Mfanyakazi wa Kiwanda cha Saruji cha Nyati, Charles Reuben, amekufa akiwa kazini huku chanzo cha kifo kikidaiwa ni kufunikwa na kifusi cha makaa ya mawe.
Reuben amekutwa na mauti hayo usiku wa kuamkia Julai 28, 2019 baada ya kuteleza na kutumbukia kwenye eneo linalopokea makaa hayo (coal mill) kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme na mitambo ya kuunguzia malighafi zinazotengeneza saruji (clinker) kiwandani hapo.
Wakati tukio hilo linatokea inaelezwa Reuben alikuwa akichokonoa vipande vya makaa ya mawe ambavyo vilikuwa vimeziba njia ya eneo hilo.
Habibu Mfaume ambaye ni kibarua na amejitambulisha kwamba aliwahi kufanya kazi na Reuben, ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba siku ya tukio eneo la kuweka makaa ya mawe lilikuwa halipitishi makaa vizuri hivyo akaenda kwa ajili ya kuzibua ili mawe hayo yaingie kwenye kinu kwa ajili ya kusagwa na kusafirishwa kwenye mikanda ya mtambo.
“Siku hiyo mkaa ulikuwa umejaa, halafu kwenye kinu pamekaa vibaya, Reuben alipokwenda kusukuma ili ule mkaa uende kwenye mfumo rasmi, wakati anasukuma alikuwa amesimama juu ya mkaa ambao ghafla ulimeguka na akashuka nao ukamfunika,” amesema Mfaume.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 12 alfajiri, na kwamba Mfaume alifanya kazi ya kufyatua mikanda ya mashine hizo na kufanikiwa kuzima mtambo ili asimezwe kisha kutoa ripoti kwa wafanyakazi wenzake juu ya tukio hilo.
“Eneo hili limekaa kama kisima, usalama hakuna, na hili si tukio moja, kuna watu wengine waliwahi kutumbukia lakini tukawawahi na kuwaokoa kabla hawajapata madhara zaidi,” amesema Mfaume.
Zoezi la kuunasua mwili wa marehemu Reuben kwa kutumia gari lenye kijiko lilidumu kwa saa tatu, ambapo walifanikiwa kuufikia mwili na kuunasua kisha kuukimbiza Kituo cha Afya cha Kimbiji.
Chanzo chetu kimesema kwamba Reuben alikimbizwa kwenye Kituo cha Afya cha Kimbiji, Kigamboni, ambako wataalamu wa afya waligundua alikuwa amekwisha kufariki dunia.
Gazeti la JAMHURI limezungumza na mmoja wa madaktari wa kituo cha Kimbiji ambaye amekiri kwamba mwili huo ulifikishwa kituoni hapo na askari wa kituo kidogo cha Polisi cha Kimbiji wakiwa pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Kiwanda cha Saruji cha Nyati.
“Mimi siwezi kusema kama Reuben alifia kiwandani, njiani au hapa kituoni, kwa sababu alifikishwa hapa akiwa bado ni wa moto lakini hakuwa ana pumua.
“Kwa vyovyote vile wote wanaotilia shaka kwamba alifia kiwandani wanaweza wakawa sahihi lakini nilimpima nikawaeleza kuwa amefariki dunia ndipo mwili tukaupeleka chumba cha kuhifadhia maiti,” amesema na kuongeza kuwa alitaka kufanya uchunguzi kuhusu kilichomuua Reuben lakini alielezwa kuwa askari kutoka Kituo cha Polisi Kigamboni wameufuata mwili huo na kuupeleka Hospitali ya Vijibweni kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Hata hivyo baada ya vipimo kufanyika mwili wa marehemu Reuben ulisafirishwa Jumanne na kupelekwa Katoro, mkoani Geita kwa ajili ya mazishi na kwamba Sh milioni tatu zilitolewa na Kiwanda cha Nyati kugharamia mazishi hayo.
Wafanyakazi katika kiwanda hicho wanautuhumu uongozi wa kiwanda kuwa chanzo cha ajali hiyo huku wakibainisha kuwa tukio hilo ni moja kati ya matukio mengi ya ajali yanayojitokeza kiwandani hapo.
Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho ambaye hakupenda jina lake kuwekwa wazi ameliambia JAMHURI kuwa tangu mwaka 2017 zimekuwepo ajali nyingi kiwandani humo lakini viongozi wanazifumbia macho.
Amesema mwaka 2017 mfanyakazi mmoja alinaswa vidole na mkanda wa mashine, hali iliyomlazimu kufanyiwa upasuaji katika vidole hivyo na kupata ulemavu wa kudumu katika vidole vyake.
Mbali na tukio hilo, mwaka jana mfanyakazi mwingine alifariki dunia akiwa kiwandani humo, chanzo kikiwa ni kufyatukiwa chuma usoni.
Marehemu alikuwa mwajiliwa wa kudumu wa kiwanda hicho akiwa na kazi ya kukagua mitambo na maeno ya kiwanda hicho (site attendant).
“Hapa shughuli ziko hivi, unaingia siku tatu mfululizo kama ni kuanzia saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi, halafu unabadilishiwa shift unaingia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni, yaani unakuwa kama hauna muda wa mapumziko.
