Na Stella Aron, JamhuriMedia,Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa ipo haja ya wananchi kuendelea kuelimishwa kuhusiana na umuhimu wa tembo ili kusaidia kulindwa kwa shoroba ambazo zina fursa nyingi kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuwainua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa mdahalo ulioandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Afisa Wanyamapori Mkuu na Mratibu wa Maliasili, Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi, kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa a Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Hawa Mwechaga amesema kuwa tembo ni fursa hivyo wananchi wakielimishwa hilo watakuwa na utayari wa kuzilinda shoroba kwa tija.
“Wananchi wanapaswa kujua kuwa tembo ni fursa, tembo hapaswi kuwa adui, tunapaswa kuwaeleza wananchi juu ya suala hili, wakilielewa hili ni rahisi kwao kushiriki ulinzi wa shoroba,” amesema.
Amesema kuwa kama elimu itatolewa kwa jamii itasaidia wananchi kuchukua hatua za kuhifadhi shoroba kwa kutumia njia mbalimbali ili kuepukana na migongano baina yao na wanyamapori hasa tembo na hata kuzifufua na kuzilinda shoroba bila kuathiri shughuli za binadamu.
“Shida ya mwingiliano wa wanyamapori na binadamu umekuwa mkubwa na maeneo mengi utasikia changamoto hasa ya tembo, sasa tunataka kuwawezesha kutambua fursa za kuwepo na wanyama hao, kwa mfano tembo ukimtengenezea mazingira rafiki hataweza kuwa changamoto bali atakuwa fursa,” amesema.
Ameongeza kuwa suala hilo itawezekana endapo shoroba zilizopo zikigeuka kuwa fedha kwa kuwa na utalii wa picha na ufugaji wa nyuki na mengine mengi.
Akiifafanua kauli yake ya kuwa tembo ni fursa na si tatizo, amesema endapo wananchi watashiriki kulinda shoroba pamoja na kutofanya shughuli zao kwenye maeneo ya karibu na wanyamapori hao ni wazi wanyamapori hao hawataingia kwenye maeneo ya makazi ya watu, lakini pia itakuwa rahisi kwa wananchi kuendesha shughuli za utalii na kujiingizia kipato.
Amesema kuwa Serikali inakuja na mkakati wa kuhakikisha rasilimali zilizopo zinawainua wananchi kwa kuwainua kiuchumi pamoja na kupungua changamto ya ukataji miti.
Ametaja mkakati huo ni kuwapeleka watu katika biashara ya hewa ya ukaa, kuhamasisha utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi na kurudisha mifumo ya ikolojia.
“Changamoto ya mwingiliano wa wanyamapori na binadamu umekuwa mkubwa na maeneo mengi utasikia changamoto hasa ya tembo, sasa tunataka kuwawezesha kutambua fursa za kuwepo na wanyama hao, kwa mfano tembo ukimtengenezea mazingira rafiki hataweza kuwa changamoto bali atakuwa fursa,” amesema.
Naye Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Fortunata Msofe amesema kuwa Serikali amesema kuwa Serikali inazitambua shoroba 61 za wanyamapri nchini, na imeweka mikakati ya kutoa elimu kwa wananchi ili kujua maeneo ambayo wanyama wanapita na kuendelea kufanya shughuli zao na bila migongano.
“Kwa maana maeneo hayo yaweze kuruhusu wanyamapori kupita na wananchi waweze kuishi katika maeneo hayo na kufanya shughuli rafiki kwa lengo la kuondoa migongano baina ya binadamu na wanyamapori,” amesema.
Amesema katika kufanya tathmini hiyo mkakati huo ulizitambua shoroba 61 za wanyamapori nchini, ambapo kati ya hizo 20 serikali iliona ni muhimu kuzirasimisha baada ya mwingiliano wa binadamu na wanyamapori kuonekana kuwa mkubwa na kusababisha mgongano hatari kwa binadamu na wanyamapori .
“ Shoroba hizi zimepewa kipaumbele ikiwa kutafuta rasilimali fedha na utaalamu kuhakikisha maeneo haya yanatambuliwa rasmi kwa kuwekewa alama na kutangazwa kwenye gazeti la serikali.
“Maeneo hayo 20 ni yenye changamoto kubwa zaidi kati ya zile 61, changamoto yake ya mwingiliano kati ya binadamu na wanyamapori ni mkubwa,unasikia kila siku tembo kwenye maeneo haya, kwa hiyo tusipoamua kuweka mipango ya matumizi ya ardhi, changamoto hiyo itakuwa kubwa na kuhatarisha maisha ya wananchi,” amesema.
Amesema shoroba mbili ambazo ni ya Milima ya Udizungwa na Kwakuchinja iko mbioni kutangazwa rasmio huku 18 zinaendelea kufanyiwa kazi na zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inalo jukumu la kutangaza utalii nchini kwa sababu ina usajili wa bidhaa za wanyamapori na imetenga theluthi moja ya eneo kama maeneo yaliyohifadhiwa.
Ushoroba ambayo ni mapito ya wanyamapori huwasaidia kuhama kutoka hifadhi moja kwenda nyingine kutafuta malisho na maji. Hata hivyo kumekuwa na migongano baina ya binadamu na wanyamapori ambapo jamii zinazopakana na hifadhi zimekuwa zikifanya shughuli zao za kibinadamu katika maeneo hayo hali inayofikia kuyaharibu mapito hayo ya wanyama.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Dk Ellen Otaru amesema kuwa mambo mbalimbali yanayosababishwa na migongano kati ya binadamu na wanyamapori hivyo wananchi wakipewa elimu itasaidia kupunguza migongano hiyo.
“Bado wananchi wanatakiwa kupata elimu, hivyo ipo haja ya taasisi mbalimbali au mashirika kushirikiana na JET katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu na kupunguza changamoto hiyo,” amesema.
Amesema kuwa migongano hiyo inayochangiwa na sababu mbalimbali kama wananchi kujenga makazi kwenye shoroba za wanyamapori, kukosekana wa mpango bora wa matumizi ya ardhi, mifugo kuingia kwenye hifadhi ,mabadiliko ya tabia hivyo kama wananchi watapata elimu itasaidia kupunguza changamoto hiyo.