Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema kuwa sio rahisi kufikia makubaliano na Marekani kuhusu vipengele muhimu vya makubaliano ya amani yanayoweza kusitisha vita nchini Ukraine.

Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye anasema anataka kukumbukwa kama mleta amani, amekuwa akisema mara kwa mara kuwa anataka kufikia kikomo cha umwagaji damu kwa vita vya miaka mitatu nchini Ukraine, ingawa mwafaka bado haujapatikana.

Sasa Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema sio rahisi kufikia vipengele muhimu vya makubaliano. Lavrov amesema hayo katika mahojiano na gazeti la Kommersant alipoulizwa kama Moscow na Washington zimekubaliana kuhusu masuala kadhaa ya mwafaka unaosakwa wa amani. Lakini amesema majadiliano bado yanaendelea.

Siku ya Jumanne, mjumbe maalum wa Trump alisema kuwa rais wa Urusi Vladmir Putin yuko tayari kwa makubaliano ya “amani ya kudumu” na Ukraine.