Urusi na Ukraine zimebadilishana mamia ya wafungwa wa kivita, imesema Wizara ya Ulinzi ya Urusi.
Katika makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu, Urusi imesema imetoa wanajeshi 150 wa Ukraine waliokuwa mateka kwa idadi sawa ya wanajeshi wa Urusi.
Wanajeshi wa Urusi walioachiliwa walipelekwa Belarus, mshirika wa Urusi, na wanapewa matibabu na kuwasiliana na familia zao.
Ukraine bado haijatoa tamko lolote. Vilevile Ukraine haichapishi idadi ya wafungwa wa kivita wanaoshikiliwa na Urusi, lakini inadhaniwa kuwa ni zaidi ya 8,000.
Urusi imepata mafanikio makubwa katika medani ya vita mwaka huu, jambo ambalo limezusha hofu huenda idadi ya wanajeshi wa Ukraine wanaokamatwa ikaongezeka.