“Hata siku ukipata muda wa kupumzika ni siku ambayo unatakiwa kufanya shughuli zako za nyumbani, kesho yake tena unarudi kazini, kwa hiyo marehemu Reuben alikuwa hajapumzika kwa muda wa wiki mbili,” amesema mmoja wa wafanyakazi.
Wafanyakazi hao wanasema ratiba ya ufanyaji kazi katika kiwanda hicho ni mbaya, kwani haiwapi muda wa kupumzika na kwamba sera aliyoianzisha mwajiri ya kupunguza wafanyakazi ndiyo inayoleta changamoto kwao.
Inaelezwa kuwa mwajili aliyepo kiwandani hapo ni mpya na kwamba tangu mwaka juzi alipoanza kukiendesha kiwanda hicho amekuwa akifukuza wafanyakazi kwa hoja kwamba anataka kubana matumizi.
“Kama eneo alilofia Charles walikuwa wanakaa wafanyakazi watatu, lakini leo unakaa mtu mmoja, hata maeneo mengine unakuta ‘operator’ ni mmoja huku kazi zikiwa nyingi.
“Hizi kazi ni ngumu na mtu usipokuwa makini kuna uwezekano wa kuumia, kwa sababu kuna muda unakuwa umechoka hadi akili inachoka lakini wao wanakushurutisha ufanye kazi.
“Wao wanachojali ni kuona uzalishaji unafanyika, huwezi kuwaambia kuhusu kuboresha hali ya usalama kwa wafanyakazi, ukionekana unatetea wafanyakazi unafukuzwa,” chanzo chetu kimesema.
Hata hivyo wafanyakazi hao wanasema ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa Kiwanda cha Nyati, kwani eneo hilo pamoja na kuwa hatarishi halina nyenzo yoyote ya kiusalama kwa ajili kumlinda mfanyakazi.
“Kuna maeneo sisi kama mafundi makenika tunavaa mikanda ili tusidondoke lakini unakuta kibarua anapita eneo hilo bila kuvaa mkanda.
“Tangu mwaka jana afisa usalama wa kiwanda anapigania usalama katika kiwanda hiki lakini mawazo yake hayaheshimiki, unakuta hakuna vifaa vya usalama kama kofia ngumu, glovu za kuvaa mikononi, reflector (nguo za kuakisi mwanga) lakini sisi tunalazimishwa kufanya kazi tu,” kimesema chanzo chetu.
Mmoja wa viongozi wa chama cha wafanyakazi kiwandani hapo (jina linahifadhiwa), ameliambia JAMHURI kuwa tukio hilo ni sehemu ya changamoto za kiusalama zinazokikabili kiwanda hicho.
Ameongeza kwamba kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto kubwa ya kiuongozi, kwani kiwanda kinaendeshwa bila kufuata taratibu za kazi.
“Hapa kuna matabaka mawili ya wafanyakazi, kuna wageni (Wahindi) na sisi Waswahili, lakini kiwanda kinabebwa na wageni, na si kwa sababu wana ujuzi wa kazi, ni kwa vile wao wakisema wanaweza kusikilizwa, bila kujali wanasema ukweli au uongo.
“Ajali nyingi zimekuwa zikihusisha Waswahili kwa sababu wanafanya kazi kwa presha, unaweza kukuta mtu anaamrishwa kufanya kazi haraka haraka.
“Hapa wafanyakazi wengi unakuta wana hofu ya kufukuzwa, kwa hiyo wengi wanajikuta wakifanya kazi katika maeneo hatarishi kwa sababu ya hofu hiyo,” anasema kiongozi huyo.
JAMHURI limefika Kimbiji kiwandani hapo ili kushuhudia mazingira ya tukio hilo lakini likaelezwa kuwa mara baada ya tukio hilo mazingira ya eneo lilipotokea yamekwisha kuboreshwa.
Hata hivyo JAMHURI likiwa mapokezi ya kiwanda hicho lilibaini uhaba wa vifaa kinga kiwandani, kwani mmoja wa wafanyakazi alikuwa akilalama kuwa wameaibika baada ya kupokea wageni kutoka Mamlaka ya Usalama Mahala pa Kazi (OSHA) wakashindwa kuwapa kofia za kuvaa pamoja na ‘reflector’ zilizo safi.
Mfanyakazi huyo alisikika akisema: “Yaani kiwanda hiki tunachekesha kweli, wale wageni eti tumewavalisha makofia ya ovyo na machafu, tunashindwa hata kununua ‘reflectors’ za wageni, jamani.” amesema.
Akizungumza na JAMHURI, Afisa Rasilimali Watu, Julieth Daniel, ambaye ndiye msemaji wa kiwanda, amesema hawezi kusema jambo lolote kwa kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali.
“Siwezi kusema jambo lolote, naomba tusubiri taarifa ya uchunguzi ya Polisi. Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi, naomba tusubiri majibu yao,” amesema Julieth.
JAMHURI limezungumza na msemaji wa Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Eleuter Mbilinyi na kuelezwa kuwa tukio hilo limeripotiwa ofisini kwao na kwamba Meneja wa OSHA Kanda ya Pwani analishughulikia.
“Majibu ya uchunguzi yakitoka tutakujulisha, si unajua hatua za uchunguzi hazifanywi kwa siku moja, lazima ushahidi wa kina ukusanywe ili majibu yakitoka hatua stahiki zichukuliwe, nikuahidi tutakujulisha ripoti ikitoka,” alisema Mbilinyi.