Urusi imeanza maandalizi ya mazoezi ya makombora karibu na Ukraine yakiiga matumizi ya silaha za kimkakati za nyuklia ili kukabiliana na “vitisho” vya maafisa wa nchi za Magharibi.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema kauli za hivi majuzi za Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron ni “duru mpya kabisa ya kuongezeka kwa mvutano”.
Wiki iliyopita, Bw Macron alikataa kuondoa uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa Ufaransa, iwapo Ukraine itawaomba kufanya hivyo, huku David Cameron akisema kuwa Ukraine ina haki ya kutumia silaha za Uingereza kwa mashambulizi ndani ya Urusi.
Siku ya Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilisema kwamba “hisia kali yenye chuki” ya David Cameron inapingana na hakikisho la hapo awali la Uingereza kwamba makombora ya masafa marefu yaliyotumwa Ukraine hayatatumika katika ardhi ya Urusi na kumaanisha kwamba Uingereza ilikuwa “mshirika wa mzozo” huo.
Wizara hiyo iliongeza kuwa majibu ya mashambulizi ya Ukraine kwa kutumia silaha za Uingereza dhidi ya Urusi yanaweza kuhusisha kulenga vituo na vifaa vyovyote vya kijeshi vya Uingereza katika eneo la Ukraine na kwingineko.
Pia ilisema kwamba kauli ya Bw Macron kuhusu uwezekano wa kutumwa kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini Ukraine inaweza kuchukuliwa kuwa “tayari kwa makabiliano ya moja kwa moja na Urusi”.
Mabalozi wa Uingereza na Ufaransa walioko Moscow waliitwa Jumatatu.