Kituo cha chini ya ardhi cha kuhifadhi gesi nchini Ukraine kimeshambuliwa jana katika wimbi la karibuni la mashambulizi ya makombora ya Urusi kwenye vituo vya umeme.
Hayo yamejiri wakati maafisa wakirejesha huduma za umeme katika miji, kuamuru ununuzi wa umeme na kuweka utaratibu wa mgawo wa umeme ili kukabiliana na upungufu uliopo.
Shirika la nishati la serikali Naftogaz liliripoti kuhusu shambulizi hilo kwenye kituo cha kuhifadhi gesi, lakini likaongeza kuwa usambazaji wa gesi kwa watumiaji haukuathirika.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema juhudi za kujeresha umeme zinaendelea katika maeneo mbalimbali, huku kukiwa na changamoto kubwa katika mji wa pili kwa ukubwa Kharkiv. Urusi ilivishambulia vituo vya kuzalisha na kusambaza nishati vya Ukraine Ijumaa iliyopita, na kusababisha kukatikaumeme katika maeneo mengi. Vituo vya nishati katika maeneo matatu ya Ukraine pia vilishambuliwa mapema jana Jumapili.
Wakati huo huo, Urusi ilifyatulia Ukraine makombora 57 pamoja na droni mapema Jumapili, huku ikiushambulia mji mkuu Kyiv na mkoa wa Lviv ulioko magharibi mwa taifa hilo.
Jeshi la Ukraine hata hivyo liliharibu makombora 18 kati ya 29 na droni 25 kati ya 28, hii ikiwa ni kulingana na jeshi hilo kwenye taarifa yake kupitia mtandao wa Telegram.