Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Andrii Sybiha ametoa wito wa msaada kutoka kwa jamii ya kimataifa kufuatia ripoti za madai kwamba wanajeshi wa Urusi wanawapiga risasi wafungwa wa kivita wa Ukraine.

Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa X Jumapili, Sybiha alisema kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai – ICC lazima itoe hati za kukamatwa kwa wale aliowaita ”wauaji na watesaji wa Urusi.”

Sybiha pia alitoa wito kwa waangalizi wa kimataifa na madaktari kupewa idhini ya kufikia kambi za wafungwa, na kuongeza kuwa Umoja wa Mataifa unaamini kuwa 95% ya wanajeshi wa Ukraine waliotekwa na Urusi wanakabiliwa na mateso.

Matamshi ya Sybiha yanakuja baada ya ripoti za kuuawa kwa wanajeshi tisa wa Ukraine waliokuwa wamejisalimisha wakati wa mapigano katika eneo la Kursk magharibi mwa Urusi baada ya kutumia risasi zao zote. Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ukraine, wanajeshi hao waliuawa papo hapo.

Kamishna wa Haki za Kibinadamu wa Ukraine Dmytro Lubinets, alizihimiza Jumapili Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu kuchukua hatua.

Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa X, Lubinets alisema, ”Urusi ni taifa la kigaidi linalokiuka sheria zote za vita. Jamii ya kimataifa haipaswi kupuuza uhalifu kama huo.”

Hivi majuzi, mwanajeshi mmoja wa Urusialikamatwa kwa madai ya kuwapiga risasi wanajeshi kadhaa wa Ukraine akiwa na wenzake mapema mwezi Septemba, baada ya wanajeshi hao kujisalamisha.

Kitendo hicho kilirekodiwa na droni ya upelelezi. Ofisi ya mwendesha mashitaka mjini Kiev, imesema inahafamu kuhusu zaidi ya visa 90 vya mauaji ya wafungwa wa kivita wa Ukraine.

Please follow and like us:
Pin Share