ukikamata mwizi wa ndizi yako, ili umkamate inabidi uwe na hela ya kumpa mgambo akukamatie mwizi wako. Ukimpeleka mahakamani unahitaji hela ya teksi, ili mwizi wako umfikishe magereza”. Haya ni maneno kutoka kinywani mwa Askofu Benson Bagonza wa KKKT, Dayosisi ya Karagwe (rejea JAMHURI Januari 9-15, 2018)
Moja ya kikwazo kikubwa kabisa katika vita ya kupunguza rushwa miongoni mwa jamii ya Watanzania ni ukosefu wa ujasiri wa kufunguka na kupaza sauti.
Anachosema Askofu Bagonza ni kile ambacho wananchi wanaweza kusema kama wakijaliwa ujasiri na kupewa sauti.
Tabia ya kukaa kimya inatokana na hofu na pengine ule ukweli kwamba hata wakilalamika, huwa hakuna wa kuwasikiliza. Anayekaa kimya siyo mjinga. Anahofu kushughulikiwa na watuhumiwa hasa katika nchi ambayo hakuna sheria inayomlinda anayetoa siri dhidi ya wala rushwa.
Huko vijijini wananchi wanalazimika kutoa fedha hata kwa huduma zinazotolewa bure. Hali kadhalika, wamefika hatua ya kuamini kwamba ili mtu ahudumiwe katika mamlaka za umma ni sharti atoe kitu kidogo bila kujali kama yeye ni mlalamikaji au mlalamikiwa. Wote wanalazimika kutoboka mifukoni.
Kwa bahati nzuri, chini ya utawala wa Rais John Magufuli, juhudi zinafanyika kurejesha utawala wa sheria, uwazi, na uwajibikaji miongoni wa watumishi wa watu.
Juhudi za Rais Magufuli zinapata msukumo zaidi kwa uwepo wa makundi ya kijamii ambayo yamejiingiza katika mapambano ya kuzuia rushwa.
Juhudi zote hizo, hata hivyo, zinaweza kuzaa matunda pale tu ambako kila raia na kila mzalendo anajitokeza na kuchukua hatua badala ya kukaa kimya.
Ushiriki wa wananchi katika mapambano ya kuzuia rushwa yameainishwa vizuri sana kwenye mradi wa “Tuungane Kutetea Haki”, unaoendeshwa kwa pamoja na mashirika ya hiari ya Civics Education Teachers Association (CETA), Konrad Adenauer Stiftung (KAS) na Actions for Democracy and Local Government (ADLG) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).
Wajibu wa wananchi katika mradi huu ni pamoja na kuchagua viongozi makini wa Serikali katika ngazi zote na kuchukua hatua dhidi ya viongozi wala rushwa.
Mradi unawaelimisha na kuwahamasisha wananchi waone umuhimu wa kuchagua kamati za ufuatiliaji wa rasilimali za umma na za ushauri juu ya utawala bora kwenye maeneo yao.
Lakini pia, ni wajibu wa wananchi kutambua na kutoa taarifa mara wanapoona tabia au viashiria vya rushwa vya aina zote.
Moja ya kazi inayofanywa na mradi ni kuwajengea uelewa, mwamko, hamasa pamoja na ujasiri wa kuchukua hatua badala ya kukaa kimya.
Kupitia mafunzo, wananchi wanajengewa uwezo wa kupata na kufuatilia taarifa za mapato na matumizi ya fedha/rasilimali za umma. Hii ni haki yao ya msingi ambayo japo ipo kisheria, wananchi hawaifahamu.
Kupitia mradi wa “Tuungane Kutetea Haki”, wananchi wanafundishwa kuzijua sheria husika hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali Kuu inahimiza Serikali za Mitaa kutoa taarifa za fedha kwa wananchi tena kwa wakati.
Faida za wananchi kupata taarifa ziko nyingi. Zinawasaidia watu kupata na kutumia taarifa za fedha. Hali kadhalika, inawasaidia watu kuelewa uhusiano baina ya huduma zinazotolewa, fedha zinazotengwa na matumizi halisi.
