Zipo taarifa kwamba “wakubwa” wanajiandaa kufanya mipango ya kuwaengua wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wasishiriki Mkutano wa Bunge la Bajeti unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.

Pia wabunge, karibu wote kutoka chama hicho, wameandikiwa barua za wito wakitakiwa wakieleze mbele ya Kamati ya Maadili ili wajibu kile kinachotajwa kuwa ni “utovu wa nidhamu” waliouonyesha wakati wa vikao vilivyopita.


Agosti, mwaka jana niliandika kwenye ukurasa huu makala yenye kichwa cha habari, “Bunge lisiposema, wabunge watasema”.


Nilimsikiliza Naibu Spika Job Ndugai akilalamika kwamba nidhamu ya baadhi ya wabunge, hasa vijana si nzuri. Ndugai anarejea matukio kadhaa yaliyotokea wakati wa Mkutano wa Bunge la Bajeti. Analalamika kwamba asilimia zaidi ya 70 ya wabunge wa sasa ni wageni, na kwamba kuna vijana wengi ambao bado hawajazisoma na kuzitambua vema Kanuni za Kudumu za Bunge.


Mtazamo wa Ndugai kidogo unafanana na wachambuzi wengine wanaoamini kuwa matumizi ya runinga kurusha vikao vya Bunge, yamechangia wabunge wengi wafanye kazi za kisiasa kuliko za kibunge. Kwa mtazamo wao, wabunge wamejikita zaidi kutaka waonekane kwa wapigakura kuliko kujadili hoja zinazowasilishwa bungeni.


Nilisema nina mtazamo tofauti kidogo na ndugu zangu hawa. Kweli, inawezekana kuwa ugeni na ujana vikawa vigezo vya kuwapo haya tunayoendelea kuyaona na kuyasikia katika vikao vya Bunge. Kweli, inawezekana wakawapo wabunge wanaotaka kuwafurahisha wapigakura ili ikiwezekana mwaka 2015 wawatazame kwa jicho la huruma.


Mtazamo wangu kwa hoja ya Ndugai na ndugu zangu wengine ni kwamba jeuri tunayoiona kutoka kwa wabunge – hasa vijana – tena wa vyama vya upinzani na CCM inatokana na ukimya wa Serikali katika mambo ya msingi.


Wafuatiliaji wa mijadala bungeni wanaona na kusikia hoja nzito na za kufikirisha zinazotolewa na wabunge wa kambi zote, hasa Upinzani. Hoja zinazotolewa na wabunge hawa hazipati majibu ya kuridhisha.


Tofauti na wazee, vijana wa dunia ya leo wanataka kuona mambo yakienda kwa kasi zaidi. Hawataki mwendo wa kusuasua na wa ubabaishaji.


Wanataka kuona watuhumiwa wa masuala mbalimbali wakishughulikiwa haraka. Tena wapo vijana ambao wengine huwa hawataki hata kusubiri sheria ichukue mkondo, bali wao wenyewe waichukue mkononi. Ndiyo maana tunashuhudia mauaji ya wanaojiita “wenye hasira kali” yakifanywa na vijana. Sijasikia magenge ya wazee wakifanya hayo.


Mhimili mkubwa kama Bunge unapotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa, lakini ukakaa kimya, mbunge gani zuzu atakayekiheshimu kiti cha Spika? Kamati ya Nishati ni tone tu. Kamati zote zina walakini.


Watanzania wanalia umasikini. Wanajiuliza, mbona Tanzania ina madini ya aina zote? Mbona ina gesi (na mafuta yapo), ina Serengeti ambayo ni hifadhi kubwa duniani? Mbona ina Selous ambalo ni pori la akiba kubwa kuliko yote duniani? Mbona ina pwani ya bahari yenye urefu wa kilometa karibu 1,000? Mbona Tanzania ina mito na maziwa makubwa katika Afrika? Huo Mlima Kilimanjaro, lini umehitaji kipuri ili uendelee kuwapo? Bandari zetu – Tanga, Dar es Salaam, Mtwara – mbona zinatosha kuikomboa Tanzania?


Nchi ambayo ina misitu ya kila aina, nchi ambayo inastawi kila kitu, nchi ambayo kijiografia inategemewa na mataifa mengi, nchi ambayo kisiasa ina ahueni, nchi ambayo ina lugha moja ya kuwaunganisha watu wake, nchi yenye watu wenye akili, nchi yenye rasilimali watu ya kutosha; kwanini pamoja na sifa zote hizo, inaendelea kuwa masikini?


Wabunge na wananchi wanaoitakia mema wamekuwa wakijaribu kutoa maoni ya kuondokana na umasikini huu. Kwa mfano, wanaiambia Serikali kwamba matumizi ya Serikali ni makubwa mno – kila siku Watanzania lazima waonekane ughaibuni – wizi wa mali ya umma umevuka mpaka, udhibiti wa rasilimali zetu haupo, maadili ya viongozi hakuna. Pamoja na ushauri wote huu, Serikali imetia pamba masikioni. Wa kuyazibua ni nani? Wa kuyazibua ni Bunge. Wabunge wanazungumza, lakini kiti cha Spika ni kama kimeamua kula yamini ya kuitumikia Serikali. Bunge limegeuzwa na Mama Makinda na Kaka Ndugai kuwa mhuri wa kweli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nauliza, katika mazingira ya aina hii, mbunge gani anayeipenda Tanzania anaweza kuwa na lugha ya staha?


Kwa mfano, hivi kweli Tanzania ya leo, pamoja na misitu yote hii inayokatwa mkaa, inaweza kulia kwa watoto wake kukosa madawati? Kama tunashindwa kuwa na madawati, tutaweza kujenga nyumba za walimu na maabara? Hivi kweli tunakubali shule zetu zifungwe kwa sababu ya kukosa vyoo, tena vyoo vya shimo? Nani katuloga? Tufanye nini? Bunge lazima liisimamie Serikali. Spika na Naibu wake huru. Wasiwe vibaraka wa chama wanachotoka.


Kiti cha Spika kinaogopa. Wabunge wakweli wanajipembua na sasa wanaitwa wakosefu wa nidhamu. Kama kweli mwenendo wenyewe wa Bunge ndiyo huu, kiti cha Spika kitaendelea kupuuzwa maana kinaacha mambo mazito ya nchi yajiendeshe yenyewe. Mhimili wa Bunge usiposemea mambo mazito ya nchi, kazi hiyo itafanywa na mbunge mmoja mmoja. Kwa kuifanya kazi hiyo, wataitwa watovu wa nidhamu.


Kiti cha Spika kilicho butu, kinachokwepesha  mjadala wa suala la watoto wa sekondari asilimia 80 kufeli, kiti cha Spika kinachoziba midomo ya wabunge isijadili uhaba wa maji nchini; kiti cha aina hiyo, hata ningekuwa mimi ningekikosea adabu! Makinda akitaka, arogwe –awafukuze au awasimamishe wabunge wa Chadema! Umma utamhukumu.