Utunzaji mazingira

Watanzania hawajitangazi, wao wamekazana kutangaza wanyamapori na vivutio vya utalii peke yake, kama hatujitangazi kwanza sisi wenyewe, hawa wanyamapori mnafikiri wanatutangaza vyakutosha huko duniani?”

Ni Maneno ya Dk. Ellen Oturu, Mratibu wa Miradi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), katika semina ya mafunzo ya wanahabari kuhusu uhifadhi wa mazingira, wanyamapori na utalii hapa nchini.

Mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na waandishi wa habari 30 kutoka vyombo mbalimbali vya habari yanalenga kuwapa mbinu za kufanya uchunguzi na kuandika habari za uhifandhi wa mazingira, wanyamapori na utalii kwa kina.

Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira nchini (JET) chini ya mradi wa miezi sita wa PROTECT (Promote Tanzania Environment, Conservation and Tourism).

Kwenye semina hiyo, Dk. Oturu alisema Tanzania inaongoza kwa vivutio vingi vya utalii lakini haijajitangaza vya kutosha ili kuvifanya vivutio hivyo kuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi.

Anasema: “Kuna utalii wa aina mbalimbali, kuna utalii wa mila na tamaduni za watu, mtu anaweza kuamua kusafiri kwa ajili ya kutembelea sehemu fulani ili aone watu wanaishi vipi pamoja na utamaduni wao.

 “Sasa hapa kwetu unaweza kufikiri hakuna watu kuna wanyamapori na Mlima Kilimanjaro peke yake, matangazo yanayotumika kutangaza utalii wetu ukiyaona unaweza kusema Tanzania hakuna watu, kuna wanyamapori tu, yaani unaweza kufikiri ukishuka uwanja wa ndege utapokelewa na wanyama.

“Hapa ndipo uandishi wa habari unatakiwa kufanya kazi yake kubadilisha taswira hii, tusitake wanyamapori watusemee kimataifa badala yake sisi tunatakiwa kuwasemea huko,” anasema Dk. Oturu.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Bodi ya Utalii nchini (TTB), Geofrey Tengeneza, ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa sekta ya utalii nchini inakua kwa kasi.

Anasema katika kuhakikisha wanajitangaza kimataifa wameweka utaratibu wa kuwatumia waandishi wa habari wa mataifa mbalimbali pindi wanapotembelea nchi yetu kupewa fursa ya kutembelea hifadhi zilizopo nchini na kuandika habari ambazo  zitaitangaza Tanzania pamoja na hifadhi zake katika mataifa yao.

Tengeneza anasema utalii wa utamaduni hapa nchini ni bidhaa mpya ambayo hivi karibuni imeanza kupewa nguvu na kimeanzishwa kitengo maalumu kinachoshughulika na mambo ya utamaduni pekee.

“Tumeweka maofisa ambao wakilala, wakiamka kazi yao ni kufikiri juu ya utamaduni wetu unawezaje kuitangaza nchi yetu na ofisi za kitengo hiki ziko Arusha,” anasema Tengeneza.

Anasema maofisa wa kitengo hicho wamezunguka nchi nzima na kuwahamasisha wananchi kutengeneza vikundi vya utamaduni kwa ajili ya utalii kulingana na maeneo yao.

“Wakati tunaanza tulikuwa na vikundi vichache sana, lakini mpaka sasa kuna vikundi karibu 70 nchi nzima,” anasema Tengeneza.

Anaeleza kuwa kutokana na sekta ya uhifadhi kusimamiwa vema katika uongozi wa Awamu ya Tano, ujangiri wa wanyamapori umepungua na kwamba kwa sasa sekta ya utalii inakua kwa kasi huku idadi ya watalii ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

“Kwa takwimu tulizonazo za mwaka 2017, idadi ya watalii ni milioni 1.3 wakati tukitazama idadi ya watalii kwa mwaka 2016 ilikuwa milioni 1.2, hapo unaona jinsi ambavyo sekta hii inakua kila siku.

“Ukuaji wa sekta unakwenda sambamba na ongezeko la ukusanyaji wa mapato, ambapo sasa hivi kwa mwaka tunakusanya mapato karibia dola za Marekani bilioni 2.3,” anasema.

