Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea na utoaji wa huduma, kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini.
Hayo yamebainishwa leo bungeni na Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa wakati akisoma hotuba ya bajeti ya wizara hiyo bungeni.
Mbarawa amesema kuwa na mbalibya TMA kutoa utabiri wa hali na tahadharia na tahadhari ya majanga pia ni kupima na kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutafiti kisayansi mabadiliko ya hali ya hewa nchini, kubadilishana taarifa za hali ya hewa katika mtandao wa mawasiliano wa dunia kulingana na makubaliano ya Kimataifa na kuiwakilisha Tanzania katika masuala ya hali ya hewa Kikanda na Kimataifa.
Amesema kuwa Serikali kupitia TMA imeendelea kutoa huduma za utabiri wa kila siku, siku kumi na ule wa muda mrefu pamoja na tahadhari ya matukio ya hali mbaya ya hewa ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao ambapo usahihi wa utabiri umefikia asilimia 86 ambao ni juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
TMA ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa kuanzia tarehe 22 – 27 Januari 2024, na kuendelea kukidhi vigezo vya kumiliki cheti cha ubora (ISO 9001: 2015).
Amesema kuwa katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Ibara ya 59(j) na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III 2021/22-2025/26), Serikali iliahidi kuendelea kuimarisha miundombinu na huduma za hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa rada.
‘Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali kupitia TMA imekamilisha ufungaji wa rada za hali ya hewa katika mikoa ya Kigoma na Mbeya na kufikisha jumla ya rada tano (5) za hali ya hewa nchini. Aidha, utengenezaji wa rada nyingine mbili (2) unaendelea kiwandani nchini Marekani na inatarajiwa kukamilika Novemba, 2024.
‘Rada hizo zitafungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma na hivyo kukamilisha lengo la muda mrefu la kuwa na rada saba (7) za hali ya hewa nchini,’ ameaema Mbarawa.
Ameongeza kuwa sambamba na hilo, Serikali imeingia mkataba wa kuboresha rada za hali ya hewa zilizofungwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza ili kuendana na teknolojia ya kisasa ya rada za hali ya hewa.
Amesema kuwa katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga, Serikali ilikamilisha ufungaji wa mitambo mitano (5) ya kutoa huduma za hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Songwe, Zanzibar, Mtwara, Arusha na Songea.
Mbarawa amesema kuwa taratibu za ufungaji wa mitambo mitatu (3) ya kupima hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Musoma, Iringa na Mpanda zinaendelea.
“Mheshimiwa Spika, pia, Serikali imekamilisha ununuzi wa seti 28 za mitambo ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe (Automatic Weather Stations) ambapo mitambo mitatu (3) imefungwa katika vituo vya hali ya hewa vilivyopo katika viwanja vya ndege vya Mtwara, Songea na Arusha na mitambo 25 inaendelea na maandalizi ya kufungwa katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Tanga, Dodoma, Singida, Kilimanjaro, Katavi, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu, Kaskazini Unguja, Mara na Mwanza.
“Mheshimiwa Spika, kuhusu kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kujenga uwezo kwa watumishi, Serikali kupitia TMA imeendelea na ujenzi wa jengo la ofisi ya Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 39.
“Vilevile, watumishi 74 wanaendelea na mafunzo ndani na nje ya nchi katika ngazi mbalimbali za elimu” amesema.
Waziri Mbarawa amesema kuwa TMA imeendelea kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ambapo jumla ya tafiti nne (4) zilichapishwa katika majarida ya kimataifa ya kisayansi.
Ameongeza kuwa idadi hii inafanya tafiti zilizochapishwa na majarida ya kimataifa kuwa nane (8) ndani ya kipindi cha miaka miwili (2) kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2023/24. Tafiti hizo ni kuhusu tathmini ya matukio ya hali mbaya ya hewa katika Bahari ya Hindi; tathmini ya ongezeko la joto kwa kipindi kati ya mwaka 1982 hadi 2022; tathmini ya hali ya mvua katika vituo vya hali ya hewa nchini; na tathmini ya mabadiliko ya mvua na athari zake katika kilimo kwa nchi za Afrika Mashariki.
Lengo kuu la tafiti hizo ni kuboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini.
Amesema Serikali kupitia TMA imeendelea kutoa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu kupitia ofisi zake tisa (9) zilizopo katika bandari za Malindi – Unguja, Mkoani – Pemba, Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Ziwa Victoria katika Bandari ya Mwanza, Ziwa Tanganyika katika Bandari za Kigoma na Karema na Ziwa Nyasa katika Bandari ya Itungi na hivyo kuendelea kuchagiza shughuli za Uchumi wa Buluu.
Aidha, wadau wa Uchumi wa Buluu ambao wameendelea kupatiwa huduma za hali ya hewa ni pamoja na watumiaji wa vyombo vya usafiri na usafirishaji, Watafiti na wachimbaji wa Mafuta na gesi, Mamlaka za bandari, Wavuvi, Wakulima wa mwani na matango bahari, wafugaji samaki na Vikundi vya usimamizi wa maeneo ya bahari na fukwe.
Amesema kuwa kutokana na umahiri katika utoaji wa huduma za hali ya hewa, mwaka 2019, Shirika la Hali ya Hewa Duniani liliichagua Tanzania kupitia TMA kuendesha kituo cha kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri wa hali mbaya ya hewa (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo katika ukanda wa Ziwa Victoria.
Kituo hicho kipo Dar es Salaam na kinahudumia nchi tano (5) ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi. Sambamba na hilo, TMA iliteuliwa kutekeleza jukumu la kufuatilia ubora wa takwimu za hali ya hewa (data) zinazopimwa katika vituo vya hali ya hewa vya nchi sita (6) vya ukanda wa Afrika Mashariki ikujumuisha nchi ya Sudan Kusini.
Majukumu haya ambayo TMA imeendelea kuyatekeleza kwa ufanisi na kuzidi kuitangaza nchi yetu kimataifa.
“Mhesjimiwa Spika, kwa upande wa sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa, Tanzania kupitia TMA ilifanya vizuri na kuchaguliwa katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa linalosimamia sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa (Intergovernmental Panel on Climate Change- IPCC).
“Hii ni fursa kwa Tanzania kuweza kushiriki katika Maamuzi ya Kimataifa kuhusu hali ya hewa pamoja na kupata usaidizi wa vifaa na utaalam.)” amesema Waziri mbarawa.
Ameongeza kuwq, katika kuhakikisha kuwa umma wa Watanzania unapata taarifa sahihi za hali ya hewa, TMA imeongeza wigo wa kuhabarisha umma kwa kusaini mikataba ya utangazaji wa taarifa za hali ya hewa na Redio tano (5) za jamii ambazo ni Jambo FM (Shinyanga), Harvest FM (Pwani), Inland FM (Mwanza), Revival FM (Manyara) na CGFM (Tabora) na kuwa na jumla ya vyombo vya habari 108 vinavyohusisha redio 80, Televisheni 17, magazeti matatu (3) na Televisheni Mtandao (on-line TV) nane (8).