Mara zote watu katika jamii iliyoelimika na inayojitambua huacha hofu na woga. Badala yake huchukua hatua kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika dhidi ya tabia za viongozi na watumishi wa umma wapendao hongo au wanyanyasaji.
Kwa kutambua kuwa hofu, woga na silika ya kukaa kimya ni moja ya hulka ya watu wa vijijini/pembezoni, mradi wa “Tuungane Kutetea Haki” umejielekeza huko hasa ikizingatiwa kuwa ndiko wanakoishi watu wengi wa hali ya chini.
Na kama hiyo haitoshi, huko ndiko ambako rushwa na aina nyingine za uonevu zimeshika hatamu. Serikali hivi sasa inapelekeka fedha nyingi za miradi ya maendeleo na kupambana na umaskini. Lakini kwa sababu ukosefu wa utawala bora na rushwa, juhudi hizo za Serikali hazionekani.
Kwa sababu hiyo, kuelekeza nguvu katika mapambano dhidi ya rushwa, utawala mbovu na uwajibikaji vijijini, ni moja ya hatua murua na iliyo endelevu kabisa. Huko ndiko haki za binadamu zinavunjwa kila uchao, lakini pia huko ndiko kunapatikana kila aina ya kielelezo cha umaskini na mkwamo wa maendeleo ya watu.
Wakati Serikali inazidi kumimina fedha za miradi ya maendeleo huko, kiasi kikubwa cha fedha hizo hakiwafikii walengwa au kutumika kwenye miradi iliyokusudiwa kutokana na wizi, ubadhirifu, kutokujali, usiri pamoja na ukosefu wa uwajibikaji, bila kusahau mdudu – rushwa.
Kama hiyo haitoshi, watu wema wasio na hatia wamejikuta wakitoa rushwa hata kwa huduma ambazo wanastahili kupewa bure.
Hii ndio sababu mradi huu unajielekeza katika kubadilisha hali hiyo huko vijijini mkazo ukiwa katika utoaji wa elimu, kupata mwamko na mtazamo mpya wa umma.
Ni dhahiri mambo yanayochangia kushamiri kwa rushwa katika maeneo ya pembezoni /vijijini ni ukosefu wa elimu pamoja na hofu ya wananchi. Wananchi wamejengewa hofu ya kuogopa kudai haki zao kwa mamlaka husika.
Kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania, hivi sasa, kumejengeka tabia ya kutegemea utendaji wa kiongozi mmoja mmoja badala ya kujenga mfumo unaofanya kazi hata pale watendaji hawa mahiri watakapoondoka.
Ndio maana mkazo umewekwa kwenye ujenzi wa msingi wa mfumo ili uweze kufanya kazi pasipo kutegemea uwepo wa mtu. Kuwawezesha wananchi kujua utaratibu unatakiwa kufuatwa katika kupata huduma au haki iwe kwenye zahanati, kituo cha polisi, ofisi ya kijiji au katika Mahakama ya Mwanzo.
Uelewa huu si tu utarahisisha upatikanaji wa huduma, bali pia utapunguza urasimu usio na tija wenye nia ya ‘kudai kitu kidogo’.
Chini ya mradi wa “Tuungane Kutetea Haki” redio jamii zimepewa nafasi kubwa katika kuelimisha umma nini maana ya utawala bora, uwajibikaji na aina zote za rushwa bila kusahau wajibu wa wananchi.
Redio jamii zinategemewa kuwatumia wataalam kutoka kwenye azaki za kiraia na mashirika ya hiari au vyama vya kitaaluma katika kuelimisha wananchi juu ya wajibu na haki zao katika mazingira yao ya maisha ya kila siku.
Kwa njia hii mfumo mzima wa kiutawala, kisiasa, kiuchumi na kijamii utaweza kujengwa na kufuatwa pasipo watu kuyumbishwa.
Mwandishi wa makala hii, Lawrence Kilimwiko, ni mwanahabari mahiri ndani na nje ya Tanzania. Anapatikana kwa simu: 0754-321308, barua pepe: [email protected]