Tengeneza anasema mikakati ambayo wameianzisha ya kutangaza uhifadhi katika mapori ya akiba yaliyopo ni pamoja na kuwatumia watu mbalimbali kuyatangaza wakiwemo wasichana watano wanaoshinda kinyang’anyiro cha mashindano ya urembo (Miss Tanzania).

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira nchini (JET), John Kichomo, amesema malengo ya semina hiyo ni kuboresha utalii wa ndani ili uweze kukua na kueleweka kimataifa.

Kichomo anasema suala la uhifadhi wa mazingira linapaswa kupewa kipaumbele ili kuitunza ekolojia ya wanyama na mimea na kwamba waandishi wa habari na wadau mbalimbali wa sekta hiyo wanapaswa kufanya ushawishi kwa sekta binafsi ili ziwekeze  kwenye sekta hiyo.

“Tumeanza na mafunzo haya na baadaye tutaendelea na hatua nyingine zinazofuata, ikiwemo ya waandishi husika kwenda kufanya uchunguzi kwenye hifadhi na kuandika habari zinazohusu mazingira.

“Mafunzo haya ni sehemu ya mradi unaoshughulikia kuendeleza uhifadhi wa mazingira ambapo ndani yake kuna kuangalia mafanikio, pia unashughulika na changamoto zinazohusu uhifadhi,” anasema Kichomo.

Umhimu wa kuhifadhi mazingira na wanyamapori

Gerald Mollel, Meneja wa Usajili wa Kemikali nchini, Ofisi ya Mkemia Mkuu, amezungumzia umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira kuwa ni kwa ajili ya kutunza uhai wa viumbe vyote vilivyopo duniani.

Anasema maisha ya binadamu, wanyamapori pamoja na mimea ni vitu vinavyotegemeana na endapo kimojawapo kikitoweka mfumo wa maisha utapata hitilafu.

Anasema: “Ikiwa mimea itakosekana, maisha ya binadamu wala wanyama hayatakuwepo, vilevile binadamu na wanyama tusipokuwepo hata mimea nayo haiwezi kuishi, kwa sababu sisi tunategemea hewa inayozalishwa na mimea, mimea nayo inategemea hewa tunayozalisha sisi pamoja na wanyama,” anasema Mollel.

Raziah Mwawanga kutoka Mfuko wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), akiwa miongoni mwa watoa mada katika semina hiyo alieleza umuhimu wa kuhifadhi mazingira pamoja na wanyamapori kuwa ni kwa ajili ya kuendeleza uhai endelevu baina ya binadamu na wanyamapori.

Alieleza kuwa shughuli za binadamu kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya wanyamapori zinaweza kuleta athari hivyo ili kuleta uwiano sawa watu wote wanatakiwa kuelimishwa kuhusu umuhimu wa wanyamapori walioko katika mazingira yao.

Naye Atilio Tagalile, mwandishi wa habari mkongwe wakati akitoa mada katika semina hiyo alieleza kuwa uhifadhi una manufaa makubwa kwa nchi ikiwa ni pamoja na kuendeleza asili ya dunia.

Tagalile akaongeza kuwa sekta ya uhifadhi na utalii ikiboreshwa uchumi wa nchi utaongezeka kwa kiwango kikubwa, kwani ipo mifano ya nchi kadhaa duniani zimekuza uchumi wake kwa kutegemea sekta hiyo peke yake.

Mwanasheria wa Chama cha Wanasheria wa Mazingira Tanzania (LEAT), Stanslaus Nyembea, akitoa mada katika semina hiyo alieleza kuwa masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yapo kisheria, hivyo kuuendeleza uhifadhi  ni kwa lengo la kuzitii sheria hizo.

Anazieleza sheria hizo kwamba zilianzishwa tangu enzi za mkoloni. “Masuala ya uhifadhi yalianza wakati wa utawala wa Mjerumani, kuanzia mwaka 1885 hadi 1891.

“Mjerumani baada ya kuona changamoto za ujangili na biashara ya meno ya tembo uliofanywa na Mwarabu, aliamua kuanzisha sheria, kanuni na taratibu za kudhibiti uhifadhi,” anasema Nyembea.