Urusi imeapa siku ya Jumamosi kulipiza kisasi baada ya kuishutumu Ukraine kushambulia eneo la mpakani la Belgorod kwa kuvurumisha makombora ya masafa marefu ya ATACMS yaliyotolewa na Marekani.

“Hatua hizi za serikali ya Kyiv, ambayo inaungwa mkono na washirika wa Magharibi, itakabiliwa na kisasi,” ilisema taarifa ya wizara ya ulinzi ya Urusi ikiishutumu Ukraine kwa kulenga eneo la mpakani la Belgorod kwa makombora ya masafa marefu.

Hata hivyo Moscow imesema ilifanikiwa kuyadungua makombora manane ya ATACMS na kuonya kwamba matumizi yake yanaweza kuzua shambulio la kombora la masafa marefu lenye uwezo mkubwa katikati mwa mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.

Mwishoni mwa mwaka jana, rais anayeondoka wa Marekani Joe Biden aliiruhusu Ukraine kutumia makombora hayo dhidi ya Urusi, hatua ambayo ililaaniwa na Kremlin iliyosema inavichochea vita hivyo.

“Mifumo ya ulinzi wa anga iliharibu makombora manane yaliyovurumishwa ya ATACMS pamoja na droni 72,” Hii ikiwa ni kulingana na wizara ya ulinzi ya Urusi. Makombora hayo yana uwezo wa kusafiri hadi kilometa 300.

Wizara hiyo pia ilisema kuwa imechukua udhibiti wa kijiji cha Ukraine cha Nadiia, mojawapo ya maeneo machache yaliyosalia kwenye udhibiti wa Kyiv katika eneo la mashariki la Lugansk.