Jeshi la Ukraine limesema kuwa kitengo chake cha ulinzi wa anga kimedungua droni 59 kati ya 116 zilizorushwa na Urusi usiku kucha. Jeshi hilo limeongeza kuwa lilipoteza mwelekeo wa droni 45 ambazo huenda zilianguka katika eneo lake.
Jeshi hilo pia limesema mashambulizi kadhaa yalilenga miundombinu ya umma.
Katika ujumbe kupitia mtandao wa Telegram, mkuu wa jeshi mjini Kyiv, Serhiy Popko, alisema ulikuwa usiku mwingine wa wasiwasi na kuongeza kuwa adui hataki kupunguza kasi ya mashambulizi ya anga dhidi ya Ukraine.
Tahadhari za uvamizi wa anga mjini Kyivzilidumu kwa zaidi ya masaa matano kabla ya jeshi la anga kutangaza usalama wa anga mwendo wa saa nane za usiku.
Shambulizi hilo lilifuatia mashambulizi ya Urusi dhidi ya Kyiv na miji mingine hapo jana ambayo yalijeruhi watu 17 katika mji mmoja katikati mwa Ukraine.
Mjini Kharkiv, eneo la mashariki mwa Ukraine linalopakana na Urusi, takribani watu 12 walijeruhiwa baada ya Urusi kufanya mashambulizi ya anga. Haya ni kwa mujibu wa ujumbe uliochapishwa katika mtandao wa Telegram na polisi.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikuweza kuthibitishwa kwa njia huru na shirika la habari la Reuters. Pia hakukuwa na jibu la haraka kutoka Urusi.
Korea Kusini imemuita balozi wa Urusi leo kukosoa uamuzi wa Korea Kaskazini wa kutuma maelfu ya wanajeshi kusaidia vita vya Urusi nchini Ukraine. Nchi hiyo imetaka kuondolewa kwa wanajeshi hao mara moja.
Kwa muda mrefu, Korea Kusini imekuwa ikidai Kaskazini yenye silaha za nyuklia inaipatia Urusi silaha kwa ajili ya matumizi nchini Ukraine,na kuelezea wasiwasi wake kuhusu kupelekwa kwa wanajeshi hao, hatua inayokuja baada ya kiongozi wa Kaskazini, Kim Jong Un, na Rais Vladimir Putin wa Urusi kutia saini mkataba wa kijeshi mwezi Juni.
Mbali na hayo, Yulia Navalnaya, mkewe marehemu kiongozi wa upinzani wa Urusi, Alexei Navalny, amesema kwamba siku moja atarejea Urusi na kugombea urais wakati rais wa nchi hiyo Vladimir Putin atakapoondoka madarakani. Haya yameripotiwa na shirika la habari la BBC.
Navalnaya amesema mpinzani wake wa kisiasa ni Putin na atafanya kila awezalo kuuangusha utawala wake haraka iwezekanavyo.