Na Tatu Saad,JAMHURI MEDIA

Usajili wa mshambuliaji kutoka nchini Zambia Kennedy Musonda wakati wa dirisha dogo umewapa kiburi cha tambo viongozi wa klabu ya Yanga.

Afisa habari wa klabu hiyo Ally Kamwe amesema uongozi wa klabu hiyo haukukurupuka kumsajili mshambuliaji huyo.

Amesema uongozi uliyafanyia kazi kwa vitendo mapendekezo ya benchi la ufundi wa timu hiyo kumsajili mshambuliaji kama huyo.

Kamwe amesema uongozi ulikaa kimya wakati wadau wa soka walipokuwa wanakosoa usajili wa mchezaji huyo kwani ulikua unajua umesajili mchezaji wa aina gani.

“Tulisikia kejeli za baadhi ya watu kuhusu Musonda, lakini tuliamua kukaa kimya kwa sababu tulijua kuna siku atawajibu kwa vitendo uwanjani. Na imekuwa hivyo.” amesema Kamwe.

Kamwe amedai kuwa Musonda alisajiliwa maalum kwa ajili ya michuano ya kimataifa na kuisaidia timu kwa upande wa ushambuliaji akisaidiana na Fiston Mayele.

“Kila mchezaji anatimiza majukumu yake lakini Musonda huyu aliletwa maalumu kwa ajili michezo ya kimataifa hilo ni ya jambo ambalo linaonekana kwa sasa.amesema Kamwe.

Aidha Ally ameeleza kuwa wanajivunia sana Musonda kwani ni mchezaji ambae ana uwezo wa kufunga na kutoa paso za magoli, hivyo mashabiki wategemee makubwa kutoka kwa mchezaji huyo na klabu kwa ujumla.

“Anafunga anatoa pasi za mabao unadhani nini tunakihitaji kutoka kwake bado kuna kazi kubwa ipo kwa kila mmoja mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,” amesema Kamwe.

Hadi sasa Musonda ameshaifungia Young Africans mabao mawili katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, akifanya hivyo dhidi ya TP Mazembe kisha US Monastir ambayo yamesaidia klabu yake kutinga Robo Fainali ya michuano hiyo.