Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
SPIKA wa Bunge na Rais wa 31 wa Muungano wa Mabunge Duniani IPU ,Dkt. Tulia Ackson, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, mkoani Pwani, kuacha ushindani na makundi ndani ya chama, ambao unaweza kusababisha madhara kwa kutoa upenyo kwa upinzani wakati wa Uchaguzi.
Aidha Dkt. Tulia aliwaambia wanachama wakati wa Uchaguzi ukifika wachague viongozi wanaowafaa na bora badala ya kuchagua wale wenye nia ya kutaka kujaribu.

Akizungumza April 25,2025 na viongozi ,mabalozi pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kibaha Mjini, kutoka kata ya Viziwaziwa,Kongowe na Msangani wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, Dkt Tulia ambae alikuwa mgeni maalum aliongeza, waachane na ushindani ili kukiimarisha Chama.
“Msifanye ushindani wa namna ya Yanga na Simba, bali muangalie viongozi ambao wanaonekana kufanya kazi kwa manufaa yenu”.
Vilevile Tulia anabainisha, Kibaha Mjini haipo kinyonge, ilani ya utekelezaji ya CCM imetekelezwa kwa kiasi kikubwa.

” Wanaccm lazima tuwatupe mbali wapinzani, utekelezaji unaonekana kwa macho, Rais Samia Suluhu Hassan anastahili heshima kwa kumpa kura za ushindi na sio za kinyonge.”
Nae mgeni rasmi Mjumbe wa Kamati Kuu na Mlezi wa Mkoa wa Pwani, Leilah Ngozi alisema wanachama wanaojipitisha kwa kufanya kampeni kabla ya wakati, wakemewe bila woga na kufikishwa kwenye vikao vya kimaadili.
Pia aliwakumbusha viongozi kuzingatia haki katika kufanya uteuzi wa nafasi mbalimbali za Uongozi katika mchakato wote wa uchaguzi.
Mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, alieleza mafanikio yaliyopatikana bungeni, akisema kuwa asilimia 97 ya maswali na majibu yaliyoulizwa bungeni yametekelezwa.
“Naishukuru serikali kwa kutatua kero mbalimbali kupitia sekta ya afya, maji, elimu, barabara ambazo nilizozifikisha bungeni na nyingine zinatekelezwa na serikali kuu,” alisema Koka.

Koka anajivunia kuhusu utekelezaji wa ilani ya CCM, akisisitiza kuwa anajivunia hatua zilizofikiwa, ikiwemo kushirikiana na viongozi wa wilaya kupigania halmashauri ya Mji kuwa na hadhi ya Manispaa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Mwl. Mwajuma Nyamka alieleza , mji huo una kata 14 ,wajumbe wa mkutano huo ni 8,000 ,mikutano itafanyika kwa siku tano kuanzia April 23- 27 ambapo kila siku zitashiriki kata tatu .
