URUSI imesema vikosi vyake vilifanya mashambulizi makali dhidi ya vikosi vya Ukraine katika mkoa wake wa magharibi wa Kursk, ambako jeshi la Ukraine liliripoti ongezeko la mapigano katika masaa 24 yaliyopita.
Kwa mujibu wa mkuu wa majeshi wa Ukraine, siku ya Jumanne (Januari 7) kulitokea makabiliano 218 kwenye maeneo yote ya mstari wa mbele ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita, ambapo kwenye mkoa wa Kursk pekee jeshi hilo limekabiliana na mashambulizi 94 ya Urusi.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, kamandi ya kikosi maalum cha Ukraine ilichapisha taarifa kwamba wanajeshi 13 wa Korea Kaskazini waliuawa, ingawa shirika la habari la Ujerumani (dpa) lilishindwa kuthibitisha taarifa hiyo kupitia vyanzo huru.
Mnamo mwishoni mwa wiki, Kiev ilianzisha tena uvamizi wa kushitukiza kwenye mkoa huo ulio magharibi mwa Urusi, ambapo kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Vita ya Marekani (ISW), vikosi vya Ukraine vimesonga mbele kuelekea kaskazini mashariki mwa mji wa Sudzha.
ISW imesema hatua hiyo inaashiria kuwapo kwa operesheni iliyopangwa kwenye mkoa huo na pia matayarisho ya mashambulizi kwenye maeneo mengine ya mstari wa mbele, ikinukuu taarifa za data kutoka picha zilizochapishwa mtandaoni.